Ofisi ya Afisa Madini Mkazi – Mbogwe inapenda kutoa ufafanuzi kwa umma na vyombo vya habari kuhusu tukio la ajali lililotokea katika Mgodi wa Dhahabu wa Msasa (Msasa Gold Mine) uliopo katika Kijiji cha Msasa, Runzewe, Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita.
Mgodi wa Msasa unamilikiwa na Khadija Mkopi Mohamed, Amani Jackonia Mkaga, Boaz Lucas Nkise na Fadhili Victor Malema, ukiwa na jumla ya leseni 17 za uchimbaji zilizotolewa tarehe 22 Oktoba 2025.
Shughuli za uchimbaji zilianza kushika kasi mwezi Novemba 2025, na hadi sasa mgodi unakadiriwa kuwa na maduara takribani 2,000 pamoja na zaidi ya watu 20,000 wanaojihusisha na shughuli za uchimbaji na utoaji huduma mbalimbali.
Mnamo Jumapili tarehe 29 Machi 2026 majira ya saa 4:00 asubuhi, katika eneo la Area A kulitokea mpasuko wa ardhi ulioathiri maduara manne (4) yenye namba KO 46A, 47A, 48A na 49A. Maduara hayo yalikuwa yamesimamishwa uzalishaji kufuatia maelekezo ya wakaguzi wa mgodi yaliyotolewa tarehe 27 Machi 2026 ili kufanyiwa ukarabati wa kiusalama.
Mpasuko huo ulisababisha maduara hayo kutitia ardhini, hali inayohusishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini na kusababisha kulegea kwa udongo na miamba.
Ni muhimu kufahamu kuwa, wakati tukio linatokea hapakuwa na shughuli zozote za uzalishaji katika eneo husika kwani watendakazi wote walikuwa tayari wameondolewa kupisha ukarabati. Shughuli za ukaguzi katika mgodi huo hufanyika kila siku kupitia Ofisi ya Ukaguzi wa Mgodi inayoongozwa na Mkaguzi Mkuu wa Mgodi akisaidiwa na takribani wakaguzi 200 waliopo muda wote katika eneo la mgodi, chini ya usimamizi wa karibu wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi – Mbogwe, Mkaguzi Mkuu wa Migodi Tanzania pamoja na taasisi nyingine za Serikali kwa mujibu wa sheria.
Baada ya kubainika dalili za hatari, wakaguzi wa mgodi walichukua hatua za haraka kuwaondoa mafundi waliokuwa chini ya ardhi pamoja na watu waliokuwa jirani na eneo hilo ambapo wote waliweza kutoka salama. Vikosi vya uokozi vilivyohusisha Ofisi ya Mgodi, Ofisi ya Madini, Kikosi cha Uokozi na Zimamoto, Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vya usalama vilifika mara moja katika eneo la tukio na kusimamisha shughuli zote za mgodi kwa muda, kuweka utepe wa tahadhari katika eneo lililoathirika na kudhibiti wananchi waliokuwa wakijaribu kusogea katika eneo la hatari.
Ukaguzi wa kina unaendelea kufanywa ili kubaini hatua sahihi za ukarabati na kuandaa mpango salama wa kuendelea na shughuli za uchimbaji.
Hadi sasa, kwa mujibu wa taarifa ya pamoja ya timu ya uokozi, wakaguzi wa migodi na vyombo vya usalama, hakuna mtu aliyeripotiwa kupata majeraha wala kupoteza maisha kutokana na tukio hilo.
Tume ya Madini inawakumbusha wachimbaji na wananchi wote kuendelea kuzingatia taratibu za usalama migodini na kutoa taarifa mapema kwa Tume ya Madini au vyombo vya dola wanapoona dalili zozote za hatari ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wakati.







0 comments:
Post a Comment