Nafasi Ya Matangazo

January 31, 2024



Makao Makuu ya Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika ambayo yatahifadhi  kumbukumbu na Historia ya Ukombozi wa nchi za Bara la Afrika yanatarajiwa  kujengwa katika eneo la Kiromo wilayani Bagamoyo, Pwani ili kuenzi mchango wa Tanzania katika harakati za ukomboa Barani Afrika.

Hayo yamebainishwa Januari 30, 2024 Jijini Dodoma katika kikao cha Mawaziri wa Wizara Tano kilichoongozwa na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma.

Kikao hicho kimebainisha sababu za kujengwa Makao Makuu hayo katika eneo hilo lenye ukubwa wa hekari 100  kuwa ni  utekelezaji wa Azimio la Umoja  wa Afrika (AU) la mwaka 2011 lililoelekeza Kamisheni ya Umoja huo kushirikiana na Tanzania katika  kujenga makao makuu hayo kwa kuzingatia kuwa  Makao Makuu ya sasa ya Kituo cha Urithi wa Bara hilo yapo katika Jengo la Kihistoria la iliyokua Makao Makuu ya Kamati ya Ukombozi ya Afrika jijini Dar es Salaam.

Kupitia Makao Makuu hayo nchi mbalimbali za Umoja wa Afrika zitakuwa na maeneo maalum ya kuonesha Historia na kumbukumbu mbalimbali za  harakati za ukombozi hatua itakayovutia wageni kutoka Mataifa mbalimbali kukitembelea kituo hicho.

Aidha, Wizara inatarajia kuanzisha ufadhili wa mafunzo ya muda mfupi kwa vijana wa nchi zilizoshiriki katika harakati za Ukombozi wa Afrika itakayojulikana kama "Hashim Mbita Scholarship" kwa ajili ya kujifunza kwa kina kuhusu Historia hiyo, pamoja na Kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Mataifa ya Afrika hasa yaliyosaidiwa na Tanzania kujikomboa.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mbarouk N. Mbarouck, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe.Omar Kipanga, Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Deogratius Ndejebi, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula, Makatibu Wakuu   na Watalaam kutoka Wizara hizo.

Na Shamimu Nyaki
Posted by MROKI On Wednesday, January 31, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo