Nafasi Ya Matangazo

July 27, 2026

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Ndugu Prisca Burton Lwangili kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwenye hafla iliyofanyika Ikulu ya Tunguu Zanzibar, tarehe 27 Julai, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Dkt. LatifaMohammed Khamis kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano kwenye hafla iliyofanyika Ikulu ya Tunguu Zanzibar, tarehe 27 Julai, 2026.

Viongozi  Wateule wakiapa kiapo cha uadilifu kwa Viongozi wa Umma kwenye hafla iliyofanyika Ikulu ya Tunguu Zanzibar, tarehe 27 Julai, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi wateule kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, ushirikiano na bila upendeleo, wakitanguliza huduma kwa wananchi na maslahi ya Taifa. Rai hiyo ameitoa leo Ikulu, Tunguu, Zanzibar, baada ya kuwaapisha Naibu Makatibu Wakuu wawili na kushuhudia viongozi wengine wanne wakila Kiapo cha Uadilifu kwa Viongozi wa Umma. Amesema uteuzi huo unaonesha imani ya Serikali kwa viongozi hao, hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa bidii, weledi na kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.

Rais Dkt. Samia pia ameiagiza Ofisi ya Makamu wa Rais kuimarisha usimamizi wa masuala ya Muungano na kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinatatuliwa kwa ushirikiano ili kuendelea kuulinda na kuuimarisha Muungano. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa mazingira kwa kushirikiana katika utekelezaji wa programu za uhifadhi na kukabiliana na changamoto zinazotishia mazingira na ustawi wa Taifa.

Katika kuimarisha utendaji wa Serikali, Rais ameitaka Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuweka mazingira bora yatakayowawezesha watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Kwa upande wa sekta ya uchukuzi, ameelekeza kuongeza kasi ya ujenzi na usimamizi wa miradi ya reli, barabara, bandari na meli, sambamba na kutathmini fursa za kupanua biashara ya anga ya Shirika la Ndege la Tanzania.

Vilevile, Rais Dkt. Samia ameitaka Wizara ya Katiba na Sheria kuendelea kuimarisha upatikanaji wa haki nchini kwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa kampeni za msaada wa kisheria ili huduma hizo ziwafikie wananchi wengi zaidi na kuwawezesha kupata haki zao kwa wakati. Aidha, ameitaka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuimarisha ukuzaji wa biashara pamoja na usimamizi wa maonesho ya biashara nchini.

Kwa upande wa uhifadhi wa maliasili, Rais ameliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuimarisha usimamizi na ulinzi wa hifadhi za wanyamapori na rasilimali za utalii, akisisitiza kuwa taasisi hiyo ina nafasi muhimu katika kulinda na kukuza sekta ya utalii nchini. Pia amelitaka Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuendelea kuimarisha nafasi yake kama chombo cha Serikali na sauti ya Taifa kwa kuboresha maudhui, kuongeza ufanisi wa utendaji na kuendeleza weledi wa watumishi wake.

Walioapishwa ni Dkt. Latifa Mohammed Khamis, aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya Muungano, na Bi. Prisca Burton Lwangili, aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Viongozi wengine walioapa Kiapo cha Uadilifu kwa Viongozi wa Umma ni Bw. Ephraim Balozi Mafuru, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE); Bw. Salum Nassor Mnuna, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA); Bw. Massana Gibril Mwishawa, Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA); na Bi. Asha Dachi Mbaruk, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).









Posted by MROKI On Monday, July 27, 2026 No comments

Babati, Manyara
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Babati ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mhe. Remidius Mwema, amesisitiza kuwa uhifadhi endelevu wawanyamapori ni nguzo muhimu ya ukuaji wa sekta ya utalii, uwekezaji na maendeleo ya jamii, huku akiwataka askari wahifadhi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uzalendo.

Mhe. Mwema ametoa kauli hiyo  alipofungua rasmi mafunzo maalum ya siku tano kwa askari wahifadhi wanaotekeleza majukumu katika Ikolojia ya Tarangire–Manyara, hususani maeneo yenye mtawanyiko wa wanyamapori na ushoroba wa _“Kwakuchinja.”_

Mafunzo hayo yaliandaliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Babati kwa kushirikiana na Chem Chem Association(CCA) na kuwakutanisha askari wahifadhi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Hifadhi ya Taifa ya Tarangire (TANAPA), Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Burunge pamoja na Chem Chem Association, mafunzo hayo yalifanyika kuanzia Julai 20 hadi 25, 2026.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhe. Mwema alisema Serikali inaendelea kuwekeza na kuimarisha uwezo wa watumishi wa sekta ya uhifadhi ili kuhakikisha rasilimali za wanyamapori zinalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

_"Tunashuhudia ukuaji wa sekta ya utalii, uwekezaji katika vitalu vya uwindaji, ujenzi wa hoteli za kitalii na maendeleo ya jamii yanayotokana na uwepo wa rasilimali hizi, Wanyamapori wakitoweka, fursa hizo pia zitatoweka. Hivyo, ni muhimu kuendelea kuimarisha mapambano dhidi ya ujangili pamoja na kujenga ushirikiano madhubuti na wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi ili wawe walinzi na mabalozi wa uhifadhi,"_  Alisema Mhe. Mwema.

Alieleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali na wadau wa uhifadhi kwa lengo la kuongeza maarifa, ujuzi na weledi wa askari wahifadhi katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazokabili maeneo yaliyohifadhiwa.

Aidha, amesema ushirikiano kati ya taasisi za uhifadhi, wadau wa maendeleo na wananchi ni msingi wa kuhakikisha shoroba za wanyamapori zinaendelea kuwa salama na kuchangia ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya utalii.

Mafunzo hayo pia yalihusisha  wakufunzi kutoka nchini Marekani, ambao walishiriki kutoa uzoefu na mbinu za kisasa za kimataifa katika ulinzi na usimamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa askari wahifadhi katika kutekeleza majukumu yao.

Katika hafla hiyo, Mhe. Mwema aliambatana na Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Babati pamoja na wataalamu kutoka TANAPA, TAWA, Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Burunge na Halmashauri ya Wilaya ya Babati.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuimarisha uwezo wa askari wahifadhi katika kulinda Ikolojia ya Tarangire–Manyara, eneo lenye umuhimu mkubwa kwa uhifadhi wa bioanuwai, maendeleo ya utalii na ustawi wa uchumi wa Taifa. 








Posted by MROKI On Monday, July 27, 2026 No comments

July 26, 2026

 




Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga amewakabidhi wadau wa usalama wa Mji wa Tunduma, Wilaya ya Momba mkoani Songwe vyeti vya pongezi kwa kutambua mchango wao mkubwa katika kuimarisha ulinzi na usalama, pamoja na kujitolea kuboresha miundombinu ya Kituo cha Polisi Tunduma ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vyeti hivyo iliyofanyika Julai 26, 2026, SACP Senga aliwashukuru wadau hao kwa moyo wao wa uzalendo na ushirikiano wanaouonesha kwa Jeshi la Polisi. Waliotunukiwa vyeti hivyo ni Kessy Kahise aliyetoa vifaa vya usafi, Abel Waya aliyetoa shilingi milioni nne kwa ajili ya ununuzi wa pampu na ujenzi wa kisima cha maji katika Kituo cha Polisi Tunduma, pamoja na Alex Ngasala, Msaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Tunduma aliyemwakilisha Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, ambaye alitoa shilingi milioni nne kwa ajili ya ujenzi wa kisima hicho na shilingi laki tano kwa ajili ya ununuzi wa malighafi za ujenzi wa choo kinachoendelea kujengwa kituoni hapo.

Kwa upande wao, wadau hao waliipongeza kazi inayofanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe na kueleza kuwa wamehamasishwa na dhana ya Polisi Jamii, jambo lililowafanya kutambua kuwa ulinzi na usalama ni jukumu la kila mwananchi. Walisema ushirikiano huo umewapa hamasa ya kuendelea kuchangia maendeleo ya Jeshi la Polisi na kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za kiusalama kwa wananchi.

Naye Mkuu wa Polisi Wilaya ya Momba, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Bhoke Simango aliwataka wadau wengine kuiga mfano huo kwa kujitokeza kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya Jeshi la Polisi, ikiwemo kukamilisha ujenzi wa choo na miradi mingine katika Kituo cha Polisi Tunduma. Alisema hatua hiyo ni matokeo ya mafanikio ya dhana ya Polisi Jamii, ambayo imeendelea kuimarisha ushirikiano, kujenga imani kati ya wananchi na Jeshi la Polisi, na kuongeza ari ya wananchi kujitolea kushiriki katika kulinda amani, usalama na maendeleo ya jamii.
Posted by MROKI On Sunday, July 26, 2026 No comments
Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limeungana na wananchi wa Mji Mdogo wa Mlowo, Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Songwe kufanya zoezi la usafi katika eneo la Stendi Mpya ya Mabasi ya Mlowo ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha usafi wa mazingira, kuimarisha afya ya jamii na kuendelea kujenga ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi.

Zoezi hilo la usafi lililofanyika Julai 26, 2026 katika Stendi Mpya ya Mabasi ya Mlowo Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe na kuongozwa na Mkuu wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Maria Kway, alisema kuwa ushirikiano waliouonesha katika kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na salama kwa wafanyabiashara, wasafiri na wananchi wote wanaotumia eneo hilo uendelee na uwe utamaduni wa maisha ya kila siku.

Aidha, ACP Kway aliwahimiza wananchi hao kuzingatia usafi katika maeneo wanayofanyia biashara kwa kuhakikisha wanakuwa na vifaa vya kuhifadhia taka na kuweka utaratibu wa kufanya usafi kwa pamoja kila wiki ili kudumisha mazingira safi na yenye afya.

Mwisho, ACP Kway aliwakumbusha wananchi hao kuendelea kutii sheria za nchi bila kushurutishwa kwa kujiepusha na vitendo vya uhalifu, badala yake waelekeze nguvu zao katika kufanya kazi halali na kujipatia kipato cha halali, huku akiwasisitiza kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe katika kuzuia na kutokomeza uhalifu ili kudumisha amani na usalama wa Mkoa wa Songwe.






Posted by MROKI On Sunday, July 26, 2026 No comments

July 25, 2026

SONGWE
Wananchi wa Kata ya Mkwajuni, Wilaya na Mkoa wa Songwe, wametakiwa kufuata sheria za usalama barabarani, ili kupunguza ajali za barabarani katika eneo  hilo.

Akizungumza na wananchi Julai 25, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mheshimiwa Jabiri Makame alisema wakati wa ziara yake katika kampeni ya Serikali Nyumbani Kwako iliyofanyika katika kata hiyo. amepita katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo na kujionea namna wananchi wanavyothamini kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe, huku akisisitiza kuwa ni wajibu wa kila mtumiaji wa barabara kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili kulinda maisha na mali za wananchi.

Aidha Mh. Makame aliwataka askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani kuendelea kusimamia sheria kwa weledi, uadilifu na bila upendeleo, huku wakichukua hatua za kisheria dhidi ya wote watakaobainika kukiuka sheria na kanuni za usalama barabarani.

Pia Mh Makame alisema kuna mambo matatu ya msingi yatakayosaidia kupunguza ajali za barabarani ambazo ni kuzingatia alama za usalama barabarani, kuendelea kutoa elimu kwa madereva wa bodaboda na watumiaji wengine wa barabara kuzingatia matumizi salama ya  barabara, pamoja na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wote wanaokiuka sheria na taratibu za usalama barabarani.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga, aliwataka wasafirishaji wote kuzingatia sheria za usalama barabarani kwa kuvaa kofia ngumu (helmet) wakati wote, kuepuka kubeba mizigo au abiria kinyume cha sheria, pamoja na kuendesha kwa mwendo unaoruhusiwa, hususan katika maeneo ya makazi, akibainisha kuwa kufanya hivyo kunalinda maisha yao, familia na jamii kwa ujumla.

Akihitimisha, Kamanda Senga aliwataka madereva wote kuachana na tabia ya kuendesha vyombo vya moto wakiwa wametumia pombe au vilevi vya aina yoyote, akieleza kuwa vitendo hivyo ni hatari kwa maisha ya dereva na watumiaji wengine wa barabara, huku akisisitiza kuwa kila mmoja anapaswa kuchukua tahadhari ili kulinda usalama wake na wa vizazi vijavyo.










Posted by MROKI On Saturday, July 25, 2026 No comments





RUKWA
Wananchi, Wafugaji pamoja na Wafanyabiashara wa Mifugo katika mnada wa mifugo uliopo katika Kijiji cha Kisumba, Kata ya Matanga, Wilaya ya Sumbawanga mjini Mkoani Rukwa wametakiwa kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi wakiaswa kuwa hiyo sio njia ya kumaliza migogoro baina yao.

Hayo yameelezwa leo Julai 25, 2026 na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Nchini (STPU) Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Simon Pasua ambapo amewataka Wananchi hao kuripoti matukio ya uhalifu katika vituo vya Polisi kuanzia ngazi ya Kata na sio kujichukulia sheria mkononi, kwani kwa kufanya hivyo kunachangia kuongezeka kwa matukio hayo.

Aidha Kamanda Pasua amewataka Wananchi hao kuonyesha ushirikiano katika vyombo vya sheria ili kufanikisha kesi za uhalifu, huku akiwaagiza wenyeviti wa Vijiji kuwapa Wafugaji, barua za utambulsho wa uhalali wa umiliki mifugo pindi wapelekapo mifugo yao katika minada.

Naye Mkaguzi Kata wa Kata hiyo (INSP) Fatuma Mkumbo amesema Jeshi la Polisi katika Kata hiyo litaendelea kuimarisha ulinzi katika minada yote ya Mifugo, huku akitoa rai kwa Wafugaji kuacha kuwatumia watoto katika shughuli za uchungaji mifugo.
Posted by MROKI On Saturday, July 25, 2026 No comments

Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Mbeya Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Notker Kilewa ameitaka jamii kuwakumbuka watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.

Hayo amezungumza Julai 25, 2026 alipowaongoza Maafisa, Wakaguzi na Askari wa Kikosi cha usalama barabarani Mkoani humo kutembelea na kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto wanaolelewa katika kituo cha Nuru Orphans Center kilichopo Uyole Jijini Mbeya.

Aidha SSP Kilewa alisema kuwa, Jeshi la Polisi kama sehemu ya jamii limekuwa likifanya kazi zake kwa kushirikiana na jamii ili kuzuia uhalifu na ajali za barabarani, limetembelea kituo hicho na kutoa vitu mbalimbali kama sehemu ya kurejesha kwa jamii na kama sehemu ya kuguswa na watoto yatima.

"Nalaani vitendo vya baadhi ya wazazi kutupa na kutelekeza watoto na kusababisha wengine kupoteza maisha, wengine kuishi katika mazingira magumu na hata kukosa mahitaji muhimu, haki zao za msingi, nitoe wito kwa jamii kutembelea kituo hiki na kutoa msaada wa mahitaji kwa watoto" alisema SSP Kilewa.

Naye, Meneja wa Kituo hicho Bi. Mary Emily amesema kuwa kituo hicho kilianza mwaka 2006 na kinapokea watoto kuanzia umri wa mwaka 0 na kuendelea, kituo kinapata watoto kutoka Ustawi wa Jamii na hadi sasa kituo kina jumla ya watoto 39.

Vilevile, Bi. Mary amelishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kuwafikiria na kutoa msaada wa vitu mbalimbali ambavyo vimegusa mahitaji yao. Pia Bi. Mary ametoa wito kwa jamii kuendelea kuwakumbuka watoto wanaoishi katika mazingira magumu na yatima.

Kwa upande wake, mmoja wa watoto wanaolelewa katika kituo hicho tangu mwaka 2006 Melania Nuru amelishukuru Jeshi la Polisi kwa msaada na ameiomba jamii kuwasaidia watoto wenye mahitaji. Kwa sasa amemaliza kidato cha nne na anatarajia kuendelea na masomo ya elimu ya juu, hivyo anaiomba jamii kumsaidia mahitaji yatakayomsaidia kukidhi masomo yake.










Posted by MROKI On Saturday, July 25, 2026 No comments
  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo