Na Mwandishi wetu, Dodoma
Jumla ya Wapiga Kura 38,151 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura watashiriki katika uchaguzi wa marudio katika Kata za Malangali iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga Mkoa wa Rukwa na Mzinga iliyopo katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,
Jaji wa Rufaa Mhe. Jacobs Mwambegele amesema hayo leo Januari 21, 2026 jijini
Ddodoma wakati akisoma risala maalum kuhusu uchaguzi katika Kata hizo utakao
fanyika Januari 22, 2026 na kusema kuwa jumla ya vituo 92 vya Kupigia Kura
vitatumika.
Aidha, amesema jumla ya wagombea sita (6)
kutoka katika vyama vya siasa vitatu (3) wanawania nafasi wazi za udiwani
katika maeneo hayo na kuvipongeza vyama vya siasa na wagombea waliojitokeza
kushiriki katika uchaguzi huo.
“Kati ya wagombea sita (06), wagombea watano
(05) sawa na asilimia 83.3 ni wanaume na mgombea mmoja (01) sawa na asilimia
16.7 ni Mwanamke. Kwa namna ya pekee, Tume inavipongeza vyama vilivyoshiriki na
wagombea waliojitokeza kushiriki,” alisema Jaji Mwambegele.
Vyama vya Siasa vinavyoshiriki uchaguzi kesho
Januari 05, 2026 vimetakiwa kuzingatia wajibu wao wa kuweka mawakala katika
vituo vyote vya zoezi la kupiga, kuhesabu na kujumlishia kura.
“Wasimamizi wa uchaguzi katika Majimbo na
Kata husika, wamekamilisha taratibu zinazoweka mazingira yanayowawezesha
mawakala wa vyama vya siasa kufuatilia mchakato mzima wa uchaguzi,” alisema
Jaji Mwambegele.
Amesema, mawakala hao, wanawajibika katika
kulinda maslahi ya vyama na wagombea wao. Hivyo, wanapaswa kuzingatia Sheria,
Kanuni, taratibu za Uchaguzi na maelekezo ya Tume katika utekelezaji wa
majukumu yao vituoni.
Jaji Mwambegele amesema vituo vitafunguliwa
saa 01:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni. Ifikapo muda wa kufunga kituo
saa 10:00 kamili jioni, kama wapiga kura bado wapo kwenye mistari, mlinzi wa
kituo atasimama nyuma ya mtu wa mwisho na zoezi la upigaji kura litaendelea
hadi wapiga kura walio kwenye mstari watakapomalizika.
“Baada ya kumaliza kupiga kura, mpiga kura
anatakiwa kuondoka eneo la kituo cha kupigia kura; na Mpiga kura awapo kituoni,
anatakiwa kufuata maelekezo yote atakayopewa na karani mwongozaji wapiga kura,”
alisema Jaji Mwambegele.
Kwa mpiga kura ambaye ameandikishwa katika
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na taarifa zake zipo katika Daftari la Kudumu
la Wapiga Kura lililopo katika kituo husika, lakini amepoteza kadi yake au kadi
yake imeharibika, ataruhusiwa kupiga Kura kwa kutumia moja wapo ya vitambulisho
cha Taifa (NIDA), Leseni ya udereva au Pasi ya kusafiria (Passport).
Jumla ya Wapiga Kura 38,151 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura watashiriki katika uchaguzi wa marudio katika Kata za Malangali iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga Mkoa wa Rukwa na Mzinga iliyopo katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.





0 comments:
Post a Comment