Nafasi Ya Matangazo

October 07, 2026


Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini ambaye ni Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Judith Kapinga amekabidhi kilo 1,000 za mbegu za kahawa kwa AMCOS 20.

Pia amekabidhi kikundi kimoja mbegu ili kiweze kuzalisha vitalu vya miche ya kahawa milioni 3.5 na kuendeleza jitihada za kuzalisha kahawa Wilayani humo.

Amekabidhi mbegu hizo  leo Oktoba 07,2026 wakati wa Ziara yake alipotembelea Halmashauri ya Mbinga iliyopo katika Jimbo hilo ambapo amesema uchumi wa Halmashauri hiyo unategemea zaidi kilimo cha kahawa.

Akitolea mfano wa msimu ulipita Kapinga alisema,  Halmashauri hiyo ilizalisha tani elfu 18 na kwa msimu huu imepanga kuzalisha tani 19 ambapo mpaka sasa imevuka malengo hayo  kabla ya msimu kuisha.

Waziri Kapinga ameongeza kuwa utoaji wa mbegu hizo ni kuchagiza uzalishaji wa kahawa kwa wingi ili kuchochea uchumi kwa wananchi wa Mbinga pamoja na upatikanaji wa mapato kwa Halmashauri. 

Mkoa wa Ruvuma kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, umejipanga kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa kutoka tani 26,088.05 za msimu 2025/2026 hadi kufikia tani 29,000 katika msimu wa kilimo 2026/2027.

Uzalishaji wa kahawa mkoani Ruvuma umekuwa ukiongezeka kwa kasi kutokana na mikakati ya serikali, matumizi ya miche ya kisasa, na usimamizi mzuri kupitia vyama vya ushirika.
 
Halmashauri ya Mji Mbinga pekee imeweka lengo la kukusanya Shilingi bilioni 5.7 za mapato kupitia ushuru na usimamizi wa karibu wa zao la kahawa kwa kushirikiana na AMCOS (Vyama vya Msingi vya Ushirika).

Posted by MROKI On Wednesday, October 07, 2026 No comments


Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amefanya ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa na Halmashauri ya Mji wa Kondoa, ambapo amekagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kusikiliza na kutatua kero za wananchi, huku akitoa wito wa maandalizi dhidi ya mvua kubwa zinazotarajiwa na kusisitiza wananchi kuendelea na shughuli za kilimo kwa kuzingatia tahadhari.

Ziara hiyo iliyofanyika Oktoba 06, 2026, imehusisha maeneo mbalimbali ya Kondoa, ikiwemo Kata ya Itaswi na Pahi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa pamoja na Kata ya Serya katika Halmashauri ya Mji wa Kondoa, ambapo Mkuu huyo wa Mkoa amekagua miradi ya elimu, maji na miundombinu, pamoja na kufanya mikutano ya hadhara na kusikiliza changamoto za wananchi.

AGIZO LA KUKAMILISHA BWAWA LA ITASWI
Akiwa Kata ya Itaswi, Mhe. Senyamule alikagua ujenzi wa Bwawa la Itaswi, mradi wenye thamani ya shilingi bilioni 5.7, unaolenga kuongeza upatikanaji wa maji na kupunguza changamoto ya maji kwa wananchi wa eneo hilo.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa TARURA Wilaya ya Kondoa, Ndugu Majid Mtili, alisema ujenzi wa bwawa hilo umekuwa ukienda kwa kasi ndogo kutokana na mkandarasi kupokea fedha za utekelezaji kwa awamu tofauti.

Mhe. Senyamule amesisitiza umuhimu wa mradi huo kukamilishwa ili wananchi wa Itaswi waanze kunufaika na uwekezaji huo, hususan katika kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji.

SHULE MPYA KUFUNGUA FURSA ZA ELIMU KONDOA

Katika Kijiji cha Potea, Kata ya Pahi, Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Mkuu wa Mkoa alitembelea na kukagua ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Potea, inayotarajiwa kukamilika mwishoni mwa Novemba 2026.

Mradi huo utakapokamilika utakuwa umegharimu shilingi milioni 540, na shule hiyo inatarajiwa kuanza kupokea wanafunzi Januari 2027, hatua inayolenga kuongeza fursa za elimu kwa watoto wa eneo hilo na maeneo jirani.

Aidha, katika Halmashauri ya Mji wa Kondoa, Kata ya Serya, Mhe. Senyamule aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa Shule mpya ya Msingi Serya, mradi ambao hadi kukamilika kwake utagharimu shilingi milioni 302.

Shule hiyo pia inatarajiwa kuanza kupokea wanafunzi Januari 2027, ikienda sambamba na juhudi za Serikali za kuongeza miundombinu ya elimu na kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kujifunzia karibu na maeneo wanayoishi.

ITASWI: SERIKALI YAENDELEA KUWEKEZA KATIKA HUDUMA ZA JAMII

Akizungumza na wananchi wa Kata ya Itaswi, Mhe. Senyamule alieleza kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika huduma za kijamii na kuboresha maisha ya wananchi.

Alitaja miongoni mwa miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Haire wenye thamani ya shilingi milioni 98, ujenzi wa Shule ya Msingi Chubi wenye thamani ya shilingi milioni 100, pamoja na utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vitatu yenye jumla ya shilingi milioni 24.5.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema uwekezaji huo unaakisi azma ya Serikali ya kuhakikisha rasilimali zinaelekezwa katika maeneo yenye mahitaji muhimu kwa wananchi na kwamba miradi inapokamilika inatoa huduma na matokeo yanayokusudiwa.

RC SENYAMULE: “TAHADHARI YA MVUA ISIWE SABABU YA KUACHA KULIMA”

Katika ziara hiyo, Mhe. Senyamule pia alitoa msisitizo kuhusu tahadhari dhidi ya mvua kubwa zinazotarajiwa, akiwataka wananchi kuzingatia utabiri na ushauri unaotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

Hata hivyo, amesisitiza kuwa tahadhari dhidi ya uwezekano wa mvua kubwa isiwe sababu ya wananchi kuacha shughuli za kilimo, bali watumie fursa ya mvua kwa kuendelea kulima huku wakizingatia ushauri wa wataalamu kuhusu maeneo salama na muda unaofaa kwa shughuli za kilimo.

Mhe. Senyamule amewataka wananchi wanaoishi katika maeneo ya mabonde na maeneo mengine yanayoweza kuathiriwa na maji kuchukua tahadhari mapema na kuhamia maeneo salama yatakayotengwa na Serikali pindi hali inapohitaji.

“Ni afadhali kuhama mapema kabla mvua hazijaanza kama unakaa bondeni kwani ni njia ya maji. Natoa wito kwa wananchi wote kuanza kuchukua tahadhari,” amesema Mhe. Senyamule.

Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari bila kusimamisha shughuli za uzalishaji, ikiwemo kilimo, akisisitiza umuhimu wa kutumia mvua hizo kama fursa ya kuongeza uzalishaji wa chakula, huku wakifuata maelekezo ya wataalamu.

WAZAZI WAONYWA KUWA MAKINI NA USALAMA WA WATOTO

Mhe. Senyamule amewataka wazazi na walezi kuwa karibu zaidi na watoto wakati wa kipindi cha mvua, akisisitiza kuwa maji ya mvua hayapaswi kujaribiwa kwa kuvuka maeneo yenye maji yanayotiririka kutokana na hatari zinazoweza kujitokeza.

“Maji huwa hayajaribiwi. Ukiona maji sehemu usiseme ngoja nijaribu kupita hapa. Tuchukue tahadhari kubwa, na nitoe wito kwa wazazi tuwalinde sana watoto wetu kwa kuhakikisha tupo nao karibu wakati wote ili wasipate madhara,” amesema.

Amesema Serikali imechukua hatua za maandalizi kwa kuhakikisha mitihani ya wanafunzi inafanyika mapema ili wanafunzi wawe majumbani kabla ya mvua kuanza, hivyo jukumu la wazazi na walezi ni kuhakikisha watoto wanakuwa salama wakati wote.

Aidha, ameelekeza wananchi watakaokumbwa na changamoto kutokana na mvua kuchukua hatua za haraka na kuhamia katika maeneo salama yaliyotengwa na Serikali, ikiwemo kutumia majengo ya shule kama maeneo ya hifadhi inapobidi.

MIUNDOMBINU YA MINADA KUIMARISHWA

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wliaya ya Kondoa, ndugu Shabani Milao, alieleza kuwa Halmashauri imetenga fedha kwa ajili ya kuimarisha miundombinu katika maeneo ya minada, ikiwemo ujenzi wa vyoo na miundombinu ya maji, hatua inayolenga kuboresha mazingira na huduma kwa wananchi wanaotumia maeneo hayo.

KONDOA YAENDELEA NA MAANDALIZI YA MVUA

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Mhe. Fatma Almas Nyangasa, amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa ziara hiyo, akisema imetoa fursa ya kukagua miradi ya maendeleo, kusikiliza changamoto za wananchi na kuchukua hatua za kuzitatua.

Mhe. Nyangasa amesema Serikali imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu tahadhari dhidi ya mvua zinazotarajiwa, ambapo viongozi wamekuwa wakifika katika kata, vijiji na mitaa mbalimbali kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi na kuhamasisha maandalizi.

“Maandalizi kuelekea mvua za El Nino tumekuwa tukipita kata kwa kata, vijiji na mitaa yote ya Kondoa kuwaelimisha wananchi na kuchukua tahadhari,” amesema.

Ziara ya Mhe. Senyamule imeendelea kuweka msisitizo katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inakamilishwa na kuleta matokeo kwa wananchi, kero zinapatiwa ufumbuzi na wananchi wanakuwa salama, huku wakitumia fursa zinazotokana na mvua kwa ajili ya kuendeleza uzalishaji wa kilimo na kuimarisha ustawi wa familia na jamii.
Posted by MROKI On Wednesday, October 07, 2026 No comments

October 06, 2026

Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, akizungumza na wabunge wanawake katika Jukwaa la Wanawake wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Oktoba 5, 2026, katika ukumbi wa AICC, jijini Arusha.
Na Mwandishi Wetu - MAELEZO, ARUSHA, 
Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson, amezitaka nchi wanachama kuhakikisha usawa wa kijinsia hauishii katika kuongeza idadi ya wanawake, bali uwape ushawishi na madaraka katika ngazi za maamuzi.

Akizungumza katika Mkutano wa 153 wa IPU - Jukwaa la Wanawake katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), Dkt. Tulia amesema katika kipindi chake cha uongozi IPU imefanya marekebisho ya Katiba na Kanuni zake kwa lengo la kuimarisha usawa wa kijinsia katika ngazi mbalimbali.

Amesema IPU pia imepitisha kwa mara ya kwanza Sera ya Kupinga Unyanyasaji katika Mikutano na Matukio, inayokataza aina zote za unyanyasaji, ikiwemo wa kingono, pamoja na kuweka mifumo ya kuripoti na kushughulikia vitendo hivyo.

Dkt. Tulia amesisitiza kuwa wanawake wanapaswa kuwa na nafasi ya kushiriki kikamilifu katika kufanya maamuzi, akisema, “Tunapaswa kuhakikisha kwamba usawa wa kijinsia unaenda sambamba na uwakilishi, ushiriki na fursa sawa za uongozi na kufanya maamuzi,” amesema Dkt. Tulia.

Aidha, amewataka washiriki wa mkutano huo kurejea katika nchi zao na kupeleka maazimio, mipango ya utekelezaji na mikakati ya usawa katika mabunge yao, huku wanaume wakishirikishwa kama wadau muhimu katika kufanikisha usawa huo.

Amesisitiza pia umuhimu wa kuwapa nafasi wanawake vijana, wanawake kutoka jamii zilizotengwa na wanawake wenye ulemavu kushiriki katika uongozi na kufanya maamuzi.




Posted by MROKI On Tuesday, October 06, 2026 No comments

October 04, 2026

Na Mwandishi Wetu 
WANANCHI wa Kitongoji cha Saburi, Kata ya Makuyuni, wametoa taarifa ya dharura kuomba ulinzi na uingiliaji kati wa haraka kutoka kwa viongozi wao wa serikali dhidi ya vitendo vya kinyama na uvunjifu wa amani vinavyofanywa na mwekezaji Akram Aziz.

Wamesema mwekezaji huyo leo amefika kwenye kitongoji chao akiwa na tingatinga kubwa (bulldozer) kwa lengo la kubomoa nyumba zote zaidi ya 600, pamoja na kuharibu misikiti, kanisa, shule, na zahanati.

 Kwa mujibu wa wananchi hao wameeleza kwamba kitendo hicho kimesababisha taharuki kubwa, simanzi, na kuzuka kwa vurugu kati ya vibaraka wake na wananchi wenye hasira waliokuwa wakitetea haki na mali zao za maisha yote, jambo ambalo lililazimu upande wa mwekezaji kukimbia ili kunusuru maisha yao kutokana na ghadhabu za wananchi.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Oktoba 3,2026 na wananchi wa kitongoji hicho kuhusu kinachoendelea katika kijiji hicho wamesema wameishi katika Kitongoji cha Saburi kwa zaidi ya miaka 30. 

Wamesema kuwa eneo hilo walipewa kihalali na mwekezaji aliyetangulia, na baadaye Halmashauri ilipima na kuweka alama (beacons) kutenga eneo hilo kutoka katika  Shamba la mwekezaji na wananchi hao pia waliuza  vipande vya maeneo ilikupata pesa kwaajili ya kujenga makazi na kujiendeleza katika eneo lao. 

“Kwa sasa eneo hili limetambuliwa na kusajiliwa rasmi na TAMISEMI kama Kitongoji kinachojitegemea, chenye miundombinu kamili ikiwemo shule,Zahanati, Miskiti na Kanisa, Miundombinu ya Umeme wa REA na Visima vya Maji.Pia kuna makazi ya wananchi zaidi ya 600

Wakieleza zaidi wamesema mwaka 2025 halmashauri ilimuandikia barua rasmi mwekezaji huyo ikimtaka aachie ekari 400 ili kupisha makazi ya wananchi hawa waliowekeza maisha yao hapo zaidi ya miaka 30. 

Hata hivyo, mwekezaji huyo amegoma kabisa kutii agizo hilo, akionyesha wazi kiburi cha kupambana na maamuzi ya Serikali za Mitaa.

Kuhusu tukio la mwekezaji kwenda na tingatinga wananchi hao wamesema hali hiyo inaweza kuhatarisha amani ya eneo lao wakati wowote.”Tunaiomba Serikali kupitia ofisi za Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa kuchukua hatua za dharura ikiwemo kumzuia mara moja Akram Aziz kufanya jaribio lolote la kubomoa makazi na taasisi za kijamii katika Kitongoji cha Saburi.

 Hatua nyingine ni kufanya uchunguzi wa dharura kuhusu hati anazozitumia kujitwalia ardhi ya wananchi waliokaa kihalali kwa zaidi ya miongo mitatu pamoja na kulinda usalama wa maisha na mali zao kwa kupeleka vyombo vya ulinzi kuzuia mwekezaji huyu kujichukulia sheria mkononi.

“Haiwezekani wananchi wa Kitongoji cha Saburi tuwe wakimbizi ndani ya nchi yetu wenyewe baada ya kuishi kwa zaidi ya miaka 30. Tunaomba msaada wa haraka, “wamesema wananchi wa Kitongoji cha Saburi, Makuyuni.






 

Posted by MROKI On Sunday, October 04, 2026 No comments

October 03, 2026




WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameagiza kupatiwa taarifa za uchunguzi kuhusu majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Bunda yaliyotitia, akitaka hatua zichukuliwe dhidi ya waliohusika iwapo itathibitika kuwa kulikuwa na uzembe.

Dkt. Mwigulu ametoa agizo hilo leo, Jumamosi, Oktoba 3, 2026, wakati akizungumza na wananchi katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika Nyamuswa, Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, baada ya kukagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Bunda.

“Nimeambiwa Waziri wa Afya alishatengeneza timu na ikafanya kazi na TAKUKURU ameshafanyia kazi. Nizipate hizo taarifa ili hawa waliofanya makosa haya wawajibike kule kule walipo. Lazima wawajibike. Hii kuharibu wilaya hii na kuhamishiwa ukaharibu na wilaya nyingine, hii haikubaliki,” amesema.

Amesema wakati wa ukaguzi huo amekuta majengo mawili yakiwa yametitia na kupewa maelezo kuwa hali hiyo imesababishwa na uwepo wa maji katika eneo la mradi pamoja na udongo wa mfinyanzi.

“Namuuliza kwa nini majengo yametitia? Wanasema kwa sababu yamejengwa karibu na chanzo cha maji. Chanzo cha maji kile kimekuja baada ya kujenga msingi? Si kilikuwepo pale pale? ... Wanasema udongo huu ni wa mfinyanzi,” amesema.

Dkt. Mwigulu amesema Serikali itaendelea kufuatilia suala hilo ili kubaini ukweli wa kilichosababisha majengo hayo kutitia na kuhakikisha wananchi hawapati adhabu kutokana na uzembe katika utekelezaji wa miradi ya Serikali.

Amesema Serikali pia inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha maeneo yaliyobaki ya ujenzi wa hospitali hiyo ili wananchi waendelee kupata huduma za afya katika eneo lao.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na kupanda kwa bei ya saruji, ikiwemo kuelekeza kuondolewa kwa kodi kwenye klinka, malighafi inayotumika katika uzalishaji wa saruji.

“Nimewaelekeza Mamlaka ya Mapato waondoe kodi kwenye klinka, malighafi inayotumika kwenye uzalishaji wa saruji ili upatikanaji wa saruji uwe wa uhakika na bei iweze kuwa bei himilivu,” amesema.

Amesema Serikali inalenga kuhakikisha upatikanaji wa saruji unaendelea kuwa wa uhakika na bei yake inakuwa himilivu kwa wananchi, akibainisha kuwa katika baadhi ya maeneo bei imekuwa ikipanda hadi kufikia zaidi ya Sh. 25,000, Sh. 27,000 na katika baadhi ya mikoa kufikia Sh. 32,000 kwa mfuko.

Kuhusu huduma za afya, Dkt. Mwigulu amesisitiza kuwa wananchi hawapaswi kuchangishwa fedha za mafuta kwa ajili ya magari ya Serikali, hususan magari ya wagonjwa yanayotumika kuokoa maisha.

“Hatuwezi tukawa na magari ya Serikali yana mafuta, halafu ambulance ya kunusuru maisha ya wagonjwa tuchangishane mafuta. Haya ni mambo ya mazoea ambayo hatutaki kuwa utaratibu wa Serikali,” amesema.

Amesema mwananchi yeyote atakayeombwa fedha za mafuta kwa ajili ya gari la wagonjwa anatakiwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili hatua zichukuliwe.

Dkt. Mwigulu pia amesisitiza umuhimu wa wagonjwa walio katika hali mbaya kupewa huduma ya dharura mara moja kabla ya kukamilisha taratibu nyingine za kiutawala.

“Mgonjwa aliyezidiwa amefika, hatua ya kwanza apelekwe moja kwa moja kwenye kitanda apate huduma. Hata kumwandikisha mtamwandikisha akiwa ameshapata huduma ya kwanza. Kanusuru kwanza maisha yake. Usifanye itifaki kwenye maisha,” amesema.

Kuhusu upatikanaji wa dawa, amesema Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba, hivyo amewataka viongozi na watendaji wa afya kuhakikisha dawa zinawafikia wananchi waliokusudiwa na matumizi yake yanafuatiliwa ipasavyo.

Hospitali ya Wilaya ya Bunda ilianza kutekelezwa tarehe 8 Mei, 2019, ikiwa ni miongoni mwa hospitali 67 za awamu ya kwanza za halmashauri zilizolenga kusogeza huduma za afya za ngazi ya hospitali karibu na wananchi. Hadi sasa, Serikali imetoa jumla ya Sh. bilioni 5.39 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Hospitali hiyo imeanza kutoa huduma mbalimbali, ikiwemo huduma za wagonjwa wa nje, maabara, afya ya uzazi na mtoto, kujifungua, radiolojia, kulaza wagonjwa, huduma za macho, meno na huduma za dharura.
Posted by MROKI On Saturday, October 03, 2026 No comments

October 02, 2026

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akishuhudia utiaji Saini Mkataba wa Utekelezaji wa Mpango wa Ufadhili wa Kuunganisha Umeme kwa Wananchi kati ya TANESCO na CRDB, hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam, leo tarehe 02 Oktoba 2026. (kushoto ni Mkurugenzi wa CRDB Dkt. Abdulmajid Nsekela na kulia ni Mkurugenzi wa TANESCO Razaro Twange)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akiwa na Viongozi mbalimbali wakishiriki hafla ya utiaji Saini Mkataba wa Uzinduzi wa Mpango wa Ufadhili wa Uunganishaji Umeme kwa Wananchi, kati ya Benki ya CRDB na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam. Tarehe 02 Oktoba 2026.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akiwa na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Juma Homera pamoja na Viongozi mbalimbali, akizindua Mpango wa Ufadhili wa Uunganishaji Umeme kwa Wananchi, kati ya Benki ya CRDB na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), katika hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam. Tarehe 02 Oktoba 2026.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akihutubia wakati wa hafla ya utiaji Saini Mkataba wa Uzinduzi wa Mpango wa Ufadhili wa Uunganishaji Umeme kwa Wananchi, kati ya Benki ya CRDB na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam. Tarehe 02 Oktoba 2026.
Viongozi, wadau na wananchi mbalimbali wakishiriki katika hafla ya utiaji Saini Mkataba wa Uzinduzi wa Mpango wa Ufadhili wa Uunganishaji Umeme kwa Wananchi, kati ya Benki ya CRDB na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi. Tarehe 02 Oktoba 2026.
Viongozi, wadau na wananchi mbalimbali wakishiriki katika hafla ya utiaji Saini Mkataba wa Uzinduzi wa Mpango wa Ufadhili wa Uunganishaji Umeme kwa Wananchi, kati ya Benki ya CRDB na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi. Tarehe 02 Oktoba 2026.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi ametoa wito kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kushirikiana na wadau husika wa sekta binafsi kuandaa mpango utakaowawezesha wananchi kununua umeme kwa mkopo kama ilivyo mikopo katika mitandao ya simu ili kuwasaidia wananchi wanapokuwa na uhitaji wa umeme lakini hawana fedha.
 
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati wa hafla ya utiaji Saini Mkataba wa Uzinduzi wa Mpango wa Ufadhili wa Uunganishaji Umeme kwa Wananchi, kati ya Benki ya CRDB na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam. Amesema hatua hiyo itaweza kusaidia wananchi kuendelea kutumia huduma ya umeme na kufanya uzalishaji mali au mahitaji ya nyumbani hata pale wanapokuwa na changamoto ya fedha ya kununua umeme huo.
 
Aidha, Makamu wa Rais ameitaka Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuendeleza mradi ulioanzishwa chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha wananchi wanaoishi mazingira yanayofanana na kijijini lakini mipaka ya kiutawala inamtambua yupo mjini wanaunganishiwa huduma ya umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 kama ya wananchi wa vijijini. Amesema yapo maeneo ambayo ni mipaka ya kiutawala inawatenganisha wananchi kati ya mijini na vijijini lakini wananchi hao maisha yao yanafanana.
 
Makamu wa Rais, amesema azma hiyo, inalenga kufikia lengo la kitaifa, malengo ya “mission 300” pamoja na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, kuhakikisha huduma ya umeme inamfikia mtanzania kwa gharama nafuu.
 
Makamu wa Rais ameipongeza TANESCO na Benki ya CRDB kwa hatua hiyo muhimu inayolenga kuimarisha na kuboresha maisha ya wananchi kwa kupata huduma ya umeme.  Amesema ushirikiano huo ni mfano bora wa namna ya Taasisi za Umma na Sekta Binafsi zinavyoweza kuwaunganisha watanzania na kuwekeza nguvu na rasilimali ili kutatua changamoto zinazowagusa wananchi moja kwa moja.
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dkt. Abdulmajid Nsekela amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono na uwepo wa Dira ya Maendeleo 2050. Amesema Serikali na Sekta binafsi kupitia ubunifu itawezesha kutekelezwa na kufanikiwa kwa Dira 2050 inayolenga kujenga uchumi mkubwa, yenye kuzalisha ajira, wenye ushindaji, unaotumia teknolojia na kuboresha maendeleo ya wananchi.
 
Amesema Benki ya CRDB imedhamiria kuwa mshirika wa maendeleo yan chi kwa kutumia uwezo wa kifedha, teknolojia iliyopo, rasilimali ya wataalamu waliopo, mtandao uliopo na ubunifu katika kusaidia kutatua changamoto ya maendeleo ya Taifa.
 
Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Razaro Twange amesema upatikaji wa umeme umeendelea kuongezeka nchini na ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme na kusambaza umeme ikiendelea kujengwa. Amesema Tanzania inafikia megawati 4500-4600 hivi sasa huku kukiwa na mtandao wa kiliometa 9000 za kusafirisha umeme, na mtandao wa zaidi ya kilometa 220,000 wa njia za kusambaza umeme.
 
Utiaji wa Saini wa Mpango wa Ufadhili wa Uunganishaji Umeme kwa Wananchi, kati ya Benki ya CRDB na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), utawezesha wananchi wa maeneo ya vijiji kuunganishwa bure huduma ya umeme kutokana na ruzuku kutoka Benki ya CRDB, na kwa wananchi maeneo ya mijini watapewa huduma hiyo kwa mkopo wa riba nafuu ambao wataweza kuunganishwa umeme na kufanya shughuli za uzalishaji mali.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi akiwa Viongozi mbalimbali katika picha ya pamoja na Viongozi wa mitaa na vijiji mara baada ya hafla ya utiaji Saini Mkataba wa Uzinduzi wa Mpango wa Ufadhili wa Uunganishaji Umeme kwa Wananchi, kati ya Benki ya CRDB na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam. Tarehe 02 Oktoba 2026.

Posted by MROKI On Friday, October 02, 2026 No comments
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza na Wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mwibara, eneo la Kibara, mkoani Mara leo tarehe Oktoba, 2026. 
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akisalimiana na baadhi ya Viongozi wakati akiwasili katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mwibara, eneo la Kibara, mkoani Mara leo tarehe Oktoba, 2026.  
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuwawezesha Watanzania kujiletea maendeleo, ikiwemo kurekebisha sheria mbalimbali zinazowakwaza katika kutekeleza shughuli zao.

Ameyasema hayo leo, Ijumaa, Oktoba 2, 2026, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mwibara, eneo la Kibara, mkoani Mara.

Amesema baadhi ya mambo yamefanyika ndani ya siku 100 kama alivyoahidi Rais, huku mengine yakiendelea kuchukuliwa hatua.

“Leo tunavyoongea, tumerekebisha sheria mbalimbali ili tuweze kuhakikisha kuwa Watanzania hawakwazwi na baadhi ya sheria katika kutekeleza wajibu wao,” amesema.

Amesema miongoni mwa hatua hizo ni kuwapa wafanyabiashara wapya muda wa kuimarisha biashara zao, ambapo kodi ya mapato kwa biashara mpya inaanza baada ya mwaka mmoja tangu kupata TIN kwa ajili ya kuanza biashara.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekemea tabia ya baadhi ya watumishi kuwachangisha wananchi fedha kwa ajili ya mafuta ya magari ya wagonjwa (ambulance), akisema vitendo hivyo havikubaliki.

“Hatuwezi tukawa na magari ya Serikali yana mafuta, halafu ambulance ya kunusuru maisha ya wagonjwa tuchangishane mafuta. Haya ni mazoea mabaya ambayo hatutaki kuwa utaratibu wa Serikali. Wa aina hiyo akipatikana, tunachukua hatua kali,” amesema.

Aidha, amekemea tabia ya kuficha dawa zilizotolewa na Serikali huku wagonjwa wakielekezwa kununua dawa nje ya vituo vya afya, na kuwaagiza viongozi wa afya kufuatilia hali hiyo hatua kwa hatua ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma zinazostahili.

Katika sekta ya nishati, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kusogeza huduma ya umeme kwenye vitongoji, mitaa na maeneo mapya ya makazi, akisisitiza kuwa wananchi katika maeneo hayo wanapaswa kunufaika na huduma hiyo.

Kuhusu mvua, amewataka viongozi na mamlaka zinazohusika kujiandaa kukabiliana na uwezekano wa mvua kubwa, ikiwemo kusafisha mifereji na maeneo ya kupitisha maji ili kupunguza athari za mafuriko.

Aidha, amewataka wananchi kutotumia nguvu au kuchukua sheria mkononi katika kushughulikia migogoro ya ardhi na mifugo, akisema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kutatua changamoto za maeneo ya malisho na upatikanaji wa maji kwa mifugo.

Waziri Mkuu pia amewataka Watanzania kuendelea kulinda amani ya nchi na mali za umma, akisisitiza kuwa shule, barabara na vituo vya afya ni mali za wananchi na uharibifu wake unawaathiri wao wenyewe.
Posted by MROKI On Friday, October 02, 2026 No comments






📍GEITA. 
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Dkt. Deogratias Sangu, ameitaka Tume ya Madini kuimarisha mikakati ya kuitangaza tanzanite katika masoko ya kimataifa, akisema madini hayo ni miongoni mwa alama muhimu zinazoitambulisha Tanzania duniani.

Dkt. Sangu ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea banda la Tume ya Madini katika Maonesho ya Kitaifa ya Tisa ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bomba Mbili mkoani Geita.

Amesema tanzanite ina umuhimu wa kipekee kwa Tanzania kwa kuwa hupatikana katika eneo la Mirerani, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, eneo linalotajwa kuwa chanzo pekee kinachojulikana duniani cha madini hayo.

Aidha, Dkt. Sangu ameipongeza Tume ya Madini kwa usimamizi wa Sekta ya Madini, akisema juhudi hizo zimechangia mafanikio mbalimbali, ikiwemo kuongezeka kwa ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali, kuimarika kwa ushiriki wa Watanzania na wawekezaji kutoka nje katika sekta hiyo, pamoja na kupungua kwa vitendo vya utoroshaji wa madini.

Maonesho hayo ya kitaifa yanaendelea kwa lengo la kutoa fursa kwa wadau kujifunza kuhusu teknolojia, uwekezaji, uzalishaji, uongezaji thamani na biashara ya madini, na yanatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 3, 2026.
Posted by MROKI On Friday, October 02, 2026 No comments








📍GEITA
Serikali kupitia Tume ya Madini inatarajia kuanza kuhakiki umiliki halali wa kampuni zinazotoa huduma kwenye migodi ya madini nchini, ili kuhakikisha fursa za ajira, huduma na biashara zinawanufaisha Watanzania wenye sifa na uwezo unaohitajika.

Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema hatua hiyo inalenga kudhibiti utaratibu unaodaiwa kuwepo wa kampuni za kigeni kuingia ubia na Watanzania wasio na sifa stahiki kwa ajili ya kutimiza matakwa ya ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini.

Waziri Mavunde ametoa kauli hiyo mapema leo Oktoba 2, 2026, wakati akifungua Siku ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, ikiwa ni sehemu ya Maonesho ya Kitaifa ya Tisa ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bomba Mbili, Geita.

Amesema katika utekelezaji wa Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, imebainika kuwepo kwa kampuni za kigeni zinazoingia ubia na Watanzania kwa lengo la kutimiza matakwa ya umiliki wa hisa, wakati kiuhalisia kampuni hizo zinamilikiwa na wageni.

“Nimebaini kumekuwepo na kampuni za kigeni ambazo zimekuwa zikiingia ubia na Watanzania ambao wanatakiwa kuwa na asilimia 20 ya hisa kimaandishi, lakini ukija kiuhalisia unabaini kampuni inamilikiwa na wageni pekee,” amesema.

Amesema Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini, kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali ikiwemo BRELA na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), itahakiki umiliki wa kampuni hizo pamoja na miamala inayofanyika ili kubaini umiliki halali wa kampuni husika.

Waziri Mavunde pia amewataka Watanzania kujiandaa kuchangamkia fursa za kutoa huduma na bidhaa kwenye migodi, akisema kampuni 14 zinatarajiwa kuanza shughuli za uchimbaji wa madini, huku leseni nyingine 28 zikiwa katika hatua za kutolewa.

Amesema ongezeko hilo linatarajiwa kuongeza mahitaji ya huduma na bidhaa mbalimbali migodini, hivyo kuwataka watoa huduma wa ndani kujiandaa na, pale inapowezekana, kuungana ili kuwa na uwezo wa kukidhi mahitaji makubwa ya kampuni za uchimbaji.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde amesema Serikali imeanza kutekeleza mkakati wa kutumia asilimia 10 ya makusanyo ya maduhuli yatokanayo na Sekta ya Madini kwa ajili ya shughuli za utafiti wa madini.

Amesema katika kipindi cha miezi mitatu ya mwaka wa fedha 2026/2027, kuanzia Julai hadi Septemba, Wizara kupitia Tume ya Madini ilikusanya shilingi bilioni 411, sawa na asilimia 117 ya lengo la shilingi bilioni 351.

“Katika makusanyo hayo, kiasi cha shilingi bilioni 40, sawa na asilimia 10, kitaanza kutumika katika shughuli za utafiti wa madini,” amesema.

Ameongeza kuwa Serikali pia imetenga eneo lililokuwa likitumika na Mgodi wa Buzwagi kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vitakavyozalisha bidhaa zinazohitajika katika shughuli za migodini, hatua inayolenga kuongeza ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa thamani wa Sekta ya Madini.

Aidha, amesema Serikali inalenga kuhakikisha asilimia 90 ya manunuzi ya kampuni za madini, yenye thamani ya takribani shilingi trilioni 5.1 kwa mwaka, yanafanywa na Watanzania ili kuongeza mchango wa Sekta ya Madini katika kukuza uchumi wa nchi.

Waziri Mavunde pia amewapongeza wachimbaji wadogo kwa mchango wao unaofikia asilimia 40 katika Sekta ya Madini, akisema katika mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali ilikusanya shilingi trilioni 1.393 kutokana na shughuli za sekta hiyo.

Amesema utekelezaji wa Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini umeendelea kuleta matokeo, ikiwemo kuongezeka kwa ajira rasmi 19,000, huku raia wa kigeni wakichangia asilimia nne ya ajira katika sekta hiyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Alexander Mnyeti, amewataka Watanzania kuacha kulalamika kuhusu fursa zilizopo na badala yake kuwa wabunifu na kuzichangamkia ili kuongeza ushiriki wao katika Sekta ya Madini.


Mbunge wa Geita, Chacha Wambura, ameiomba Wizara ya Madini kuendelea kusimamia kwa nguvu utekelezaji wa Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini, huku ikiendelea kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo nchini.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), John Bina, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo, pamoja na kufanya maboresho ya Sheria na Kanuni za Madini.

Awali, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo, amesema mkutano huo uliowakutanisha wamiliki wa leseni za madini na watoa huduma kwenye migodi unalenga kubadilishana uzoefu, kutoa elimu, kuweka mikakati ya ushirikiano na kubuni njia bora za kutatua changamoto zinazowakabili wadau wa Sekta ya Madini.
Posted by MROKI On Friday, October 02, 2026 No comments
  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo