Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Kaspar Mmuya amesema atahakikisha anasimamia kila mwananchi mwenye uhalali wa kupata hati milki ya eneo lake analomiliki anapata hati.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye Kliniki Maalum ya Ardhi inayoendelea katika Ofisi za Ardhi Mkoa wa Dodoma leo tarehe 28 Januari, 2026 Mhe. Mmuya amesema, upo umuhimu wa kuhakikisha wananchi waliokamilisha taratibu za kumilikishwa wanapata hati zao kwa kuwa wapo waliofuatilia kwa muda mrefu.
"Nitasimamia kuhakikisha kila mwananchi mwenye uhalali wa kumiliki Ardhi anapata hati yake kwa wakati” amesema Naibu Waziri Mmuya.
Ili kutoa huduma bora, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amewataka wataalamu wa Sekta ya Ardhi nchini kuhakikisha wanatoa elimu ya matumizi bora ya ardhi pamoja na jinsi ya kupata hatimiliki za ardhi, hatua aliyoieleza itasaidia kuepusha ujenzi holela unaoenda kinyume na matumizi yaliyopangwa.
Mhe. Mmuya amesema, Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kusimamia haki ya umiliki wa ardhi kwa vitendo na kuhakikisha wamiliki wa ardhi wanapata hati zao.
Ameeleza kuwa, Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawahakikishia wananchi kuendelea kupata huduma za hati katika maeneo mbalimbali nchini.
Ameongeza kuwa, wizara hiyo chini ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo imeweka mkakati wa siku 14 kuhakikisha kila mwananchi wa Jiji la Dodoma aliyekidhi vigezo vya kupata hati milki ya ardhi anapata hati yake hatua aliyoieleza kuwa, itaidia kurahisisha huduma na kulinda haki za wananchi.
Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga amesema, wamiliki wa ardhi waliokamilisha taratibu za umiliki wapewe Hatimiliki zao na hawahitaji maneno mengi.
Mhandisi Sanga amesisitiza kuwa, ni marufuku kwa mtumishi wa sekta ya ardhi anayefutwa na mwanachi mwenye shida kumwambia aende kwa mtu mwingine kupata huduma na kueleza kuwa, atasimamia msimamo huo kwa kuwa mwananchi anachohitaji ni huduma.
Katika siku ya kwanza ya zoezi hilo, tayari zaidi ya Hatimiliki 150 zimetolewa ambapo Edward Aloyce na Colletha Magema miongoni mwa wananchi waliopata hati zao wamethibitisha kwamba, zoezi hilo ni muhimu na linawasaidia wananchi kupata hati za ardhi kwa lengo la kumiliki maeneo yao kihalali.
Zoezi la Kliniki Maalum ya Ardhi ambayo imejikita kutoa Hatimiliki za Ardhi katika jiji la Dodoma ni la siku 14 kuanzia 28 Januari hadi Februari 10, 2026.











0 comments:
Post a Comment