Na:
OWM (KAM) – Dodoma
Serikali
kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano imetangaza vijana 5,746
kujiunga na mafunzo ya uanagenzi ambayo yatawawezesha kupata ujuzi wa vitendo utakao
wasaidia kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi kwa kujiajiri na
kuajiri wenzao.
Hayo
yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na
Mahusiano Mhe. Deus Clement Sangu wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari
uliofanyika leo Januari 16, 2026, Jijini Dodoma ukilenga kuelezea vijana
waliochaguliwa kushiriki mafunzo ya Uanagenzi kwa mwaka 2025/2026.
Aidha,
amesema mafunzo hayo yanafadhiliwa na Serikali kwa asilimia 100.
Mhe.
Sangu amesema, mafunzo hayo ya ufundi stadi yatatolewa katika vyuo 47 nchini
kupitia fani za ubunifu wa mitindo na ushonaji nguo, ufundi bomba, uashi,
useremala, uchomeleaji na uungaji vyuma, upakaji rangi na maandishi ya alama,
upishi, utengenezaji wa vipuri vya mitambo, ufundi magari na mitambo, umeme wa
majumbani na viwandani, umeme wa magari, huduma za hoteli na utalii, ukataji
madini na ufundi vyuma.
“Fani
hizi ni muhimu sana kwa vijana wetu, kwa kuwa zitawawezesha kupata ujuzi ambao
utawawezesha kuajiriwa au kujiajiri,” amesema
Vilevile
amesema kuwa, Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,
imeendelea kuweka mikakati na kutekeleza afua mbalimbali zitakazowezesha kuwa
na jamii yenye ustawi na kujenga nguvu kazi yenye ujuzi utakao wawezesha
kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Amesema,
afua hizo ni pamoja na utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi kwa
njia ya Uanagenzi inayolenga kuimarisha nguvukazi ya taifa ili kumudu ushindani
katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi kwa kupata ujuzi unaoendana na
mahitaji ya soko la ajira na hatimaye kuweza kuajiriwa au kujiajiri.
Kadhalika,
Waziri Sangu amevitaka vyuo vilivyopata dhamana ya kutoa mafunzo hayo, kutoa
ushirikiano kwa vijana waliochaguliwa, kuwafundisha na kuwasimamia vyema
kipindi chote cha mafunzo yao. Pia, ametoa wito kwa vijana waliochaguliwa
kushiriki mafunzo kusoma kwa bidii, kuwa na nidhamu na kufuata sheria na
taratibu za vyuo.
Posted by MROKI
On Friday, January 16, 2026
No comments
0 comments:
Post a Comment