Nafasi Ya Matangazo

July 27, 2026


Babati, Manyara
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Babati ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mhe. Remidius Mwema, amesisitiza kuwa uhifadhi endelevu wawanyamapori ni nguzo muhimu ya ukuaji wa sekta ya utalii, uwekezaji na maendeleo ya jamii, huku akiwataka askari wahifadhi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uzalendo.

Mhe. Mwema ametoa kauli hiyo  alipofungua rasmi mafunzo maalum ya siku tano kwa askari wahifadhi wanaotekeleza majukumu katika Ikolojia ya Tarangire–Manyara, hususani maeneo yenye mtawanyiko wa wanyamapori na ushoroba wa _“Kwakuchinja.”_

Mafunzo hayo yaliandaliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Babati kwa kushirikiana na Chem Chem Association(CCA) na kuwakutanisha askari wahifadhi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Hifadhi ya Taifa ya Tarangire (TANAPA), Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Burunge pamoja na Chem Chem Association, mafunzo hayo yalifanyika kuanzia Julai 20 hadi 25, 2026.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhe. Mwema alisema Serikali inaendelea kuwekeza na kuimarisha uwezo wa watumishi wa sekta ya uhifadhi ili kuhakikisha rasilimali za wanyamapori zinalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

_"Tunashuhudia ukuaji wa sekta ya utalii, uwekezaji katika vitalu vya uwindaji, ujenzi wa hoteli za kitalii na maendeleo ya jamii yanayotokana na uwepo wa rasilimali hizi, Wanyamapori wakitoweka, fursa hizo pia zitatoweka. Hivyo, ni muhimu kuendelea kuimarisha mapambano dhidi ya ujangili pamoja na kujenga ushirikiano madhubuti na wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi ili wawe walinzi na mabalozi wa uhifadhi,"_  Alisema Mhe. Mwema.

Alieleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali na wadau wa uhifadhi kwa lengo la kuongeza maarifa, ujuzi na weledi wa askari wahifadhi katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazokabili maeneo yaliyohifadhiwa.

Aidha, amesema ushirikiano kati ya taasisi za uhifadhi, wadau wa maendeleo na wananchi ni msingi wa kuhakikisha shoroba za wanyamapori zinaendelea kuwa salama na kuchangia ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya utalii.

Mafunzo hayo pia yalihusisha  wakufunzi kutoka nchini Marekani, ambao walishiriki kutoa uzoefu na mbinu za kisasa za kimataifa katika ulinzi na usimamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa askari wahifadhi katika kutekeleza majukumu yao.

Katika hafla hiyo, Mhe. Mwema aliambatana na Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Babati pamoja na wataalamu kutoka TANAPA, TAWA, Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Burunge na Halmashauri ya Wilaya ya Babati.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuimarisha uwezo wa askari wahifadhi katika kulinda Ikolojia ya Tarangire–Manyara, eneo lenye umuhimu mkubwa kwa uhifadhi wa bioanuwai, maendeleo ya utalii na ustawi wa uchumi wa Taifa. 








Posted by MROKI On Monday, July 27, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo