Nafasi Ya Matangazo

October 03, 2026




WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameagiza kupatiwa taarifa za uchunguzi kuhusu majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Bunda yaliyotitia, akitaka hatua zichukuliwe dhidi ya waliohusika iwapo itathibitika kuwa kulikuwa na uzembe.

Dkt. Mwigulu ametoa agizo hilo leo, Jumamosi, Oktoba 3, 2026, wakati akizungumza na wananchi katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika Nyamuswa, Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, baada ya kukagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Bunda.

“Nimeambiwa Waziri wa Afya alishatengeneza timu na ikafanya kazi na TAKUKURU ameshafanyia kazi. Nizipate hizo taarifa ili hawa waliofanya makosa haya wawajibike kule kule walipo. Lazima wawajibike. Hii kuharibu wilaya hii na kuhamishiwa ukaharibu na wilaya nyingine, hii haikubaliki,” amesema.

Amesema wakati wa ukaguzi huo amekuta majengo mawili yakiwa yametitia na kupewa maelezo kuwa hali hiyo imesababishwa na uwepo wa maji katika eneo la mradi pamoja na udongo wa mfinyanzi.

“Namuuliza kwa nini majengo yametitia? Wanasema kwa sababu yamejengwa karibu na chanzo cha maji. Chanzo cha maji kile kimekuja baada ya kujenga msingi? Si kilikuwepo pale pale? ... Wanasema udongo huu ni wa mfinyanzi,” amesema.

Dkt. Mwigulu amesema Serikali itaendelea kufuatilia suala hilo ili kubaini ukweli wa kilichosababisha majengo hayo kutitia na kuhakikisha wananchi hawapati adhabu kutokana na uzembe katika utekelezaji wa miradi ya Serikali.

Amesema Serikali pia inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha maeneo yaliyobaki ya ujenzi wa hospitali hiyo ili wananchi waendelee kupata huduma za afya katika eneo lao.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na kupanda kwa bei ya saruji, ikiwemo kuelekeza kuondolewa kwa kodi kwenye klinka, malighafi inayotumika katika uzalishaji wa saruji.

“Nimewaelekeza Mamlaka ya Mapato waondoe kodi kwenye klinka, malighafi inayotumika kwenye uzalishaji wa saruji ili upatikanaji wa saruji uwe wa uhakika na bei iweze kuwa bei himilivu,” amesema.

Amesema Serikali inalenga kuhakikisha upatikanaji wa saruji unaendelea kuwa wa uhakika na bei yake inakuwa himilivu kwa wananchi, akibainisha kuwa katika baadhi ya maeneo bei imekuwa ikipanda hadi kufikia zaidi ya Sh. 25,000, Sh. 27,000 na katika baadhi ya mikoa kufikia Sh. 32,000 kwa mfuko.

Kuhusu huduma za afya, Dkt. Mwigulu amesisitiza kuwa wananchi hawapaswi kuchangishwa fedha za mafuta kwa ajili ya magari ya Serikali, hususan magari ya wagonjwa yanayotumika kuokoa maisha.

“Hatuwezi tukawa na magari ya Serikali yana mafuta, halafu ambulance ya kunusuru maisha ya wagonjwa tuchangishane mafuta. Haya ni mambo ya mazoea ambayo hatutaki kuwa utaratibu wa Serikali,” amesema.

Amesema mwananchi yeyote atakayeombwa fedha za mafuta kwa ajili ya gari la wagonjwa anatakiwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili hatua zichukuliwe.

Dkt. Mwigulu pia amesisitiza umuhimu wa wagonjwa walio katika hali mbaya kupewa huduma ya dharura mara moja kabla ya kukamilisha taratibu nyingine za kiutawala.

“Mgonjwa aliyezidiwa amefika, hatua ya kwanza apelekwe moja kwa moja kwenye kitanda apate huduma. Hata kumwandikisha mtamwandikisha akiwa ameshapata huduma ya kwanza. Kanusuru kwanza maisha yake. Usifanye itifaki kwenye maisha,” amesema.

Kuhusu upatikanaji wa dawa, amesema Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba, hivyo amewataka viongozi na watendaji wa afya kuhakikisha dawa zinawafikia wananchi waliokusudiwa na matumizi yake yanafuatiliwa ipasavyo.

Hospitali ya Wilaya ya Bunda ilianza kutekelezwa tarehe 8 Mei, 2019, ikiwa ni miongoni mwa hospitali 67 za awamu ya kwanza za halmashauri zilizolenga kusogeza huduma za afya za ngazi ya hospitali karibu na wananchi. Hadi sasa, Serikali imetoa jumla ya Sh. bilioni 5.39 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Hospitali hiyo imeanza kutoa huduma mbalimbali, ikiwemo huduma za wagonjwa wa nje, maabara, afya ya uzazi na mtoto, kujifungua, radiolojia, kulaza wagonjwa, huduma za macho, meno na huduma za dharura.
Posted by MROKI On Saturday, October 03, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo