Nafasi Ya Matangazo

January 22, 2026

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo (katikati), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Abdulmajid Nsekela, kwa pamoja wakizindua rasmi Ofisi ya Uwakilishi ya Benki ya CRDB Dubai. Hafla hiyo ilifanyika jana katika ukumbi wa hoteli ya InterContinental, Dubai.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo (katikati) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Abdulmajid Nsekela wakisalimiana na baadhi ya wawekezaji na wakuu wa taasisi kutoka Dubai na Falme za Kiarabu katika hafla ya uzinduzi wa Ofisi ya Uwakilishi ya Benki ya CRDB Dubai iliyofanyika jana katika ukumbi wa hoteli ya InterContinental, Dubai.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo akizungumza wakati wakiwasili katika hafla ya ufunguzi wa Ofisi ya Uwakilishi ya Benki ya CRDB Dubai, iliyofanyika jana katika ukumbi wa hoteli ya InterContinental, Dubai.
katika ukumbi wa hoteli ya InterContinental, Dubai.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akizungumza wakati wakiwasili katika hafla ya ufunguzi wa Ofisi ya Uwakilishi ya Benki ya CRDB Dubai, iliyofanyika jana katika ukumbi wa hoteli ya InterContinental, Dubai.
Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil akizungumza wakati wakiwasili katika hafla ya ufunguzi wa Ofisi ya Uwakilishi ya Benki ya CRDB Dubai, iliyofanyika jana katika ukumbi wa hoteli ya InterContinental, Dubai.
Balozi wa Tanzania katika Falme za Kiarabu, Mhe. Balozi Luteni Jenerali Mstaafu, Yacoub Mohammed akizungumza wakati wakiwasili katika hafla ya ufunguzi wa Ofisi ya Uwakilishi ya Benki ya CRDB Dubai, iliyofanyika jana katika ukumbi wa hoteli ya InterContinental, Dubai.
 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo (wapili kushoto), akiwa ameongozana na Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar, Juma Malik Akil (kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori (kushoto) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Abdulmajid Nsekela (wapili kulia) wakati wakiwasili katika hafla ya ufunguzi wa Ofisi ya Uwakilishi ya Benki ya CRDB Dubai, iliyofanyika jana katika ukumbi wa hoteli ya InterContinental, Dubai.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Abdulmajid Nsekela, Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB na kampuni zake tanzu, pamoja na baadhi wawekezaji waliohudhuria hafla ya ufunguzi wa Ofisi ya Uwakilishi ya Benki ya CRDB Dubai, iliyofanyika jana katika ukumbi wa hoteli ya InterContinental, Dubai.
Washiriki wakifuatilia hafla ya uzinduzi wa Ofisi ya Uwakilishi ya Benki ya CRDB wakifuatilia onyesho la ndege zisizo na rubani ‘drone’ likionyesha nembo ya Benki hiyo katika Falme za Kiarabu iliyofanyika jana katika ukumbi wa hoteli ya InterContinental, Dubai.
Washiriki wa hafla ya uzinduzi wa Ofisi ya Uwakilishi ya Benki ya CRDB iliyofanyika jana katika ukumbi wa hoteli ya InterContinental, Dubai.

Dubai, UAE, 20 Januari 2026 – Mahusiano ya kiuchumi kati ya Afrika na Falme za Kiarabu (UAE) yamefikia hatua muhimu leo kufuatia uzinduzi rasmi wa Ofisi ya Uwakilishi ya Benki ya CRDB Dubai katika Kituo cha Fedha cha Kimataifa cha Dubai (DIFC). Hii ni mara ya kwanza kwa benki ya Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kupanua wigo wa huduma zake katika moja ya vituo vya fedha vyenye ushawishi mkubwa zaidi duniani.

Hatua hii inaweka Tanzania, pamoja na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, uchumi wa pamoja unaokaribia dola za Marekani bilioni 800, moja kwa moja katika mfumo wa mitaji ya kimataifa, kupitia taasisi ya fedha ya Kiafrika iliyoasisiwa barani Afrika, ikifanya kazi kama daraja kati ya fursa za kikanda na za kimataifa.

Uzinduzi huo uliwakutanisha viongozi wakuu kutoka taasisi za fedha za kimataifa, wawekezaji kutoka kote duniani, makampuni makubwa ya kimataifa na washirika wa maendeleo ya kifedha. Ushiriki huu unaonyesha kuongezeka kwa hamasa ya kimataifa kuhusu Afrika kama eneo linalofuata kwa ukuaji mkubwa wa uchumi duniani.

Hafla ya uzinduzi rasmi wa Ofisi hiyo iliongozwa na Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza kwa niaba ya Rais, Waziri Kombo aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuendeleza dira ya uchumi ya Tanzania kupitia diplomasia ya uchumi, jitihada ambazo zimekuwa zikitekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita. Alisema kuingia kwa benki hiyo Dubai ni mkakati madhubuti, akitaja nafasi ya Dubai kama kitovu kikuu cha mitaji ya dunia pamoja na uwepo wa mfumo imara wa kifedha na udhibiti.

“Uwepo wa benki ya Tanzania nchini Dubai utaimarisha mahusiano ya kiuchumi na kibiashara kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Falme za Kiarabu, ukichochea biashara ambayo tayari imefikia takribani dola za Marekani bilioni 2.5 kwa mwaka. Aidha, utaimarisha muunganiko wa Afrika Mashariki na Kati na masoko ya kimataifa,” alisema Waziri Kombo.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Juma Akili, alisema hatua hiyo inaashiria kukomaa kwa sekta ya fedha ya Tanzania.

“Hatua hii muhimu inaonyesha ukomavu na kuongezeka kwa umahiri wa sekta ya fedha ya Tanzania, pamoja na uwezo wa taasisi zetu za ndani kushindana katika masoko ya fedha ya kimataifa.”

Ikiwa na idadi ya watu zaidi ya milioni 60, Tanzania imeonyesha uthabiti mkubwa wa kiuchumi kwa zaidi ya miongo miwili, ikidumisha ukuaji wa Pato la Taifa wa wastani wa asilimia 6–7 na kudhibiti mfumuko wa bei katika viwango vya tarakimu moja. Uthabiti huu umeifanya Tanzania kujijengea nafasi ya kipekee kama lango la uchumi linalounganisha Bahari ya Hindi na masoko ya nchi zisizo na bandari za Afrika Mashariki na Kati.

Kwa kuzingatia nafasi hiyo ya kimkakati, Benki ya CRDB imekuwa miongoni mwa taasisi za kifedha zilizo mstari wa mbele kuchochea ukuaji wa uchumi wa kikanda. Tangu kuanzishwa kwake miaka 30 iliyopita, Benki imekua sambamba na uchumi wa Tanzania na ajenda ya muunganiko wa kikanda. Kwa sasa, Benki ya CRDB inahudumia zaidi ya wateja milioni sita katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ikiwa na jumla ya mali inayozidi dola za Marekani bilioni 9, na uwepo katika Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Akizungumza katika hafla hiyo, Abdulmajid Nsekela, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kundi la Benki ya CRDB, alisema upanuzi wa benki kwenda Dubai ni hatua ya kimantiki katika mkakati wa kikanda unaotokana na jiografia ya uchumi wa Tanzania na ajenda ya muunganiko wa Afrika.

“Benki ya CRDB imejengwa katika misingi ya kufadhili ukuaji wa Tanzania. Jinsi ambavyo Tanzania imekuwa ikikua na kuwa lango la uchumi katika ukanda huu, ndivyo Benki nayo imekuwa ikikua kikanda,” alisema. “Dubai sasa inatuwezesha kuunganisha mitaji ya kimataifa, Tanzania, na Afrika Mashariki na Kati.”

Afrika Mashariki na Kati kwa pamoja zinawakilisha soko la karibu watu milioni 400, ikishuhudia kuongezeka kwa biashara ya ndani ya Afrika, upanuzi wa miundombinu, rasilimali kubwa za madini na nishati, pamoja na nguvu kazi changa zaidi duniani. Afrika kwa ujumla ina watu bilioni 1.4, uchumi nwenye thamani ya dola za Marekani trilioni 3.4, na inatarajiwa kuwa robo ya idadi ya watu duniani ifikapo mwaka 2050.

Licha ya ukubwa huu, upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu bado ni changamoto kubwa. Ofisi ya Uwakilishi ya Benki ya CRDB Dubai imeanzishwa kuziba pengo hili kwa kuanzisha miradi, kupanga miundo ya ufadhili na kuhamasisha mitaji ya kimataifa kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika ukanda huu. “Afrika haina uhaba wa fursa,” alibainisha Nsekela. “Mara nyingi kinachokosekana ni daraja kati ya mitaji na utekelezaji. Ofisi hii ndiyo daraja hilo.”

Kwa kuanzisha uwepo wa benki ya Tanzania katika Dubai, Benki ya CRDB inatarajiwa kuimarisha ufadhili wa biashara, kuvutia mitaji ya uwekezaji na ushirikiano na taasisi za kifedha za kimataifa kati ya Ghuba na Afrika, ikitumia Tanzania kama lango la Afrika Mashariki na Kati. Ofisi hiyo pia inaongeza ushiriki wa Tanzania na ukanda huu katika masoko ya fedha za Kiislamu, ambayo thamani yake duniani inazidi dola za Marekani trilioni 4.

Neema Mori, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, alisema hatua hiyo inaakisi kuongezeka kwa imani kwa Benki hiyo kufanya kazi kwa viwango vya juu zaidi duniani. “Hiki ni kielelezo ni kauli kuhusu utawala bora, uwezo na uaminifu wa Benki yetu kimataifa,” alisema. “Uwepo wa Benki ya CRDB Dubai unaonesha kuwa benki za Afrika zinaweza kuanzisha ushirikiano wa kimataifa huku zikiendelea kuzingatia vipaumbele vya maendeleo ya Afrika.”

Viongozi wa Mamlaka ya Huduma za Fedha ya Dubai (DFSA) wameikaribisha Benki ya CRDB katika Kituo cha Fedha cha Kimataifa Dubai (DIFC), wakibainisha kuwa uwepo wa benki ya Kiafrika yenye mizizi imara ya kikanda unaimarisha korido ya fedha kati ya Afrika na Mashariki ya Kati, na kuboresha mtiririko wa mitaji ya muda mrefu kuelekea masoko yanayochipukia.
Posted by MROKI On Thursday, January 22, 2026 No comments





Waziri wa Nishati Mhe. Deogratius Ndejembi, leo tarehe 22 Januari, 2026 amefungua rasmi Kikao cha 55 cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kinachofanyika mkoani Dodoma.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Waziri Ndejembi amemshukuru Mhe. Rais Dkt Samia kwa kuboresha maslahi na stahiki za wafanyakazi wa TANESCO, huku akisisitiza usimamizi madhubuti wa masuala ya haki za wafanyakazi na kuimarisha ushirikiano mahali pa kazi, pamoja na kuendeleza utoaji wa elimu kwa umma kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu huduma ya umeme. 

"Natambua mmekutana hapa  kujadili kwa kina mambo yanayowahusu wafanyakazi naomba mhakikishe mnazungumza yote na kukubaliana ili kuendelea kuboresha utendaji wa shirika na maslahi ya wafanyakazi''.

Amehimiza pia umuhimu wa kuendelea kuboresha utoaji wa huduma bora na za uhakika za umeme kwa wateja wake nchini.

Akimkaribisha katika kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la umeme Bw. Lazaro Twange amemshukuru Mhe Waziri kwa kukubali wito wa kuja kufungua kikao hicho na kumuahidi kuwa wataendelea kusimamia haki za wafanyakazi na kuhakikisha wanakuwa na matokeo katika utendaji.

“Kipekee nikushukuru kwa kuitikia wito wa kuja kutufungulia kikao hiki, kama Mwenyekiti wa baraza hili nikuahidi kuwa nitaenda kuyasimamia yote tutakayojadili hapa kwa ajili ya kuleta tija na maendeleo ya Shirika hili na kuongeza ufanisi katika kuhudumia wananchi”, alieleza Twange. 

Kikao hicho kimewakutanisha viongozi wa TANESCO, wawakilishi wa Chama cha Wafanyakazi (TUICO), Wakurugenzi wa Kanda, pamoja na wawakilishi wa wafanyakazi kutoka kampuni tanzu na ofisi mbalimbali za mikoa nchini.
Posted by MROKI On Thursday, January 22, 2026 No comments







Na Mwandishi wetu, Dodoma
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa ambao ofisi zao zitabainika kuhusika au kusababisha migogoro katika shughuli za uchimbaji wa madini, akisisitiza ulazima wa kuzingatia kikamilifu Sheria na Kanuni za Madini katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mhe. Mavunde ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi  kikao cha Menejimenti cha Tume ya Madini kilichowakutanisha Wakurugenzi, Mameneja na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, kilicholenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka, pamoja na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika Sekta ya Madini.

Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo; Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo; Kamishna wa Tume ya Madini, Mhandisi Theonestina Mwasha, pamoja na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo.

Waziri Mavunde amesema kumekuwepo na baadhi ya maafisa katika Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa wanaochangia migogoro ya mara kwa mara kwenye maeneo ya uchimbaji wa madini kwa kutoa leseni kwa waombaji wasiostahili, hali inayosababisha malalamiko na migongano baina ya wachimbaji.

“Nikiona kwenye ofisi yako kuna migogoro ya wachimbaji wa madini na kujiridhisha bila shaka kuwa ofisi inahusika, sitasita kuchukua hatua kali ikiwemo kukuondoa kwenye nafasi uliyokuwa nayo,” amesisitiza Mhe. Mavunde.

Ameagiza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuhakikisha wanazingatia misingi ya haki, uwazi na weledi katika utoaji wa huduma, sambamba na kuhamasisha wananchi wengi zaidi kuomba leseni za madini kwa kuweka mazingira rafiki na wezeshi ya uwekezaji.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuwasilisha ndani ya siku saba orodha ya leseni kubwa za utafiti wa madini zisizofanyiwa kazi, ili hatua za kisheria zichukuliwe ikiwemo kuandikiwa hati za makosa na kufutiwa leseni hizo. Aidha, amemtaka Mkurugenzi wa Leseni kuwasilisha orodha ya kampuni zenye leseni kubwa za utafiti kwa ajili ya ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wake.

“Mimi kwa kushirikiana na Naibu Waziri tutahakikisha tunafuatilia kila leseni. Zile zitakazobainika kutofanyiwa kazi zitafutwa na maeneo hayo kupewa wachimbaji wadogo wa madini,” amesema.

Kadhalika, amemtaka Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini kuhakikisha kuwa kabla ya Juni 30, 2026, mfumo wa e-leseni unaowezesha wateja kupata huduma bila kufika ofisini unaanza kufanya kazi kikamilifu, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kupunguza urasimu katika utoaji wa huduma.

Vilevile, Waziri Mavunde amewataka wamiliki wa leseni za madini kuhakikisha wanazifanyia kazi leseni walizopewa, akionya kuwa leseni zitakazobainika kutofanyiwa kazi zitachukuliwa hatua ikiwemo kufutwa na kupewa wawekezaji wengine wenye dhamira ya dhati.

Pia amewaagiza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuwasilisha kabla ya Februari 28, 2026, taarifa ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wanawake na vijana kupitia Mradi wa Mining for a Brighter Tomorrow (MBT).

Katika kuimarisha utendaji kazi, Waziri Mavunde amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano miongoni mwa Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, hususan katika kushughulikia changamoto za sekta, huku akiwahimiza kusimamia maadili ya watumishi walio chini yao, akibainisha kuwa wao ndiyo taswira ya Wizara ya Madini kwa wananchi.

Wakati huo huo, Waziri Mavunde ameipongeza Tume ya Madini kwa kuvuka malengo ya makusanyo ya maduhuli kwa miaka mfululizo, akieleza kuwa makusanyo yameongezeka kutoka shilingi bilioni 161 mwaka 2015/2016 hadi kufikia shilingi trilioni 1.071 mwaka 2024/2025, mafanikio yanayotokana na maboresho ya sheria, uanzishwaji wa masoko na vituo vya ununuzi wa madini, pamoja na kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato.

Ameongeza kuwa kwa kipindi cha Julai 2025 hadi Januari 22, 2026, Serikali tayari imekusanya shilingi bilioni 719, sawa na asilimia 59.9 ya lengo la shilingi trilioni 1.2 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

“Hii ni hatua nzuri na nina imani kubwa kuwa tutavuka lengo lililowekwa na Serikali kabla ya Juni 30, 2026,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amempongeza Waziri Mavunde kwa kuendelea kuaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa Wizara na taasisi zake zitaendelea kushirikiana kwa karibu ili Sekta ya Madini izidi kuimarika.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, pamoja na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo, wameishukuru Serikali kwa maelekezo na maboresho yanayoendelea kufanywa katika utoaji wa huduma na upatikanaji wa vitendea kazi ndani ya Tume ya Madini.
Posted by MROKI On Thursday, January 22, 2026 No comments








Na Mwandishi wetu, Dodoma
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameipongeza Sekta ya Madini kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika kuongeza makusanyo ya mapato ya Serikali na hivyo  kuiwezesha Tanzania kuandika historia mpya ya uendeshaji wa sekta hiyo Barani Afrika.

Dkt. Mwigulu amesema mafanikio hayo yametokana na mageuzi makubwa ya kisera, kisheria na kiutendaji yaliyofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Madini, yaliyoiwezesha sekta hiyo kuwa jumuishi na shirikishi, huku Watanzania hususan vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum wakishiriki kikamilifu katika mnyororo mzima wa thamani wa madini.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo Januari 22, 2026, wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Wizara ya Madini lililopo katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Amesema hapo awali sekta ya madini haikuwashirikisha ipasavyo Watanzania katika uchumi wa rasilimali hizo, hali iliyosababisha manufaa ya sekta hiyo kuwafikia wananchi kwa kiwango kidogo. Hata hivyo, maboresho yaliyofanywa na Serikali yamebadilisha taswira hiyo na kuifanya sekta ya madini kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa taifa.

Kutokana na mafanikio hayo, Dkt. Mwigulu amesema Tanzania imekuwa kielelezo cha kuigwa Barani Afrika, huku nchi jirani zikifika nchini kujifunza mbinu bora za uendeshaji wa sekta ya madini, hususan katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo kupitia mafunzo ya kitaalamu, upatikanaji wa teknolojia ya kisasa, pamoja na mikopo yenye riba nafuu.

Ameeleza kuwa hatua hizo zimeongeza mchango wa uchimbaji mdogo katika Pato la Taifa na kusaidia kukuza ajira, kipato cha wananchi na mapato ya Serikali.

Akizungumzia utafiti wa madini, Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Madini kupitia taasisi zake kuongeza kasi ya utafiti wa kina wa madini kutoka asilimia 16 iliyopo sasa, akisisitiza kuwa taarifa sahihi na za uhakika za rasilimali ndizo msingi wa kuvutia uwekezaji wa kimkakati.

Kuhusu migogoro katika sekta ya madini, Waziri Mkuu ameitaka Tume ya Madini kuchukua hatua za haraka na za mapema kuzuia na kutatua migogoro, hususan inayowahusu wachimbaji wadogo ambao mara nyingi wamekuwa mstari wa mbele kugundua maeneo yenye madini. Ameelekeza wachimbaji hao wapewe kipaumbele katika ugawaji wa leseni ili kulinda haki zao na kuongeza tija katika uzalishaji.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. William Lukuvi, ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa usimamizi thabiti wa Mradi wa Mji wa Serikali Mtumba, akieleza kuwa majengo 24 kati ya 29 yamekamilika na watumishi tayari wamehamia, huku utekelezaji wa mradi ukifikia zaidi ya asilimia 90.

Naye, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, ameipongeza Serikali kwa kufanikisha ujenzi wa jengo la Wizara ya Madini, ambapo wizara ilihamia rasmi Mei 25, 2025, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesema jengo hilo lenye ghorofa sita lina uwezo wa kuhudumia watumishi 360, ambapo hadi sasa watumishi 160 tayari wamehamia, hali inayoongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.

Sekta ya Madini imeendelea kuvuka malengo ya makusanyo kwa miaka sita mfululizo, ambapo mapato yameongezeka kutoka shilingi bilioni 161 mwaka 2015/2016 hadi kufikia shilingi trilioni 1.071 mwaka 2024/2025.

Aidha, katika kipindi cha Julai 2025 hadi Januari 22, 2026, Serikali tayari imekusanya shilingi bilioni 719, sawa na asilimia 59.9 ya lengo la shilingi trilioni 1.2 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Posted by MROKI On Thursday, January 22, 2026 No comments




Na Mwandishi Wetu, Accra, Ghana
Tanzania kupitia Tume ya Madini imefanikiwa kufanya ziara ya kikazi kwa taasisi mbili muhimu za sekta ya madini yaani Ghana Chamber of Mines na Ghana Extractive Industries Transparency Initiative (GHEITI) ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha usimamizi, uwazi, uwekezaji na maendeleo endelevu katika  Sekta ya Madini.

Ziara hiyo imelenga kubadilishana uzoefu wa kitaalam na kujifunza kwa vitendo namna Ghana imefanikiwa kuunganisha Serikali, sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo katika kusimamia rasilimali za madini kwa tija, uwajibikaji na maslahi mapana ya taifa. Taasisi hizo zinatambulika kimataifa kwa mchango wao katika kuimarisha sera bora, kukuza uwekezaji endelevu na kuhakikisha uwazi katika mapato yatokanayo na sekta ya madini.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Ghana Chamber of Mines amesema ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na sekta binafsi ni nguzo muhimu ya mafanikio ya sekta ya madini nchini humo. Amesisitiza kuwa sera za ushirikishwaji wa wananchi (local content) haziwezi kuleta matokeo chanya endapo hazitakuwa na msingi thabiti wa kibiashara unaoonesha manufaa ya wazi kwa pande zote zinazohusika.

“Tunaposhirikiana na Serikali, matokeo yanakuwa ya manufaa makubwa zaidi, jambo ambalo ni moja ya vipaumbele vya taasisi yetu. Ili sera za ushirikishwaji wa wananchi ziwe na maana na matokeo endelevu, ni lazima ziwe na msingi imara wa kibiashara unaoonesha faida zake kwa Serikali, wawekezaji na wananchi,” amesema.

Kwa upande wa GHEITI, ujumbe wa Tanzania umejifunza kwa kina mifumo ya uwazi na uwajibikaji katika ukusanyaji na matumizi ya mapato ya madini, ikiwemo namna taarifa za sekta ya uziduaji zinavyowekwa wazi kwa umma ili kujenga imani kwa wananchi na wadau wa maendeleo.

Ziara hiyo imewezesha Tume ya Madini kupata maarifa muhimu kuhusu mbinu bora za usimamizi wa sekta ya madini, utekelezaji wa sera za uwazi, pamoja na mikakati ya kukuza uwekezaji unaozingatia maendeleo endelevu na ustawi wa jamii zinazozunguka maeneo ya migodi.
Posted by MROKI On Thursday, January 22, 2026 No comments


Watumishi wa Wizara ya Maji wakimsikiliza Waziri Muu, Dkt. Mwigulu Nchemba alipozungumza wakati alipotembelea makao makuu ya Wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma, Januari 22, 2026.
 Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza na watumishi wa Wizara ya Maji alipotembelea Makao Makuu ya Wizara hiyo, Mtumba jijini Dodoma, Januari 22, 2026. Kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, William Lukuvi, wa pili kulia ni Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri .
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza na watumishi wa Wizara ya Maji alipotembelea Makao Makuu ya Wizara hiyo, Mtumba jijini Dodoma, Januari 22, 2026.
 Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba akisikiliza maelezo kutoka kwa Waziri wa Madini, Anthony Mavunde alipotembelea Makao Maku ya Wizara ya Madini jijini Dodoma, Januari 22, 2026. Kulia ni Waziri wa chi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi.

**************
 WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa Serikali inataka kazi zote zifanyike makao makuu ya nchi ili kusogeza huduma karibu na Wananchi.
 
Amesema hayo leo Alhamisi (Januari 22, 2026) alipotembelea Ofisi za Wizara ya Maji na Wizara ya Madini zilizopo mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma.
 
“Ninawapongeza sana, mmehamia Makao Makuu, taasisi zote za Serikali zinapaswa kutambua kwamba makao makuu ya nchi ni Dodoma, na huduma zote zinapaswa kutolewa hapa, hii sio kambi na wala hatutakuwa na Makao Makuu mbili zilizo sambamba”.
 
Pia, Mheshimiwa Mwigulu ameziagiza Taasisi zote ambazo zimeshakamilisha ujenzi wa majengo katika makao makuu kuyatoa majengo hayo kwa Taasisi ambazo haziwajibiki kuhamia Dodoma lakini bado zimepanga.
 
“Mheshimiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu mwelekeze Katibu Mkuu atengeneze timu ifanye tathmini ya majengo yote ya Serikali yaliyoko Dar es Salaam ambayo hayana matumizi ili tuyagawe kwa taasisi nyingine ambazo zimepanga, angalia Serikali ina majengo yasiyotumika”
 
Kadhalika Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema kwa kuwa Ofisi za Serikali zipo karibu, hivyo hakuna haja ya kuandikiana  barua za masuala mbalimbali ya utekelezaji badala yake waweke mpango wa kutembeleana katika ofisi husika ili kutatua jambo lilikokwama kwa wakati”
 
Akizungumza na Watumishi wa Wizara ya Maji Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amewataka kwenda katika hatua ya kukomesha kabisa upotevu wa maji. “Tunapokwenda kutekeleza dira mpya tunatakiwa twende na ustaarabu na miundombinu inayomuhakikishia mtanzania uhakika wa kupata maji”
Akizungumza wakati akikagua majengo ya Wizara ya Madini, mheshimiwa Dkt. Mwigulu amewataka wataalam wa madini kuendeleza jitihada kwenye tafiti za madini ili kujua utajiri uliopo nchini.
 
Kwa Upande wake, Waziri wa Maji Jumaa Aweso amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya maamuzi ya kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi kubwa zilizowahakikishia watumishi mazingira mazuri ya ufanyaji kazi.
Naye, Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema kuwa ujenzi wa jengo hilo umesaidia kutekeleza maagizo ya Rais Dkt. Samia ya kuhakikisha huduma zote zinatolewa katika eneo hilo, watanzania wote waliokuwa wanapata changamoto ya kupata huduma kwasasa changamoto hiyo imeondoka" 

Posted by MROKI On Thursday, January 22, 2026 No comments
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi akizungumza kabla ya hafla ya makabidhiano kati ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Kituo cha Taifa cha Ufuatiaji Kaboni (NCMC) mjini Morogoro Januari 21,2026.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi akizungumza kabla ya hafla ya makabidhiano kati ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Kituo cha Taifa cha Ufuatiaji Kaboni (NCMC) mjini Morogoro Januari 21,2026.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi (mwenye tai) akiwa kwenye ziara ya kutembelea jengo la Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) kabla ya hafla ya kukabidhi Ofisi kati ya Chuo Kikuu Kilimo cha Sokoine (SUA) na Kituo cha Taifa cha Ufuatiaji Kaboni (NCMC) mjini Morogoro Januari 21, 2026.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wakati wa hafla ya makabidhiano ya Ofisi kati ya Chuo Kikuu Kilimo cha Sokoine (SUA) na Kituo cha Taifa cha Ufuatiaji Kaboni (NCMC) mjini Morogoro Januari 21, 2026.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi amekitaka Kituo cha Taifa cha Kufuatilia Kaboni (NCMC) kuimarisha ushiriki wa Tanzania katika masoko ya kimataifa ya kaboni kwa kuimarisha miradi ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira.

Hayo ameyasema Januari 21, 2026 wakati wa makabidhiano ya kituo hicho kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kwenda Ofisi ya Makamu wa Rais, ambapo Dkt. Muyungi amefafanua kuwa kituo kitachangia kukua kwa uchumi wa Taifa na kujenga uwezo wa Tanzania kushiriki katika biashara hiyo.

“Katika Dira ya 2050 tumejiwekea malengo ya kukusanya mapato ya dola bilioni moja kwa mwaka kutoka katika biashara ya kaboni ya nchi kavu na dola bilioni moja kutoka uchumi wa bluu”

Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa SUA Prof. Raphael Chigunda amemhakikishia Katibu Mkuu kuwa chuo hicho kitaendelea kutoa ushirikiano wa kitaalamu katika masuala ya biashara ya kaboni ili kituo kiendelee kuibua na kuandaa miradi ya kaboni na hatimaye Taifa na wananchi waweze kunufaika.

Awali akaiongea katika hafla hiyo; aliyekuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa NCMC Prof. Eliakimu Zahabu amesema ataendelea kutoa ushirikiano kwa wataalamu wa kituo hususan katika Kutafuta fursa za uwekezaji katika biashara ya kaboni.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Kituo hucho Bi. Kathryn Kigaraba, amebainisha kuwa Kituo hicho kitaendelea na usimamizi wa gesi joto; na biashara ya kaboni na masoko ya kaboni ili kuwa taaasisi muhimu katika mfumo wa kitaifa wa mabadiliko ya tabianchi na masoko ya kaboni. 

Kituo hicho kimeanzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 29 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura ya 191 (Marekebisho ya 2025), Kituo hicho ni taasisi ya kimkakati ya kitaifa yenye jukumu la kuratibu shughuli zinazohusiana nausimamizi wa gesi joto pamooja na biashara ya kaboni na masoko ya kaboni. 

Biashara ya Kaboni ni mfumo wa kiuchumi unaoruhusu uuzaji na ununuzi wa Viwango vya Kaboni ambapo lengo lake ni kupunguza gesijoto angani.
 
Posted by MROKI On Thursday, January 22, 2026 No comments
Chuo cha VETA Shinyanga hadi napotoa taarifa hii, kina uwezo wa kupokea wanafunzi wa Bweni 179 tu. Huo ndiyo uwezo wa juu kabisa wa chuo.

Katika mwaka huu wa masomo wa 2026, Chuo cha VETA Shinyanga kimepangiwa jumla ya wanafunzi 635, ambapo wanafunzi 179 wamepangiwa kukaa Bweni na wanafunzi 456 ni wa kutwa.

Hata hivyo kutokana na uhitaji mkubwa wa vijana kujiunga VETA na ili kutowaacha vijana wengi nje ya mifumo ya kujenga ujuzi na kujiajiri, Mamlaka za VETA ziliamua kuanzisha programu maalum ya masomo ya jioni (Evening Classes) ambayo inaanza kwa mara ya kwanza mwaka huu wa 2026 na wakati inaanzishwa ilinuiwa ichukue wanafunzi wa kutwa ambao watatokea nyumbani.

Kupitia programu hiyo ya masomo ya jioni ya VETA, Chuo cha VETA Shinyanga kimepangiwa tena wanafunzi wapya 139, lakini wanafunzi 50 kati ya hawa 139  wanasomeka watakuwa Bweni. Ndiyo kusema kuwa kuna jumla ya wanafunzi 229 waliopangiwa kusoma Bweni lakini Chuo kikiwa na nafasi 179 tu za Bweni.

HATUA
Nimeuelekeza Uongozi wa Chuo cha VETA Shinyanga, na tumekubaliana kuwa, darasa moja ambalo limeshapauliwa, kwa sababu halina mahitaji ya haraka, ligeuzwe kuwa bweni na wanafunzi wa ziada waanze kupata mahali pa kuishi wakati Mamlaka za VETA zinaweka utaratibu wa kutatua changamoto za aina hii, na maelekezo yangu yameanza kutekelezwa.

Nimeelekeza Chuo cha VETA Shinyanga kiendelee kupokea wanafunzi wote wanaotoka katika mkoa wowote na tunasimamia kuhakikisha kuwa wote wanakaa Bweni kama inavyosomeka kwenye mfumo.

Kama kuna mwanafunzi yeyote amepangiwa Bweni lakini hadi sasa yuko mtaani au anatafuta chumba mtaani kwa hoja kuwa amekosa nafasi ya bweni chuoni, mwanafunzi huyo atembelee ofisi ya Mkuu wa Wilaya au awasiliane nami moja kwa moja kupitia namba ya simu 0787536759.

Hadi sasa, hakuna mwanafunzi wa VETA ambaye ameporwa nafasi yake ya bweni ili apewe mwanafunzi wa kutwa - changamoto iliyopo ni hii ya idadi kubwa ya udahili katika mfumo wa bweni ambayo imekuwa juu ya uwezo wa chuo.
Julius S. Mtatiro (Adv),
Mkuu wa Wilaya,
Shinyanga.
Posted by MROKI On Thursday, January 22, 2026 No comments

January 21, 2026

Na Mwandishi Wetu.
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imewasisitiza waajiri kwenye vyombo vya habari nchini kuzingatia kikamilifu masharti ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, hususan wanapoajiri au kuwasainisha mikataba watumishi wa kada ya habari, ili kuepuka migogoro ya kisheria inayoweza kujitokeza baadaye.

Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, tarehe 20-21 Januari, 2026 wakati wa ziara ya kikazi ya Bodi katika mikoa ya Dodoma na Iringa, ilipotembelea vyombo kadhaa vya habari kwa lengo la kukagua kiwango cha uzingatiaji wa Sheria hiyo kwa watumishi wanaojihusisha na shughuli za kihabari, wakiwemo wahariri, waandishi wa habari, watangazaji, wapiga picha waandaaji na waandishi wa kujitegemea
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Wakili Kipangula amesema Bodi imebaini uwepo wa waandishi wenye sifa stahiki kwa mujibu wa Sheria kwenye vyombo hivyo, lakini bado hawajajisajili katika Mfumo wa TAI-HABARI ili kuomba ithibati na vitambulisho vya uandishi wa habari, hali inayoweza kuwaweka waajiri na waajiriwa katika hatari ya kukiuka Sheria.

Ameeleza kuwa ni muhimu kwa waajiri kuhakikisha kuwa watumishi wote wa kada ya habari wanakuwa wamekamilisha taratibu za usajili na kupata ithibati kabla ya kupewa majukumu au kuajiriwa ili kulinda uhalali wa ajira na kuepuka athari za kisheria.
Aidha, Wakili Kipangula amesema changamoto nyingine iliyobainika katika baadhi ya vyombo vya habari ni malipo madogo ya posho au mishahara kwa waandishi, hali inayohitaji mjadala mpana na mikakati maalum ya pamoja kati ya waajiri, wadau wa habari na Serikali ili kuhakikisha mazingira bora na ya haki ya kazi kwa waandishi wa habari.

Hata hivyo, amepongeza baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari waliobainika kuzingatia kwa umakini masharti ya Sheria, kushughulikia changamoto za waandishi wao kwa uwazi, na kufanya uwekezaji mkubwa unaolenga kujenga mazingira wezeshi, salama na rafiki ya utendaji wa kazi za kihabari.

Kwa mujibu wa Wakili Kipangula, juhudi hizo ni mfano wa kuigwa na zinachangia moja kwa moja katika kulinda hadhi ya taaluma ya habari, kuongeza weledi wa waandishi na kuimarisha uaminifu wa vyombo vya habari kwa jamii.
Posted by MROKI On Wednesday, January 21, 2026 No comments
  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo