Nafasi Ya Matangazo

January 22, 2026





Na Mwandishi Wetu, Accra, Ghana
Tanzania kupitia Tume ya Madini imefanikiwa kufanya ziara ya kikazi kwa taasisi mbili muhimu za sekta ya madini yaani Ghana Chamber of Mines na Ghana Extractive Industries Transparency Initiative (GHEITI) ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha usimamizi, uwazi, uwekezaji na maendeleo endelevu katika  Sekta ya Madini.

Ziara hiyo imelenga kubadilishana uzoefu wa kitaalam na kujifunza kwa vitendo namna Ghana imefanikiwa kuunganisha Serikali, sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo katika kusimamia rasilimali za madini kwa tija, uwajibikaji na maslahi mapana ya taifa. Taasisi hizo zinatambulika kimataifa kwa mchango wao katika kuimarisha sera bora, kukuza uwekezaji endelevu na kuhakikisha uwazi katika mapato yatokanayo na sekta ya madini.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Ghana Chamber of Mines amesema ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na sekta binafsi ni nguzo muhimu ya mafanikio ya sekta ya madini nchini humo. Amesisitiza kuwa sera za ushirikishwaji wa wananchi (local content) haziwezi kuleta matokeo chanya endapo hazitakuwa na msingi thabiti wa kibiashara unaoonesha manufaa ya wazi kwa pande zote zinazohusika.

“Tunaposhirikiana na Serikali, matokeo yanakuwa ya manufaa makubwa zaidi, jambo ambalo ni moja ya vipaumbele vya taasisi yetu. Ili sera za ushirikishwaji wa wananchi ziwe na maana na matokeo endelevu, ni lazima ziwe na msingi imara wa kibiashara unaoonesha faida zake kwa Serikali, wawekezaji na wananchi,” amesema.

Kwa upande wa GHEITI, ujumbe wa Tanzania umejifunza kwa kina mifumo ya uwazi na uwajibikaji katika ukusanyaji na matumizi ya mapato ya madini, ikiwemo namna taarifa za sekta ya uziduaji zinavyowekwa wazi kwa umma ili kujenga imani kwa wananchi na wadau wa maendeleo.

Ziara hiyo imewezesha Tume ya Madini kupata maarifa muhimu kuhusu mbinu bora za usimamizi wa sekta ya madini, utekelezaji wa sera za uwazi, pamoja na mikakati ya kukuza uwekezaji unaozingatia maendeleo endelevu na ustawi wa jamii zinazozunguka maeneo ya migodi.
Posted by MROKI On Thursday, January 22, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo