Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameipongeza Sekta ya Madini kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika kuongeza makusanyo ya mapato ya Serikali na hivyo kuiwezesha Tanzania kuandika historia mpya ya uendeshaji wa sekta hiyo Barani Afrika.
Dkt. Mwigulu amesema mafanikio hayo yametokana na mageuzi makubwa ya kisera, kisheria na kiutendaji yaliyofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Madini, yaliyoiwezesha sekta hiyo kuwa jumuishi na shirikishi, huku Watanzania hususan vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum wakishiriki kikamilifu katika mnyororo mzima wa thamani wa madini.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo Januari 22, 2026, wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Wizara ya Madini lililopo katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Amesema hapo awali sekta ya madini haikuwashirikisha ipasavyo Watanzania katika uchumi wa rasilimali hizo, hali iliyosababisha manufaa ya sekta hiyo kuwafikia wananchi kwa kiwango kidogo. Hata hivyo, maboresho yaliyofanywa na Serikali yamebadilisha taswira hiyo na kuifanya sekta ya madini kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa taifa.
Kutokana na mafanikio hayo, Dkt. Mwigulu amesema Tanzania imekuwa kielelezo cha kuigwa Barani Afrika, huku nchi jirani zikifika nchini kujifunza mbinu bora za uendeshaji wa sekta ya madini, hususan katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo kupitia mafunzo ya kitaalamu, upatikanaji wa teknolojia ya kisasa, pamoja na mikopo yenye riba nafuu.
Ameeleza kuwa hatua hizo zimeongeza mchango wa uchimbaji mdogo katika Pato la Taifa na kusaidia kukuza ajira, kipato cha wananchi na mapato ya Serikali.
Akizungumzia utafiti wa madini, Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Madini kupitia taasisi zake kuongeza kasi ya utafiti wa kina wa madini kutoka asilimia 16 iliyopo sasa, akisisitiza kuwa taarifa sahihi na za uhakika za rasilimali ndizo msingi wa kuvutia uwekezaji wa kimkakati.
Kuhusu migogoro katika sekta ya madini, Waziri Mkuu ameitaka Tume ya Madini kuchukua hatua za haraka na za mapema kuzuia na kutatua migogoro, hususan inayowahusu wachimbaji wadogo ambao mara nyingi wamekuwa mstari wa mbele kugundua maeneo yenye madini. Ameelekeza wachimbaji hao wapewe kipaumbele katika ugawaji wa leseni ili kulinda haki zao na kuongeza tija katika uzalishaji.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mhe. William Lukuvi, ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa usimamizi thabiti wa Mradi wa Mji wa Serikali Mtumba, akieleza kuwa majengo 24 kati ya 29 yamekamilika na watumishi tayari wamehamia, huku utekelezaji wa mradi ukifikia zaidi ya asilimia 90.
Naye, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, ameipongeza Serikali kwa kufanikisha ujenzi wa jengo la Wizara ya Madini, ambapo wizara ilihamia rasmi Mei 25, 2025, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema jengo hilo lenye ghorofa sita lina uwezo wa kuhudumia watumishi 360, ambapo hadi sasa watumishi 160 tayari wamehamia, hali inayoongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.
Sekta ya Madini imeendelea kuvuka malengo ya makusanyo kwa miaka sita mfululizo, ambapo mapato yameongezeka kutoka shilingi bilioni 161 mwaka 2015/2016 hadi kufikia shilingi trilioni 1.071 mwaka 2024/2025.
Aidha, katika kipindi cha Julai 2025 hadi Januari 22, 2026, Serikali tayari imekusanya shilingi bilioni 719, sawa na asilimia 59.9 ya lengo la shilingi trilioni 1.2 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.












0 comments:
Post a Comment