Nafasi Ya Matangazo

January 27, 2026


Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba akiwasilisha hoja ya kujadili hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bungeni jijini Dodoma, Januari
  27, 2026. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kufanya mageuzi ya sera zinazogusa moja kwa moja maslahi na ustawi wa maisha ya wananchi. 

 

Amesisitiza kuwa Serikali haitavumilia watendaji wa Serikali wanaotoa visingizio, wasiowajibika na wenye hulka ya kufanya kazi kwa mazoea, ujanja ujanja na kutoa taarifa za michakato badala ya majibu yanayotakiwa.

 

Amesema hayo Bungeni leo (Jumanne, Januari 27, 2026) wakati akitoa hoja ya kujadili hotuba ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa jijini Dodoma wakati akizindua Bunge la 13 Novemba 14, 2025.

 

“Tunapozungumzia utendaji Serikalini, msisitizo ni uadilifu na uwajibikaji wa Serikali kwa wananchi waliotuchagua ili kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali za nchi pamoja na kupata huduma wanazostahili.”

 

Dkt. Mwigulu amesema kuwa hotuba aliyoitoa Rais Dkt. Samia ilitoa mwelekeo na dira ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa kipindi cha pili. “Hotuba ya Mheshimiwa Rais ilitoa maelekezo na kubainisha changamoto pamoja na majukumu yanayotupasa kuyatekeleza kwa kushirikiana na wananchi na wadau wengine wa maendeleo.”

 

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kutekeleza vipaumbele vyote vilivyoainishwa. “Serikali imeainisha maeneo mbalimbali ya utekelezaji na kupanga mipango kazi ya utekelezaji wa muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu, na tayari utekelezaji wake umeshaanza kutekelezwa kwenye maeneo kadhaa”.
Posted by MROKI On Tuesday, January 27, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo