Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ameonya vikali wanachama wanaotafuta uteuzi wa udiwani, uwakilishi na ubunge kwa njia zisizo halali, akisisitiza kuwa chama hakitasita kuwaengua wale watakaokiuka Katiba, Kanuni na maadili ya CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa makatibu wa matawi na kata kutoka Wilaya ya Dodoma, Balozi Nchimbi alisema baadhi ya wanachama wameanza kampeni kabla ya muda rasmi kwa kutumia mbinu kama kuanzisha mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), kufadhili matukio ya kijamii kama kumbukumbu za misiba na sherehe za ndoa, pamoja na kushinikiza vikao vya chama kuwapitisha bila kupingwa.
“Tayari tumeshuhudia baadhi ya wabunge na madiwani wakitafuta mbinu za kuhakikisha wanapitishwa bila kupingwa. Wengine wanahamasisha matamko ya vikao, huku baadhi wakihudhuria matukio yenye lengo la kujitambulisha mapema kwa wapiga kura. Wapo wanaowapa posho wahudhuriaji wa mikutano wakiwa wamevaa sare za CCM ili kuonesha wanaungwa mkono. Tunawataka waache mara moja. CCM ina mfumo madhubuti wa kufuatilia mwenendo wa wanachama wake, na kumbukumbu hizi zote zinahifadhiwa. Wanaweza kushangaa majina yao yakiwekwa pembeni,” alisema.
Balozi Nchimbi aliwataka madiwani na wabunge walioko madarakani kuacha kupuuza majukumu yao kwa kisingizio cha maandalizi ya uchaguzi, akisema chama kitafanya tathmini kwa kila mgombea kulingana na utendaji wake, si kwa uwezo wa kutoa fedha kwa wapiga kura.
“Tumeshuhudia watu wakichaguliwa lakini wanakaa miaka mitano bila kufanya kazi kwa sababu wanajua wapiga kura wachache wa ndani ya chama watakaowarudisha tena madarakani. Mfumo wetu mpya unalenga kumchagua mgombea kwa misingi ya kazi zake, si kwa kutumia rushwa au mbinu za kificho. Tunataka ukichaguliwa ukafanye kazi kwa wananchi,” alisisitiza.
Alieleza kuwa mabadiliko ya Katiba ya CCM yaliyofanyika chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, yalilenga kuongeza idadi ya wapiga kura katika kura za maoni ili kupata taswira pana ya maoni ya wananchi na kudhibiti mianya ya rushwa.
Aidha, Balozi Nchimbi alisema baadhi ya wanachama wanaotaka nafasi za uongozi wameanza kutumia mbinu mbalimbali kuhakikisha wanapitishwa bila kupingwa, jambo ambalo alisema halikubaliki ndani ya chama.
“Tumeanza kuona matukio ya baadhi ya wabunge na madiwani wakipitisha fomu ili watangazwe kuwa wagombea pekee. Wengine wanahamasisha vikao kutoa matamko kwamba wapitishwe bila kupingwa. Wapo wanaoandaa kumbukumbu za misiba, siku za kuzaliwa na hata sherehe za ndoa, lakini wahudhuriaji wanapewa posho na wamevaa sare za CCM ili ionekane kama mkutano wa kisiasa,” alisema.
Aliongeza kuwa CCM ina utaratibu wa kufuatilia mwenendo wa wanachama wake, na wale wote wanaoendesha kampeni za chinichini wataenguliwa mapema.
“Wengine wameanzisha NGOs kwa malengo ya kisiasa, wengine wanatumia mbinu za kuwachafua waliopo madarakani kwa sasa. Kwa wote hawa, tunasema waache mara moja. Wanapoteza muda na kutufanya tufikirie kuwaengua. Hatutavumilia mambo haya,” alionya.
Balozi Nchimbi aliwataka viongozi wa CCM katika ngazi zote kuhakikisha wanatenda haki kwa kusimamia Katiba na Kanuni za chama bila upendeleo.
“Mafunzo haya tunayotoa yanalenga kuwawezesha makatibu wa matawi na kata kujua dhamana yao ndani ya chama, majukumu yao na mipaka yao ya kazi. Ushindi wa CCM unategemea uimara wa mfumo wake, imani ya wanachama kwa chama, pamoja na utendaji wa Serikali yake chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema.
Alihitimisha kwa kusisitiza kuwa chama hakitawavumilia wanaojihusisha na kampeni za chinichini na kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka taratibu.