Mkutano Mkuu wa Baraza la 15 la Wakala wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu (IRENA) umezinduliwa rasmi mjini Abu Dhabi Falme za kiarabu na Rais wa Baraza la 14 la IRENA, Mhe.Dkt Jimmy Gasore, Waziri wa Miundombinu wa Rwanda ambaye anamaliza muda wake.
Gasore amewataka nchi wanachama wa IRENA kuhakikisha wanaharakisha maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya nishati jadidifu ambayo ni rafiki kwa mazingira kwa maslahi mapana ya nchi wanachama ili kuimarisha upatikanaji wa Nishati kwa nchi wanachama.
Amesema miradi ya nishati jadififu imekuwa ni chachu ya kuleta maendeleo na utunzaji wa mazingira licha ya kuwepo kwa changamoto ya mabadiliko ya tabianchi jambo ambalo amesema nchi wanachama wanaendelea na mapambano dhidi ya kupunguza hewa ya ukaa na kuwa na miradi ya nishati rafiki kwa mazingira.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa nafasi ya Rais wa Baraza la 15 la IRENA, Waziri wa Mazingira Mabadiliko ya Tabianchi na Nishati wa Slovenia, Bojan Kumer amesema ipo haja ya kuwa na sera madhubuti za kutekekeza miradi ya nishati jadififu na kuwashirikisha wananchi kwenye utekelezaji wa miradi hiyo kwa nchi wanachama wa IRENA.
Amesema miradi ya nishati jadidifu licha ya kuwa rafiki kwa mazingira, pia ina gharama nafuu kwenye utekelezaji wake ikilinganishwa na vyanzo vingine ambavyo vinatumika kuzalisha nishati .
Mkutano huo wa 15 wa Baraza la Wakala wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu IRENA umehudhuriwa na wadau zaidi ya 2,000 ikiwemo nchi wanachama wa IRENA, na wadau wa sekta binafsi na makampuni mbalimbali yanayojihusisha na miradi Ya nishati.
Aidha katika mkutano huo nchi wanachama walichagua wawakilishi wa Rais na Makamu wa Rais wa Baraza la 15 la IRENA ambapo Rais alichaguliwa kutoka nchi ya Slovenia na Makamu wa Rais alichaguliwa kutoka Namibia sambamba na wawakilishi wengine baraza la IRENA kutoka nchi za Costa Rica, Falme za Kiarabu UAE, Uturuki,kutoka kila Bara kwa ajili ya uwakilishi.
Katika mkutano huo ujumbe wa Tanzania unawakilishwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu Dkt Khatibu kazungu, akiongozana na Naibu Mkurugenzi Mtendaji uzalishaji kutoka TANESCO Mha Costa Rubagumya, Kamishna Msaidizi wa Umeme na nishati Jadidifu Mha. Imani Mruma, Meneja utafiti kutoka TANESCO Samwel Kessy na Meneja utafiti kutoka kampuni ya uendelezaji Jotoardhi Mha Mkufu Tindi.
0 comments:
Post a Comment