Nafasi Ya Matangazo

January 19, 2026




Na Mwandishi Wetu, Tabora
Tume ya Madini Mkoa wa Tabora imeshiriki rasmi katika hafla ya uzinduzi wa miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) iliyofanyika Wilaya ya Igunga, Mkoa wa Tabora. Hafla hiyo ilifunguliwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Mhe. Sauda S. Mtondoo, na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali, wadau wa sekta ya madini pamoja na wananchi wa maeneo husika.

Miradi iliyozinduliwa inajumuisha ujenzi wa darasa moja na ofisi ya walimu katika Shule ya Msingi Mkwabi, pamoja na ujenzi wa vizimba vya maji katika Kijiji cha Nanga. Utekelezaji wa miradi hiyo unalenga kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji shuleni, sambamba na kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi, hivyo kuchangia kuboresha ustawi wa jamii.

Miradi hiyo imetekelezwa na Kampuni ya TAUR TANZANIA LTD kwa gharama ya Shilingi milioni 50 katika mwaka wa fedha 2024/2025, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kwa mujibu wa sheria na miongozo ya sekta ya madini nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, mwakilishi wa Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tabora, Nehemia Mudala alizitaka kampuni za uchimbaji madini kuendelea kutenga na kutumia fedha za CSR kwa kuzingatia vipaumbele vya Halmashauri husika, hususan vijiji vinavyozunguka maeneo ya uchimbaji. 

Aidha, alisisitiza umuhimu wa matumizi sahihi, uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za CSR, pamoja na utunzaji wa miundombinu ya miradi iliyotekelezwa ili kuhakikisha inatoa manufaa endelevu kwa jamii.

Kwa upande wake, Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Igunga aliipongeza Kampuni ya TAUR TANZANIA LTD pamoja na wadau wa sekta ya madini kwa mchango wao katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya wananchi wa Wilaya ya Igunga. 

Alisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na jamii ili kuhakikisha maendeleo yanayopatikana yanakuwa jumuishi na endelevu.

Ushiriki wa Tume ya Madini katika hafla hiyo unaakisi dhamira ya Serikali ya kuhakikisha sekta ya madini inaendelea kuchangia kikamilifu maendeleo ya jamii kupitia utekelezaji madhubuti wa miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii.
Posted by MROKI On Monday, January 19, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo