Nafasi Ya Matangazo

January 22, 2026

Chuo cha VETA Shinyanga hadi napotoa taarifa hii, kina uwezo wa kupokea wanafunzi wa Bweni 179 tu. Huo ndiyo uwezo wa juu kabisa wa chuo.

Katika mwaka huu wa masomo wa 2026, Chuo cha VETA Shinyanga kimepangiwa jumla ya wanafunzi 635, ambapo wanafunzi 179 wamepangiwa kukaa Bweni na wanafunzi 456 ni wa kutwa.

Hata hivyo kutokana na uhitaji mkubwa wa vijana kujiunga VETA na ili kutowaacha vijana wengi nje ya mifumo ya kujenga ujuzi na kujiajiri, Mamlaka za VETA ziliamua kuanzisha programu maalum ya masomo ya jioni (Evening Classes) ambayo inaanza kwa mara ya kwanza mwaka huu wa 2026 na wakati inaanzishwa ilinuiwa ichukue wanafunzi wa kutwa ambao watatokea nyumbani.

Kupitia programu hiyo ya masomo ya jioni ya VETA, Chuo cha VETA Shinyanga kimepangiwa tena wanafunzi wapya 139, lakini wanafunzi 50 kati ya hawa 139  wanasomeka watakuwa Bweni. Ndiyo kusema kuwa kuna jumla ya wanafunzi 229 waliopangiwa kusoma Bweni lakini Chuo kikiwa na nafasi 179 tu za Bweni.

HATUA
Nimeuelekeza Uongozi wa Chuo cha VETA Shinyanga, na tumekubaliana kuwa, darasa moja ambalo limeshapauliwa, kwa sababu halina mahitaji ya haraka, ligeuzwe kuwa bweni na wanafunzi wa ziada waanze kupata mahali pa kuishi wakati Mamlaka za VETA zinaweka utaratibu wa kutatua changamoto za aina hii, na maelekezo yangu yameanza kutekelezwa.

Nimeelekeza Chuo cha VETA Shinyanga kiendelee kupokea wanafunzi wote wanaotoka katika mkoa wowote na tunasimamia kuhakikisha kuwa wote wanakaa Bweni kama inavyosomeka kwenye mfumo.

Kama kuna mwanafunzi yeyote amepangiwa Bweni lakini hadi sasa yuko mtaani au anatafuta chumba mtaani kwa hoja kuwa amekosa nafasi ya bweni chuoni, mwanafunzi huyo atembelee ofisi ya Mkuu wa Wilaya au awasiliane nami moja kwa moja kupitia namba ya simu 0787536759.

Hadi sasa, hakuna mwanafunzi wa VETA ambaye ameporwa nafasi yake ya bweni ili apewe mwanafunzi wa kutwa - changamoto iliyopo ni hii ya idadi kubwa ya udahili katika mfumo wa bweni ambayo imekuwa juu ya uwezo wa chuo.
Julius S. Mtatiro (Adv),
Mkuu wa Wilaya,
Shinyanga.
Posted by MROKI On Thursday, January 22, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo