Nafasi Ya Matangazo

July 27, 2026

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Ndugu Prisca Burton Lwangili kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwenye hafla iliyofanyika Ikulu ya Tunguu Zanzibar, tarehe 27 Julai, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimuapisha Dkt. LatifaMohammed Khamis kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano kwenye hafla iliyofanyika Ikulu ya Tunguu Zanzibar, tarehe 27 Julai, 2026.

Viongozi  Wateule wakiapa kiapo cha uadilifu kwa Viongozi wa Umma kwenye hafla iliyofanyika Ikulu ya Tunguu Zanzibar, tarehe 27 Julai, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi wateule kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, ushirikiano na bila upendeleo, wakitanguliza huduma kwa wananchi na maslahi ya Taifa. Rai hiyo ameitoa leo Ikulu, Tunguu, Zanzibar, baada ya kuwaapisha Naibu Makatibu Wakuu wawili na kushuhudia viongozi wengine wanne wakila Kiapo cha Uadilifu kwa Viongozi wa Umma. Amesema uteuzi huo unaonesha imani ya Serikali kwa viongozi hao, hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa bidii, weledi na kuwahudumia wananchi kwa ufanisi.

Rais Dkt. Samia pia ameiagiza Ofisi ya Makamu wa Rais kuimarisha usimamizi wa masuala ya Muungano na kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinatatuliwa kwa ushirikiano ili kuendelea kuulinda na kuuimarisha Muungano. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa mazingira kwa kushirikiana katika utekelezaji wa programu za uhifadhi na kukabiliana na changamoto zinazotishia mazingira na ustawi wa Taifa.

Katika kuimarisha utendaji wa Serikali, Rais ameitaka Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuweka mazingira bora yatakayowawezesha watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Kwa upande wa sekta ya uchukuzi, ameelekeza kuongeza kasi ya ujenzi na usimamizi wa miradi ya reli, barabara, bandari na meli, sambamba na kutathmini fursa za kupanua biashara ya anga ya Shirika la Ndege la Tanzania.

Vilevile, Rais Dkt. Samia ameitaka Wizara ya Katiba na Sheria kuendelea kuimarisha upatikanaji wa haki nchini kwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa kampeni za msaada wa kisheria ili huduma hizo ziwafikie wananchi wengi zaidi na kuwawezesha kupata haki zao kwa wakati. Aidha, ameitaka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuimarisha ukuzaji wa biashara pamoja na usimamizi wa maonesho ya biashara nchini.

Kwa upande wa uhifadhi wa maliasili, Rais ameliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuimarisha usimamizi na ulinzi wa hifadhi za wanyamapori na rasilimali za utalii, akisisitiza kuwa taasisi hiyo ina nafasi muhimu katika kulinda na kukuza sekta ya utalii nchini. Pia amelitaka Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuendelea kuimarisha nafasi yake kama chombo cha Serikali na sauti ya Taifa kwa kuboresha maudhui, kuongeza ufanisi wa utendaji na kuendeleza weledi wa watumishi wake.

Walioapishwa ni Dkt. Latifa Mohammed Khamis, aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya Muungano, na Bi. Prisca Burton Lwangili, aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Viongozi wengine walioapa Kiapo cha Uadilifu kwa Viongozi wa Umma ni Bw. Ephraim Balozi Mafuru, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE); Bw. Salum Nassor Mnuna, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA); Bw. Massana Gibril Mwishawa, Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA); na Bi. Asha Dachi Mbaruk, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).









Posted by MROKI On Monday, July 27, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo