Nafasi Ya Matangazo

January 31, 2024



Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi, Eng. Aisha Amour (kulia), akisisitiza jambo kwa Katibu Mkuu wa Kilimo, Gerald Mweri (kushoto) na wataalmau kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Dodoma walipokagua eneo la Mtanana kufuatia mafuriko katika eneo hilo leo Januari 30, 2024,
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Dodoma, Eng. Zuhura Amani (kushoto), akiwaonesha Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi, Eng. Aisha Amour na Katibu Mkuu wa Kilimo, Gerald Mweri, hali ilivyokuwa walipokagua eneo la Mtanana kufuatia mafuriko katika eneo hilo leo Januari 30, 2024,
Abiria wakisubiri hali iwe shwari ili waendelee na safari kufuatia kuwepo kwa mafuriko katika eneo la Mtanana, barabara kuu ya Morogoro -Dodoma
Magari yakianza kupita baada ya hali kuwa shwari kufuatia kuwepo kwa mafuriko katika eneo la Mtanana, barabara kuu ya Morogoro –Dodoma.
**************
Katibu Mkuu Ujenzi, Balozi, Eng. Aisha Amour ameruhusu magari kupita katika eneo la Mtanana, barabara kuu ya Dodoma - Morogoro mara baada ya mafuriko kupungua katika eneo hilo ambalo mawasiliano kati ya Mtanana na Kibaigwa kukatika kufuatia mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia leo Januari 30, 2024.

Akizungumza katika eneo hilo, Balozi Amour amesema hali ya barabara sasa ni shwari hivyo magarai na wananchi watumie na kuitaka Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Dodoma kusimamia huduma ya usafiri katika eneo hilo wakati wote .

“Tuliifunga barabara hii kwa saa tatu ili kujiridhisha na uimara wa barabara kufuatia mvua kubwa iliyonyesha katika eneo hili na mikoa ya jirani na kusababisha maji kupita juu ya barabara”, amesema Balozi, Eng. Amour.

Katika hatua nyingine, Makatibu wakuu wa wizara ya Ujenzi na Kilimo, Balozi Aisha Amour na Gerald Mweri, wamekagua mafuriko katika eneo hilo na kueleza hatua ambazo Serikali imeanza kuchukua ili kumaliza kabisa changamoto ya mafuriko katika eneo hilo.

Balozi Eng. Amour amesema tayari Mkandarasi amepatikana, fedha zimetengwa na vifaa kwa ajili ya kujenga barabara na madaraja makubwa katika eneo la Mtanana- Kibaigwa (KM 6) utaanza mara baada ya mvua kupungua.

“Tumedhamiria kumaliza tatizo hili kwa kujenga hizi Kilomita 6 kati ya Mtanana hadi Kibaigwa kwa kuweka madaraja makubwa na kuongeza upana wa barabara ili kudhibiti changamoto ya kila mwaka katika eneo hili”, amesisitiza Balozi, Eng. Amour
Amesema kazi inayoendelea kwa sasa ni kuimarisha kingo za barabara ili mafuriko yanayotokea sasa yasibomoe barabara na kuhatarisha huduma ya usafiri katika eneo hilo.

Amemtaka Meneja wa TANROADS mkoa wa Dodoma kushirikiana na wananchi na viongozi ili eneo hilo lipitike mchana na usiku na kuzuia kwa muda huduma za usafirihaji pale maji yanapozidi ili kulinda usalama wa watu na mali.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo, Gerald Mweri amesema tayari kazi ya ujenzi wa mabwawa katika upande wa juu ya barabara imeanza na usanifu kwa ajili ya mabwawa mengine mawili kwa upande wa chini, usanifu unaendelea ili kuhakikisha maji yote yanayopita katika eneo hilo yanavunwa na kutumiwa kwa ajili ya shughuli za kilimo katika kipindi chote cha mwaka.

“Tutahakikisha mabwawa haya yanajengwa kwa haraka ili kuwawezesha wananchi wa eneo hili kunufaika na uzalishaji wa mazao ya kilimo na biashara katika kipindi chote cha mwaka na hivyo kukuza uchumi wao”, amesisitiza.

Ukaguzi wa Makatibu Wakuu hao katika eneo unafuatia ziara ya Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa katika eneo hilo ambapo alisisitiza umuhimu wa makatibu wakuu wa Kilimo na Ujenzi kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa eneo hilo.
Posted by MROKI On Wednesday, January 31, 2024 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo