Na Mwandishi Wetu, Geita
SERIKALI imewahimiza wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika viwanda vya uchenjuaji na uchakataji wa madini ya dhahabu mkoani Geita ili kuongeza thamani ya madini, kuimarisha ajira, kulinda mazingira na kukuza mapato ya Taifa.
SERIKALI imewahimiza wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika viwanda vya uchenjuaji na uchakataji wa madini ya dhahabu mkoani Geita ili kuongeza thamani ya madini, kuimarisha ajira, kulinda mazingira na kukuza mapato ya Taifa.
Wito huo umetolewa na Mjiolojia kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita, John Maganga, wakati wa ziara ya kutembelea masoko ya madini mkoani humo, ambapo amesema Geita ina fursa kubwa ya uwekezaji kutokana na uzalishaji mkubwa wa dhahabu unaofanywa na wachimbaji wadogo na wa kati.
Amesema licha ya uzalishaji huo, bado kuna upungufu wa viwanda vya uchenjuaji na uchakataji wa dhahabu, hali inayosababisha madini mengi kuuzwa yakiwa ghafi bila kuongeza thamani, jambo linalonyima wananchi na Serikali mapato makubwa.
“Ni wakati sasa kwa wawekezaji kuchangamkia fursa zilizopo Geita kwa kujenga viwanda vya uchenjuaji na uchakataji wa dhahabu, hatua itakayopunguza matumizi ya zebaki, kulinda afya za wananchi na mazingira, pamoja na kuongeza mapato ya Serikali,” amesema.
Ameeleza kuwa uanzishwaji wa viwanda hivyo utaenda sambamba na uwepo wa masoko rasmi ya madini, ambayo yameimarisha uwazi, usalama na ufanisi katika biashara ya dhahabu, na kudhibiti vitendo vya magendo vilivyokuwa vikisababisha upotevu wa mapato ya Serikali.
Ameongeza kuwa masoko ya dhahabu yamekuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Geita kwa kuongeza ajira, biashara na mzunguko wa fedha, huku wachimbaji wakinufaika kwa kuuza madini yao kwa bei ya soko na kwa mifumo rasmi ya Serikali.
Kwa upande wake, Afisa Mthaminishaji wa Madini, Peter Jamhuri, amesema mifumo ya kidigitali inayotumika katika masoko ya madini imeongeza uwazi na ufanisi kwa kuwezesha ukusanyaji wa takwimu sahihi za mauzo, jambo linalosaidia wafanyabiashara kupata mikopo kutoka taasisi za fedha.
Amesema mifumo hiyo imeimarisha uwazi na kuondoa magendo, huku akimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusimamia sera na mifumo bora inayochochea maendeleo ya sekta ya madini na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
“Kwa sasa wafanyabiashara wanapata ripoti za mauzo zinazotumika kama vielelezo muhimu katika taasisi za kifedha, hali inayochochea upanuzi wa biashara na uwekezaji zaidi,” amesema.
Naye mfanyabiashara wa dhahabu na mmiliki wa Gambo Mining Ltd, Magambo Magambo, amesema kuanzishwa kwa masoko rasmi ya madini kumeleta mapinduzi makubwa katika sekta hiyo na kusaidia kukuza wafanyabiashara wazawa.












0 comments:
Post a Comment