Nafasi Ya Matangazo

March 31, 2026





Na Mwandishi wetu, Dodoma
Wizara ya Madini imekutana na ujumbe wa wawekezaji kutoka Jamhuri ya Watu wa China unaotoka katika Kampuni ya Kimataifa ya Liaoning Fangda Group, kwa lengo la kujadili na kubaini maeneo ya kimkakati ya ushirikiano katika kuendeleza Sekta ya Madini nchini Tanzania.

Ujumbe huo uliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kampuni hiyo, Bw. Ao Xinhua, ambaye ameambatana na wataalamu mbalimbali kutoka Sekta za Viwanda, Madini na Teknolojia.

Kikao hicho kilifanyika Machi 30, 2026 katika Ukumbi wa Tume ya Madini jijini Dodoma, kikiongozwa na Kamishna wa Madini, Dkt. AbdulRahman Mwanga.

Katika majadiliano hayo, pande zote mbili zilijikita katika kuchambua fursa mbalimbali zilizopo katika mnyororo mzima wa thamani wa Sekta ya Madini, ikiwemo utafiti wa madini, uchimbaji, uongezaji thamani (beneficiation), pamoja na uwekezaji katika teknolojia za kisasa za uchakataji wa madini.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Dkt. Mwanga alieleza kuwa Tanzania ina mazingira rafiki ya uwekezaji, sera thabiti na mifumo ya kisheria inayolenga kuvutia wawekezaji wa ndani na nje, huku akisisitiza dhamira ya Serikali katika kuhakikisha rasilimali za madini zinatumika kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya viwanda.

Kwa upande wake, Bw. Ao Xinhua alieleza kuridhishwa na fursa zilizopo nchini na kuonesha nia ya dhati ya Kampuni yake kuwekeza na kushirikiana na Tanzania katika maeneo ya kimkakati, hususan katika miradi ya madini na viwanda vinavyoongeza thamani ya rasilimali hizo.

Kampuni ya Liaoning Fangda Group ni miongoni mwa Kampuni kubwa duniani yenye uwekezaji katika madini ya chuma, madini mengine, usafiri wa anga na uzalishaji dawa, jambo linaloifanya kuwa mshirika muhimu katika juhudi za Tanzania za kukuza uchumi wa viwanda.

Kikao hicho ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuendelea kufungua milango ya ushirikiano wa kimataifa na kuvutia uwekezaji wenye tija katika sekta ya madini, ambayo inaendelea kuwa mhimili muhimu wa ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Posted by MROKI On Tuesday, March 31, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo