Nafasi Ya Matangazo

July 26, 2024









🔴Zege yapigwa chapuo, magogo kuzuiwa

SERIKALI kupitia Wizara ya Madini, Tume ya Madini imepata mwarobaini wa kupunguza majanga kwenye migodi kwa kuwaelimisha wachimbaji wadogo kutumia zege kwenye kingo za miamba badala ya magogo.

Akizungumza leo Julai 26, 2024 katika mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa Tume ya Madini kutoka Idara ya Ukaguzi  wa Migodi na Mazingira yaliyofanyika jijini Dodoma, kwa niaba ya Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Meneja wa Mazingira Mhandisi Ephraim Mushi amesema njia mbadala ya zege kwa wachimbaji wadogo itasaidia kuondoa tatizo la ajali migodini kwa watu kupoteza maisha na wengine kuwa walemavu.

“Wachimbaji wadogo wanatumia magogo maarufu kama matimba kwa kuweka kingo kwenye miamba, sasa njia hii imeonekana sio salama kwa uchimbaji  mdogo kwa maana yanakaa baada ya muda yanaoza, yanaanguka na kusababisha ajali kwenye migodi,”amesema Mhandisi Mushi na kuongeza,
 
“Lakini pia imeonekana wachimbaji wadogo wanatumia sana haya magogo ambayo kimsingi yanaleta uhabiribifu wa mazingira, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini tumeona kuna haja ya kuja na njia mbadala ili kupunguza au kuondoa kabisa ajali migodini.


“Idara ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, elimu hii tutaenda kuitoa kwa wachimbaji wadogo, namna ya kukinga  na zege ili miamba inapoanguka isije kuleta madhara kwa wachimbaji, wakiweza kwenda na huu mfumo uzalishaji utaongezeka na utakuwa na tija na vifo vya wachimbaji vitapungua na mapato ya serikali yataongezeka,”amesisitiza Mushi.


Naye Mjiolojia Mwandamizi Fabian Mshai akitoa shukrani kwa wakufunzi kwa niaba ya washiriki amesema mafunzo waliyoyapata yamejenga   uwezo zaidi, ari na nguvu mpya kwa wakaguzi wa migodi na mazingira katika kutekeleza majukumu yao.


Amesema  kuwa ili uchimbaji wa madini uwe endelevu lazima kuwe na  usalama, kusiwe na ajali na utunzaji wa  mazingira  kwa manufaa ya kizazi cha sasa na cha baadaye na ina umuhimu katika kukuza sekta ya madini nchini.

“Elimu hii tutaishusha chini kwa wachimbaji wadogo sambamba na kukagua hali ya usalama mara  kwa mara ili kuwasaidia wachimbaji kuepuka ajali wakati wa utekelezaji wa shughuli zao.

Mafunzo hayo yalianza rasmi Jumatatu Julai 22 hadi leo Julai 26, 2024  ambapo mawasilisho mbali mbali yaliwasilishwa na wakufunzi   Mhandisi Gervas Wiliam kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mhandisi Selemani Msangi kutoka Kampuni ya HETAMIS, Mhandisi Japhet Mmary kutoka Shanta Mining Co. Ltd, Fikiri Juma kutoka Bulyanhulu Gold Mine na  Fey Kidee kutoka Kidee Mining (T) Ltd
Posted by MROKI On Friday, July 26, 2024 No comments




Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka viongozi kushirikiana na kuheshimiana ili kuchochea maendeleo ya watu na sio kukwamisha maendeleo

Dkt. Biteko amesema hayo wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Msangila, Kata ya Runzewe Magharibi, Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.

Ameongeza kuwa maono ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuwaona Watanzania wanapata maendeleo katika nyanja za kiuchumi na kijamii nchini na ndiyo sababu ya kusukuma maendeleo kwa haraka katika kipindi chake cha uongozi ndani ya miaka mitatu ambapo amefanya kila kitu kwa viwango vya juu.

"Sisi wasaidizi wake anatuagiza wakati wote tukawasikilize wananchi kero zao, tusikilize shida zao na mimi nimekuja hapa kuwaambia Rais Samia anawapenda, anawathamini  ataleta maendeleo zaidi," ameongeza Dkt. Biteko.

"Mimi ni Waziri ninayeshughulika na Sekta ya Nishati, tulikua na shida ya umeme kwenye nchi yetu,  umeme unakatika kwa sababu umeme mdogo mahitaji ni mengi, Mama Samia amesimamia, sasa hatuna mgawo wa umeme na tunaendelea kuimarisha miundombinu ya umeme," amesisitiza Dkt. Biteko.

"Mnaona tunazungumza  fedha kuja kujenga barabara, kujenga madarasa, tunazungumza hapa kukamilisha zahanati na tunazungumza hapa kuongeza visima vya maji, yote haya yanasukumwa na mpendwa wetu Rais Samia ili kutuletea maendeleo," amesema Dkt. Biteko.

Ameeleza kuwa, Rais Samia amefungua barabara katika wilaya ya Bukombe ikiwa na km 256 pekee, hadi sasa imeongezeka kufikia km 1400 na upatikanaji wa maji ulikuwa asilimia 20 tu lakini sasa kila sehemu wananchi wanapata huduma hiyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigella amewahimiza wananchi kuhakiki vitambulisho vya mpigakura ili kupata haki ya kuwachagua viongozi wanaowataka.

Naye, Diwani wa Kata ya Runzewe Magharibi, John Nguhi ameshukuru kwa fedha za maendeleo zilizotumika kuboresha huduma za Jamii na miundombinu ya Barabara.
Posted by MROKI On Friday, July 26, 2024 No comments










Tanzania na Visiwa vya Comoro zimesaini Hati nne za Makubaliano kwenye kilele cha Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Comoro uliofanyika tarehe 24 Julai,2024 jijini Dar es Salaam. 

Hati zilizosainiwa katika kikao hicho zinazojumuisha nyanja za; Ushirikiano wa Kidiplomasia, Afya, Biashara na Viwanda na Teknolojia ya Habari. Utiaji saini hati hizo umeshuhudiwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro anayeshughulikia Nchi za Kiarabu, Nchi zinazozungumza Kifaransa, Diaspora na Mtangamano wa Afrika Mhe. Mohamed Mbae.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo wa kihistoria, Waziri Tax ameelezea umuhimu wa kusainiwa kwa hati hizo kuwa itawezesha pande hizo mbili kuwa na ushirikiano ulio katika mpangilio mzuri katika nyanja husika na hivyo kuleta tija zaidi.

"Pamoja na kutia saini Hati za Makubaliano pia tumekubaliana kuendelea kushirikiana katika maeneo mengine mengi ikiwemo miondombinu, nishati, ulinzi na usalama, uchumi wa buluu, utalii, utamaduni, sanaa na michezo na Maendeleo ya vijana". Ameeleza Dkt. Tax


Naye Mhe. Mbae ameeleza kufurahishwa kwake na kufanyika kwa mkutano huo wa JPC na kuongeza kuwa mkutano huo ni kiungo muhimu katika kuendelea kukuza na kuimarisha uhusiano na kati ya Tanzania na Comoro.

Ameipongeza Tanzania kwa kuandaa mkutano huo na hivyo kuonesha dhamira ya dhati ya Tanzania katika kuendelea kushirikiana na Comoro.

Mbali na kusainiwa kwa Hati hizo Mawaziri hao wameridhishwa na kupongeza hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa makubaliano na maamuzi mbalimbali yaliyofikiwa kwa pamoja kati ya pande hizo mbili tangu kusainiwa kwa Mkataba wa Jumla wa Ushirikinao mwaka 2009. 

Vilevile mkutano huo umejadili na kuweka mikakati ya namna ya kuendelea kukuza biashara baina ya pande hizo mbili. Mikakati hiyo pamoja na mambo mengine italenga kuwahimiza sekta binafsi kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili na kuchangamkia fursa za kibiashara zilizopo na zile zinazotokana na Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) na Eneo Huria la Biashara la SADC.

Akizungumzi kuhusu mkutano huo Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Saidi Yakubu ameeleza kuwa, Comoro ni mshirika muhimu wa Tanzania katika biashara, ambapo kwa mwaka 2023 Tanzania iliuza nchini humo bidhaa zenye thamani ya shilingi bilioni 148. 

Ameongeza kusema kuwa makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano huo sio tu yataongeza ushirikiano wa kidiplomasia bali yanatarajiwa kuongeza kiasi cha bidhaa ambazo Tanzania inaingiza nchini humo. 

Katika mkutano huo ujumbe wa Tanzania umejumuisha wataalamu na watendaji kutoka sekta mbalimbali na umeongozwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Tax, ambaye pia aliongoza mkutano huo kwa kushirikiana na mwenyekiti mwenza Waziri Mbae wa Comoro.
Posted by MROKI On Friday, July 26, 2024 No comments






Na Mwandishi Wetu
TAASISI na Mashirika ambayo yana malimbikizo ya ada za ushiriki wa michezo ya wafanyakazi zimeombwa kulipia ada ya ushiriki mapema ili kufanikisha michezo hiyo inayofanyika kila mwaka wakati wa Siku Kuu ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo ya Mei Mosi Taifa Roselyne Mathew Massam kwenye kikao cha Viongozi Vilabu vya michezo ambvyo vipo kwenye Mashirikisho ya Michezo nchini ambao wamekutana kufanya tathimini ya michezo hiyo iliyofanyika mwezi Aprili mwaka huu Jijini Arusha.

Massam, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma (SHIMUTA), amesema kuwa ucheleweshaji wa ulipaji wa ada unakwamisha ufanisi wa michezo hiyo na kusababisha kushindwa kugharimia gharama za michezo hiyo ikiwemo kulipia viwanja vizuri vyenye ubora.

Massam amesema Kamati hiyo ya Michezo ya Mei Mosi inaundwa na mashirikisho ya SHIMIWI,  SHIMUTA, SHIMISEMITA na BAMATA ambapo  katika tathimini hiyo kamati hiyo imeweka mkakati wa kuongeza timu zitakazozoshiriki mashindano  hayo mwakani ambapo mwaka huu Jumla ya timu 56 zimeshiriki ukilinganisha na timu 33 zilizoshiriki mwaka jana 2023.

Amesema kuwa Kamati imekuwa na utaratibu wa kufanya tathimini  ili kutambua changamoto zilizojitokeza zisijirudie tena hivyo kuboresha michezo ijayo iwe mizuri zaidi .

Massam, amesema kamati hiyo inaendelea kuhamasisha Wizara, Idara, taasisi, mashirika ya umaa na sekta binafsi  kuhakikisha kila mfanyakazi anafanya mazoezi na kushiriki michezo hiyo kwa ajili ya kuimarisha afya.

Katibu Mkuu wa Kamati ya Michezo Taifa Alex Faustini Temba, ameishukuru Serikali kwa kutoa kibali kwa wafanyakazi kushiriki michezo hiyo ambapo mbali na kucheza michezo hiyo tofauti tofauti walichanga fedha shilingi milioni 13, ambazo walizitoa kwa Vituo vya wahutaji jijini Arusha.

Naye Mwenyekiti wa Michezo Shirika la Viwango Nchini (TBS), Nyabuchwenza Methusela, amesema michezo ya mwaka huu ilikuwa na mafanikio licha ya changamoto iliyojitokeza  ya uchelewaji wa washiriki kuhudhuria na hivyo kuathiri ratiba na kusababisha michezo kuchezwa mfululizo asubuhi na jioni.
Posted by MROKI On Friday, July 26, 2024 No comments

July 25, 2024

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama kwa ajili ya heshima ya Wimbo wa Taifa na ule wa Afrika Mashariki wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa kwenye Mji wa Serikali Mtumba Mkoani Dodoma tarehe 25 Julai, 2024. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiweka silaha za Asili (Mkuki Ngao) na shada la maua kwenye mnara wa Mashujaa wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa. Maadhimisho hayo yamefanyika katika Uwanja wa Mashujaa uliopo kwenye Mji wa Serikali Mtumba Mkoani Dodoma tarehe 25 Julai, 2024. 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama kwa ajili ya heshima ya Wimbo wa Taifa na ule wa Afrika Mashariki wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa kwenye Mji wa Serikali Mtumba Mkoani Dodoma tarehe 25 Julai, 2024. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwasili katika Uwanja wa Mashujaa uliopo Mji wa Serikali Mtumba Mkoani Dodoma kwa ajili ya kushiriki Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa tarehe 25 Julai, 2024


Posted by MROKI On Thursday, July 25, 2024 No comments
Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Rufaa (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Waratibu wa Uandikishaji wa mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA wa halmashauri yaliyoanza leo tarehe 25 hadi 26 Julai,2024 Mkoani Kagera.

Washiriki wakifatilia hotuba ya ufunguzi.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhamiaji ,Erasmi Francis  akitoa mada kuhusu uraia wakati wa mafunzo hayo. 

Washiriki wakifuatilia mada 
Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Rufaa (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk (katikati) akiwa na Wajumbe wa Tume kutoka kushoto, Mhe. Dkt. Zakia Mohamed Abubakar, Mhe. Magdalena Rwebangira pamoja na Mkurugenzi wa Habari na Elimu ya Mpiga Kura Bi. Giveness Aswile (wapili kulia) na Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Kagera, Mapinduzi 
Hakimu Mkazi wa Wilaya Bukoba, Frola Alex Kaijage akizungumza wakati wa kuwaapisha watendaji hao wa Uandikishaji Mkoa wa Kagera.

Waratibu wa Uandikishaji wa mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA wa Halmashauri wakila kiapo cha kujitoa uanachama na kutunza siri kiapo kilichoongozwa na  Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Bukoba, Flora Alex Kaijage. 
Waratibu wa Uandikishaji wa mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA wa Halmashauri wakila kiapo cha kujitoa uanachama na kutunza siri kiapo kilichoongozwa na  Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Bukoba, Flora Alex Kaijage. 
Waratibu wa Uandikishaji wa mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA wa Halmashauri wakila kiapo cha kujitoa uanachama na kutunza siri kiapo kilichoongozwa na  Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Bukoba, Flora Alex Kaijage. 
***************
Na Mwandishi wetu, Kagera
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetaka watendaji wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura Mkoani Kagera na Geita kuhakikisha wanatunza vifaa vya uandikishaji ili vikaweze kutumika maeneo mengine nchini.
 
Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Rufaa (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Waratibu wa Uandikishaji wa mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA wa halmashauri yaliyoanza leo tarehe 25 hadi 26 Julai,2024 Mkoani Kagera.
 
Mafunzo kama hayo pia yamefunguliwa Mkoani Geita na Mwenyekiti wa Tume, Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele leo mkoani humo.
 
“Kwa kusisitiza, ni muhimu kutekeleza majukumu yenu kwa umakini katika kila eneo ikiwemo utunzaji wa vifaa vya uandikishaji hasa ikizingatiwa kuwa, vifaa hivi vimenunuliwa kwa gharama kubwa sana na vinatarajiwa kutumika katika maeneo mengine ya uandikishaji nchini,” alisema Jaji Mbarouk.
 
Amesema kutokuwa makini katika utunzaji wa vifaa hivi kutapelekea athari kubwa katika ukamilishaji wa zoezi hili muhimu na amewataka kuzingatia maelekezo yote yatakayotolewa na Tume ili muweze kuyafanyia kazi wakati zoezi litakapokuwa limeanza.
 
Aidha, Jaji Mbarouk amesema matokeo bora ya zoezi hili yanategemea uwepo wa ushirikiano mkubwa kati ya watendaji wote wa uboreshaji, serikali, vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi.
 
“Ninawasihi muwe na ushirikiano mzuri na wa karibu na Tume wakati wote mtakapokuwa mnatekeleza majukumu yenu na ikiwa mnahitaji ufafanuzi au maelekezo yeyote, msisite kuwasiliana na Tume,” 
alisema Jaji Mbarouk.
 
Mapema kabla ya kuanza mafunzo hayo, washiriki walikua kiapo cha kujitoa uanachama na kile cha kutunza siri mbele ya 
Hakimu Mkazi wa Wilaya Bukoba, Frola Alex Kaijage
 
Mafunzo hayo yanahusisha namna ya ujazaji wa fomu pamoja na kutumia mfumo wa kuandikisha wapiga kura (Voters Registration System - VRS) ili waweze kupata uelewa wa pamoja utakaowapa fursa ya kutumia kwa ufasaha mfumo huo pamoja na vifaa vingine vya kuandikisha wapiga kura.
 
“Mafunzo haya, yanawajengea umahiri wa kuwafundisha Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Kata kisha nao watatoa mafunzo hayo kwa Waendeshaji wa Vifaa vya Bayometriki na Waandishi Wasaidizi ambao ndio watahusika na uandikishaji wa wapiga kura vituoni,” alisema Jaji Mbarouk
 
Aidha, Maafisa TEHAMA watapatiwa mafunzo maalum ya jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiufundi (Troubleshooting) endapo zitajitokeza wakati wa zoezi la uandikishaji wa wapiga kura vituoni.
 
Katika hatua nyingine, Jaji Mbarouk amewaambia watendaji hao kuwa  wakati wa uboreshaji wa Daftari mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura jambo ambalo litasaidia kuleta uwazi katika zoezi zima lakini pia mawakala hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za lazima.
 
Jaji Mbarouk alitoa angalizo kwa mawakala hao kutoka vyama vya siasa kuwa  hawaruhusiwi kuwaingilia watendaji wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao vituoni.
 
Tume tayari imeanza zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambapo uzinduzi ulifanyika mkoani Kigoma Julai 20, 2024 na mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB).
 
Uzinduzi huo umeenda sambamba na kuanza kwa mzunguko wa kwanza wa uboreshaji kwenye mikoa mitatu ya Kigoma, Tabora na Katavi. Uboreshaji wa Daftari kwenye mikoa hiyo unaendelea hadi tarehe 26 Julai, 2024, na kauli mbiu ya uboreshaji ni  “Kujiandikisha Kuwa Mpiga Kura Ni Msingi Wa Uchaguzi Bora”
Posted by MROKI On Thursday, July 25, 2024 No comments
  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo