Mfuko wa kimataifa wa uwekezaji Sino American Global Fund (SinoAm LLC) umeonesha nia ya kuwekeza hadi Dola za Marekani bilioni 5 nchini Tanzania katika miradi mikubwa ya kimkakati, hususan katika sekta za miundombinu, usafirishaji, nishati, teknolojia, huduma za kifedha na maendeleo ya viwanda.
Nia hiyo iliwasilishwa rasmi wakati wa mkutano kati ya uongozi wa SinoAm LLC na Prof. Kitila Alexander Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, uliofanyika jijini London, Uingereza, pembezoni mwa ziara rasmi ya Waziri huyo nchini humo.
Akizungumza kwa niaba ya SinoAm LLC, Bw. Najib Choufani, Mwenyekiti wa Mfuko huo, alieleza kuwa mfuko huo umejipanga kuwekeza kiasi kinachoweza kufikia USD bilioni 5 nchini Tanzania kwa awamu, kupitia miradi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), sambamba na vipaumbele vya maendeleo ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Bw. Choufani alibainisha kuwa SinoAm LLC imefanya tathmini ya kina ya mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania na kubaini fursa zenye tija kubwa, ikiwemo ujenzi na uendeshaji wa barabara za kisasa za kulipia (toll expressways), miradi ya reli ya kiwango cha kimataifa (SGR), pamoja na miundombinu muhimu ya uchukuzi na nishati inayochochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ushindani wa Tanzania kikanda.
Katika mkutano huo, uongozi wa SinoAm LLC pia uliambatana na Bw. Tarek Choufani, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko huo, ambaye alieleza kuwa SinoAm ina uzoefu mpana wa kimataifa katika kusimamia miradi mikubwa ya miundombinu na iko tayari kuleta si tu mitaji mikubwa, bali pia utaalamu wa kiufundi, mifumo ya kisasa ya usimamizi na mbinu bora za kimataifa nchini Tanzania.
Kwa upande wake, Waziri Mkumbo aliipongeza SinoAm LLC kwa kuonesha dhamira ya dhati ya kuwekeza kiasi kikubwa cha mitaji nchini Tanzania, akibainisha kuwa Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wakubwa wa kimataifa. Alisisitiza kuwa Tanzania ina utulivu wa kisiasa, sera rafiki za uwekezaji, na dira ya muda mrefu ya maendeleo inayotoa uhakika na ulinzi kwa uwekezaji wa kimkakati.





0 comments:
Post a Comment