Nafasi Ya Matangazo

January 19, 2026

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza na Waumini wa Kanisa Kuu Anglikana la Roho Mtakatifu Dodoma mara baada ya kushiriki Ibada ya jumapili katika kanisa hilo leo tarehe 18 Januari,2026.
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza na Waumini wa Kanisa Kuu Anglikana la Roho Mtakatifu Dodoma mara baada ya kushiriki Ibada ya jumapili katika kanisa hilo leo tarehe 18 Januari,2026.
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akishiriki Ibada ya Jumapili katika Kanisa Kuu Anglikana la Roho Mtakatifu Dodoma leo tarehe 18 Januari, 2026. Pembeni yake ni Prof. Kabudi Palamagamba, Waziri wa ofisi ya Rais-Kazi Maalum.

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba, akisalimiana na Mhashamu Dkt. Dickson Chilongani, Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika Dodoma nje ya jengo la Kanisa Kuu Anglikana la Roho Mtakatifu Dodoma mara baada ya kumalizika kwa Ibada leo tarehe 18 Januri, 2026.
****************

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Januari 18, 2026 ameshiriki Ibada ya Jumapili katika Kanisa Kuu Anglikana la Roho Mtakatifu Dodoma na amesisitiza kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa dini kujenga Taifa lenye hofu ya Mungu, upendo, haki na uwajibikaji.

 

“Sote tunatambua kwamba Taasisi za dini zina nafasi ya kipekee ya kuhubiri na kufundisha maadili ya upendo, uvumilivu na kuheshimiana, ambazo ni nguzo kuu za amani ya Taifa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua na kuthamini sana mchango mkubwa wa taasisi za dini ikiwemo Kanisa la Anglikana, katika kudumisha amani, maadili mema na mshikamano wa Kitaifa.

 

Pia, Waziri Mkuu amesema kuwa ibada za Jumapili ni sehemu muhimu ya maisha ya Mkristo na ni muda wa kujitathmini, kuimarisha mahusiano yao na Mwenyezi Mungu, na kujifunza namna bora ya kuishi kwa mujibu wa mapenzi ya Mwenyezi Mungu katika familia, jamii na Taifa kwa ujumla.

 

Amesema Watanzania wanakumbushwa kuishi kwa misingi ya upendo, unyenyekevu, haki na uwajibikaji kwani Biblia inasisitiza wazi kuwa “Umejulishwa, ee mwanadamu, yaliyo mema; na Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki, kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu mbele za Mungu wako” (Mika 6:8) na maadili hayo si ya kidini pekee, bali ni msingi muhimu wa ustawi wa jamii na maendeleo ya Taifa.

 

Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema Tanzania imeendelea kuwa kielelezo cha amani, umoja na mshikamano katika ukanda wetu na barani Afrika. Amani hii si jambo la bahati, bali ni matokeo ya jitihada za pamoja za Serikali, taasisi za dini, familia na wananchi kwa ujumla.

 

Waziri Mkuu amesisitiza kuwa imani wanayojifunza na kuimarisha katika ibada inapaswa kutafsiriwa katika matendo ya uadilifu, uwajibikaji, bidii katika kazi, kuheshimu sheria na kushiriki kikamilifu katika kujenga Taifa lenye haki, amani na maendeleo endelevu. “Imani ya kweli inapaswa kuonekana kwa matendo.”

 

Kadhalika, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa waumini wote na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuwa mabalozi wa amani katika familia zao, maeneo ya kazi na katika jamii kwa ujumla kupinga vitendo vyovyote vya chuki, migawanyiko na vurugu.

 

Awali, Askofu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Central Tanganyika, Dk. Dickson Chilongani ameipongeza Serikali kwa kuendelea kushirikiana na taasisi za kidini likiwemo Kanisa Anglikana na kwamba wapo pamoja na nayo katika kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani. “Tunataka nchi iwe na amani ili shughuli ziendelee na hatutachezea amani.”

Posted by MROKI On Monday, January 19, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo