Nafasi Ya Matangazo

January 26, 2026










Na WAF, Arusha 
Serikali imetangaza mwanzo wa enzi mpya ya uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi katika sekta ya afya baada ya kuzindua rasmi kwa mfumo wa kidijitali wa “Ongea na Waziri wa Afya” unaomuwezesha mwananchi kuwasiliana moja kwa moja na Wizara ya Afya saa 24 kwa siku.

Hayo yamesemwa na Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa  hafla ya uzinduzi iliyofanyika leo Januari 26,2026 jijini Arusha.

Waziri wa Afya, Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, amesema mfumo huo ni utekelezaji wa vitendo wa dhamira ya Serikali ya kuisogeza huduma ya afya karibu na mwananchi na kuhakikisha sauti ya wananchi inatumika kama dira ya maboresho ya huduma.

“Mfumo wa "Ongea na Waziri wa Afya" unatuma ujumbe ulio wazi kuwa sauti ya mwananchi si ya pembeni, bali ndiyo msingi wa maamuzi ya Serikali katika kuboresha huduma za afya,” amesema Waziri Mchengerwa.

Amefafanua kuwa uzinduzi wa mfumo huo ni mapinduzi makubwa katika sekta ya afya kwa kuwa unajenga utamaduni mpya wa uongozi unaosikiliza, unaojibu kwa wakati na unaotenda kwa matokeo. 

Kupitia mfumo huo, wananchi wataweza kutoa maoni, kuuliza maswali, na kuwasilisha malalamiko ambayo yatafuatiliwa hadi kupatiwa majibu au ufumbuzi wa kudumu.

Waziri Mchengerwa amesisitiza kuwa matumizi ya teknolojia katika sekta ya afya si suala la mitindo bali ni uamuzi wa kizalendo unaolenga kuokoa muda, rasilimali na maisha ya wananchi. Amesema Serikali inalenga kujenga mfumo wa afya wa kitaifa unaounganisha huduma zote kuanzia kituo cha afya hadi hospitali za rufaa, huku ukizingatia usalama wa taarifa na faragha ya mgonjwa.

Katika hotuba yake, Waziri pia ameeleza dhamira ya Serikali ya kutumia teknolojia za kisasa ikiwemo Akili Mnemba (AI) kwenye kuboresha uchunguzi wa magonjwa, upangaji wa rasilimali na maamuzi ya kitabibu, huku akisisitiza kuwa teknolojia hizo lazima zitumike kwa kuzingatia maadili na kulinda utu wa binadamu.

“AI lazima iongeze utu, si kuupunguza. Tunataka akili yenye hekima inayolinda mgonjwa na faragha zake,” amesema Mhe. Mchengerwa.

Amehakikishia wananchi kuwa hakuna Mtanzania atakayeachwa nyuma kwa kukosa simu janja au uelewa wa kidijitali, kwani Serikali itaendelea kutoa elimu, mifumo rafiki na njia mbadala za mawasiliano ili kuhakikisha teknolojia inakuwa daraja, si kikwazo.

Kupitia mfumo wa 'Ongea na Waziri wa Afya, wananchi wataweza kuwasiliana na Wizara ya Afya kwa kupiga simu ya bure namba 199, kutuma ujumbe mfupi (SMS), kutumia mitandao ya kijamii ya Wizara, au kupitia tovuti ya [www.owa.moh.go.tz](http://www.moh.go.tz). Mawasiliano yote yatasajiliwa, kufuatiliwa na kupatiwa mrejesho kwa njia ile ile iliyotumika.

Katila hatua nyingine Mchengerwa ametangaza kuwa mfumo huo utakuwa chachu ya kuanzishwa kwa Afya Forum, tukio la kitaifa litakalofanyika kila mwaka na kujumuisha mijadala ya kitaalamu, maonesho ya bunifu za afya pamoja na utoaji wa Tuzo za Afya kwa watumishi na taasisi zilizofanya vizuri, kwa kuzingatia takwimu halisi kutoka kwenye mfumo huo.

Waziri Mchengerwa amesema Serikali imejipanga kuongoza mageuzi ya afya kwa ushahidi na si kubahatisha, akisisitiza kuwa afya ni msingi wa uchumi, usalama wa taifa na heshima ya nchi.
Posted by MROKI On Monday, January 26, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo