Nafasi Ya Matangazo

January 27, 2026



Na Wizara ya Madini, Dodoma
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amesema Wizara ya Madini imeandaa rasimu ya Mkataba kati ya Wamiliki wa Leseni za Uchimbaji na Wachimbaji Wadogo, ambao umewasilishwa kwa Maafisa Madini Wakazi nchini kote kwa ajili ya usimamizi pindi utakapokuwa umesainiwa na kusajiliwa.

Dkt. Kiruswa ameyasema hayo leo Januari 27, 2026, Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu
swali la Mbunge wa Katoro, Mhandisi Kija Ntemi, aliyetaka kufahamu ni nani atasimamia
mikataba kati ya wamiliki wa leseni na wachimbaji wadogo wanaovumbua madini, pamoja
na muda wa mikataba hiyo.

Amesema mikataba hiyo itadumu kwa kipindi cha miaka mitatu na itaweza kuhuishwa kwa kipindi kingine kulingana na makubaliano ya wahusika. ‘’ Mikataba hiyo itadumu kwa kipindi cha miaka mitatu na huruhusiwa kuhuishwa kwa kipindi kingine kulingana na makubaliano ya wahusika,’’amesema Dkt. Kiruswa.

Amefafanua kuwa, kufuatia marekebisho ya Kanuni za Haki za Madini za Mwaka 2018 yaliyofanyika mwaka 2025, Kanuni ya 5A (1) imeweka sharti la mmiliki wa leseni ndogo ya uchimbaji kuingia mkataba na mchimbaji mdogo atakayefanya shughuli za uchimbaji ndani ya eneo la leseni yake, na kuhakikisha mkataba huo unaidhinishwa na kusajiliwa na Tume ya
Madini.

Katika hatua nyingine, akijibu swali la Mbunge wa Tarime Vijijini, Mhe. Mwita Waitara,
aliyetaka kujua ni lini Kanuni za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kwenye migodi zitabadilishwa
ili miradi ya maendeleo   isimamiwe na Halmashauri kwa mtindo wa Local Fund badala ya mwekezaji, Dkt. Kiruswa amesema Kanuni ya 15(1) imeelekeza mmiliki wa leseni kuwajibika kutekeleza mpango wa wajibu wake kwa jamii.

Ameeleza kuwa katika utekelezaji wa miradi ya CSR, mmiliki wa leseni anatakiwa
kuzingatia taratibu za ununuzi na anaweza kuajiri mkandarasi au mtu mwingine yeyote kwa ajili ya utekelezaji wa miradi iliyopo kwenye mpango wa CSR.

Aidha amesisitiza kwamba, Kanuni za Wajibu wa Wamiliki wa Leseni kwa Jamii (CSR),
zilizoanza kutumika rasmi mwezi Juni 2023, zinaeleza wazi majukumu ya wadau mbalimbali katika kuhakikisha jamii zinazozunguka migodi zinanufaika ipasavyo na uwepo wa migodi hiyo.

 Ameongeza kuwa utekelezaji wa majukumu hayo unapaswa kufanywa na mmiliki wa
leseni kwa kushirikiana kwa karibu na Mamlaka za Serikali za Mitaa (Halmashauri).
Posted by MROKI On Tuesday, January 27, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo