Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amefanya ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa na Halmashauri ya Mji wa Kondoa, ambapo amekagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kusikiliza na kutatua kero za wananchi, huku akitoa wito wa maandalizi dhidi ya mvua kubwa zinazotarajiwa na kusisitiza wananchi kuendelea na shughuli za kilimo kwa kuzingatia tahadhari.
Ziara hiyo iliyofanyika Oktoba 06, 2026, imehusisha maeneo mbalimbali ya Kondoa, ikiwemo Kata ya Itaswi na Pahi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa pamoja na Kata ya Serya katika Halmashauri ya Mji wa Kondoa, ambapo Mkuu huyo wa Mkoa amekagua miradi ya elimu, maji na miundombinu, pamoja na kufanya mikutano ya hadhara na kusikiliza changamoto za wananchi.
AGIZO LA KUKAMILISHA BWAWA LA ITASWI
Akiwa Kata ya Itaswi, Mhe. Senyamule alikagua ujenzi wa Bwawa la Itaswi, mradi wenye thamani ya shilingi bilioni 5.7, unaolenga kuongeza upatikanaji wa maji na kupunguza changamoto ya maji kwa wananchi wa eneo hilo.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa TARURA Wilaya ya Kondoa, Ndugu Majid Mtili, alisema ujenzi wa bwawa hilo umekuwa ukienda kwa kasi ndogo kutokana na mkandarasi kupokea fedha za utekelezaji kwa awamu tofauti.
Mhe. Senyamule amesisitiza umuhimu wa mradi huo kukamilishwa ili wananchi wa Itaswi waanze kunufaika na uwekezaji huo, hususan katika kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji.
SHULE MPYA KUFUNGUA FURSA ZA ELIMU KONDOA
Katika Kijiji cha Potea, Kata ya Pahi, Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Mkuu wa Mkoa alitembelea na kukagua ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Potea, inayotarajiwa kukamilika mwishoni mwa Novemba 2026.
Mradi huo utakapokamilika utakuwa umegharimu shilingi milioni 540, na shule hiyo inatarajiwa kuanza kupokea wanafunzi Januari 2027, hatua inayolenga kuongeza fursa za elimu kwa watoto wa eneo hilo na maeneo jirani.
Aidha, katika Halmashauri ya Mji wa Kondoa, Kata ya Serya, Mhe. Senyamule aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa Shule mpya ya Msingi Serya, mradi ambao hadi kukamilika kwake utagharimu shilingi milioni 302.
Shule hiyo pia inatarajiwa kuanza kupokea wanafunzi Januari 2027, ikienda sambamba na juhudi za Serikali za kuongeza miundombinu ya elimu na kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kujifunzia karibu na maeneo wanayoishi.
ITASWI: SERIKALI YAENDELEA KUWEKEZA KATIKA HUDUMA ZA JAMII
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Itaswi, Mhe. Senyamule alieleza kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika huduma za kijamii na kuboresha maisha ya wananchi.
Alitaja miongoni mwa miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Haire wenye thamani ya shilingi milioni 98, ujenzi wa Shule ya Msingi Chubi wenye thamani ya shilingi milioni 100, pamoja na utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vitatu yenye jumla ya shilingi milioni 24.5.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema uwekezaji huo unaakisi azma ya Serikali ya kuhakikisha rasilimali zinaelekezwa katika maeneo yenye mahitaji muhimu kwa wananchi na kwamba miradi inapokamilika inatoa huduma na matokeo yanayokusudiwa.
RC SENYAMULE: “TAHADHARI YA MVUA ISIWE SABABU YA KUACHA KULIMA”
Katika ziara hiyo, Mhe. Senyamule pia alitoa msisitizo kuhusu tahadhari dhidi ya mvua kubwa zinazotarajiwa, akiwataka wananchi kuzingatia utabiri na ushauri unaotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Hata hivyo, amesisitiza kuwa tahadhari dhidi ya uwezekano wa mvua kubwa isiwe sababu ya wananchi kuacha shughuli za kilimo, bali watumie fursa ya mvua kwa kuendelea kulima huku wakizingatia ushauri wa wataalamu kuhusu maeneo salama na muda unaofaa kwa shughuli za kilimo.
Mhe. Senyamule amewataka wananchi wanaoishi katika maeneo ya mabonde na maeneo mengine yanayoweza kuathiriwa na maji kuchukua tahadhari mapema na kuhamia maeneo salama yatakayotengwa na Serikali pindi hali inapohitaji.
“Ni afadhali kuhama mapema kabla mvua hazijaanza kama unakaa bondeni kwani ni njia ya maji. Natoa wito kwa wananchi wote kuanza kuchukua tahadhari,” amesema Mhe. Senyamule.
Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari bila kusimamisha shughuli za uzalishaji, ikiwemo kilimo, akisisitiza umuhimu wa kutumia mvua hizo kama fursa ya kuongeza uzalishaji wa chakula, huku wakifuata maelekezo ya wataalamu.
WAZAZI WAONYWA KUWA MAKINI NA USALAMA WA WATOTO
Mhe. Senyamule amewataka wazazi na walezi kuwa karibu zaidi na watoto wakati wa kipindi cha mvua, akisisitiza kuwa maji ya mvua hayapaswi kujaribiwa kwa kuvuka maeneo yenye maji yanayotiririka kutokana na hatari zinazoweza kujitokeza.
“Maji huwa hayajaribiwi. Ukiona maji sehemu usiseme ngoja nijaribu kupita hapa. Tuchukue tahadhari kubwa, na nitoe wito kwa wazazi tuwalinde sana watoto wetu kwa kuhakikisha tupo nao karibu wakati wote ili wasipate madhara,” amesema.
Amesema Serikali imechukua hatua za maandalizi kwa kuhakikisha mitihani ya wanafunzi inafanyika mapema ili wanafunzi wawe majumbani kabla ya mvua kuanza, hivyo jukumu la wazazi na walezi ni kuhakikisha watoto wanakuwa salama wakati wote.
Aidha, ameelekeza wananchi watakaokumbwa na changamoto kutokana na mvua kuchukua hatua za haraka na kuhamia katika maeneo salama yaliyotengwa na Serikali, ikiwemo kutumia majengo ya shule kama maeneo ya hifadhi inapobidi.
MIUNDOMBINU YA MINADA KUIMARISHWA
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wliaya ya Kondoa, ndugu Shabani Milao, alieleza kuwa Halmashauri imetenga fedha kwa ajili ya kuimarisha miundombinu katika maeneo ya minada, ikiwemo ujenzi wa vyoo na miundombinu ya maji, hatua inayolenga kuboresha mazingira na huduma kwa wananchi wanaotumia maeneo hayo.
KONDOA YAENDELEA NA MAANDALIZI YA MVUA
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Mhe. Fatma Almas Nyangasa, amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa ziara hiyo, akisema imetoa fursa ya kukagua miradi ya maendeleo, kusikiliza changamoto za wananchi na kuchukua hatua za kuzitatua.
Mhe. Nyangasa amesema Serikali imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu tahadhari dhidi ya mvua zinazotarajiwa, ambapo viongozi wamekuwa wakifika katika kata, vijiji na mitaa mbalimbali kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi na kuhamasisha maandalizi.
“Maandalizi kuelekea mvua za El Nino tumekuwa tukipita kata kwa kata, vijiji na mitaa yote ya Kondoa kuwaelimisha wananchi na kuchukua tahadhari,” amesema.
Ziara ya Mhe. Senyamule imeendelea kuweka msisitizo katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inakamilishwa na kuleta matokeo kwa wananchi, kero zinapatiwa ufumbuzi na wananchi wanakuwa salama, huku wakitumia fursa zinazotokana na mvua kwa ajili ya kuendeleza uzalishaji wa kilimo na kuimarisha ustawi wa familia na jamii.















0 comments:
Post a Comment