Wananchi, Wafugaji pamoja na Wafanyabiashara wa Mifugo katika mnada wa mifugo uliopo katika Kijiji cha Kisumba, Kata ya Matanga, Wilaya ya Sumbawanga mjini Mkoani Rukwa wametakiwa kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi wakiaswa kuwa hiyo sio njia ya kumaliza migogoro baina yao.
Hayo yameelezwa leo Julai 25, 2026 na Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Nchini (STPU) Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Simon Pasua ambapo amewataka Wananchi hao kuripoti matukio ya uhalifu katika vituo vya Polisi kuanzia ngazi ya Kata na sio kujichukulia sheria mkononi, kwani kwa kufanya hivyo kunachangia kuongezeka kwa matukio hayo.
Aidha Kamanda Pasua amewataka Wananchi hao kuonyesha ushirikiano katika vyombo vya sheria ili kufanikisha kesi za uhalifu, huku akiwaagiza wenyeviti wa Vijiji kuwapa Wafugaji, barua za utambulsho wa uhalali wa umiliki mifugo pindi wapelekapo mifugo yao katika minada.
Naye Mkaguzi Kata wa Kata hiyo (INSP) Fatuma Mkumbo amesema Jeshi la Polisi katika Kata hiyo litaendelea kuimarisha ulinzi katika minada yote ya Mifugo, huku akitoa rai kwa Wafugaji kuacha kuwatumia watoto katika shughuli za uchungaji mifugo.











0 comments:
Post a Comment