Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga amewakabidhi wadau wa usalama wa Mji wa Tunduma, Wilaya ya Momba mkoani Songwe vyeti vya pongezi kwa kutambua mchango wao mkubwa katika kuimarisha ulinzi na usalama, pamoja na kujitolea kuboresha miundombinu ya Kituo cha Polisi Tunduma ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi vyeti hivyo iliyofanyika Julai 26, 2026, SACP Senga aliwashukuru wadau hao kwa moyo wao wa uzalendo na ushirikiano wanaouonesha kwa Jeshi la Polisi. Waliotunukiwa vyeti hivyo ni Kessy Kahise aliyetoa vifaa vya usafi, Abel Waya aliyetoa shilingi milioni nne kwa ajili ya ununuzi wa pampu na ujenzi wa kisima cha maji katika Kituo cha Polisi Tunduma, pamoja na Alex Ngasala, Msaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Tunduma aliyemwakilisha Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, ambaye alitoa shilingi milioni nne kwa ajili ya ujenzi wa kisima hicho na shilingi laki tano kwa ajili ya ununuzi wa malighafi za ujenzi wa choo kinachoendelea kujengwa kituoni hapo.
Kwa upande wao, wadau hao waliipongeza kazi inayofanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe na kueleza kuwa wamehamasishwa na dhana ya Polisi Jamii, jambo lililowafanya kutambua kuwa ulinzi na usalama ni jukumu la kila mwananchi. Walisema ushirikiano huo umewapa hamasa ya kuendelea kuchangia maendeleo ya Jeshi la Polisi na kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za kiusalama kwa wananchi.
Naye Mkuu wa Polisi Wilaya ya Momba, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Bhoke Simango aliwataka wadau wengine kuiga mfano huo kwa kujitokeza kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya Jeshi la Polisi, ikiwemo kukamilisha ujenzi wa choo na miradi mingine katika Kituo cha Polisi Tunduma. Alisema hatua hiyo ni matokeo ya mafanikio ya dhana ya Polisi Jamii, ambayo imeendelea kuimarisha ushirikiano, kujenga imani kati ya wananchi na Jeshi la Polisi, na kuongeza ari ya wananchi kujitolea kushiriki katika kulinda amani, usalama na maendeleo ya jamii.










0 comments:
Post a Comment