Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akijibu maswali bungeni wakati wa kipindi cha maswali na majibu katika Kikao cha pili Mkutano wa 14 wa Bunge jijini Dodoma leo Januari 31, 2024.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akijadiliana jambo na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni katika Kikao cha pili Mkutano wa 14 wa Bunge jijini Dodoma leo Januari 31, 2024.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akijibu maswali bungeni jijini Dodoma leo
Januari 31, 2024 kuhusu mkakati wa Serikali wa kupambana na mabadiliko ya
tabianchi, katika Kikao cha pili Mkutano wa 14 wa Bunge.
************
Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa
kushirikiana na wizara za kisekta imeanza kufanya tathmini nchi nzima
kubainisha maeneo yanayohitaji kufanyiwa maboresho kukabiliana na athari za
kimazingira.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge
wa Mtambwe Mhe. Khalifa Mohammed Issa aliyetaka kujua lini Serikali itafanya
utafiti kuyabaini maeneo yaliyoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.
Katika kushughulikia changamoto ya mabadiliko ya
tabianchi Dkt. Jafo amesema kuwa Serikali imeanza kuyafanyia kazi maeneo hayo
kwa kutekeleza miradi ya mazingira pande zote mbili za Muungano.
Amesema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais inaendelea na
utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa tuta linalozuia maji ya bahari kuingia kwenye
makazi na mashamba unaotekelezwa eneo la eneo la Sipwese Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini, Pemba.
Halikadhalika, amesema mradi huo unatekelezwa pia katika
eneo la Mikindani, Mtwara ambako kunajengwa ukuta utakaosaidia kupunguza kasi
ya maji ya bahari kuingia kwenye makazi ya watu na kuta kwa ajili ya kurejesha
fukwe katika hali yake.
“Katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya
tabianchi Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imetuma timu ya wataalamu ikishirikiana
na wizara za kisekta kufanya tathmini ambayo itatusaidia kubaini maeneo gani yenye
changamoto na kuyafanyia kazi hivyo kuhakikisha nchi yetu inakuwa salama,” amesisitiza
Waziri Dkt. Jafo.
Awali, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano
na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis alisema Serikali inaendelea na kampeni za kuhamasisha wananchi
kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo zoezi la upandaji wa miti katika
maeneo yote nchini.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Mariam Nasoro Kisangi aliyeuliza mkakati ya Serikali wa kupambana na mabadiliko ya
tabianchi, Mhe. Khamis alisema Ofisi ya Makamu wa
Rais inafanya kampeni hizo kwa kushirikiana na taasisi kuhamasisha ubunifu,
utafiti na uendelezaji wa teknolojia za kukabiliana na changamoto hiyo.
Mhe. Khamis alibainisha kuwa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imeandaa na kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na
Mabadiliko ya Tabianchi (2021-2026) na Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi ya
Mazingira (2022-2032).
Aidha, alisema kuwa kwa upande wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar upo Mkakati wa Mabadiliko ya Tabianchi Zanzibar (2014-2030)
ambao unatekelezwa kupitia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais yenye dhamani ya
mazingira.
Alisema Serikali inayo Mipango ambayo kwa pamoja imeelezea
changamoto na hatua mbalimbali za kuzifuata katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi
yanayoathiri maeneo mbalimbali hapa nchini.
“Tunatambua mkakati tulionao wa kusafisha mito na
tayari Mhesehimiwa Waziri (Dkt. Jafo) alishaunda Kamati na kubaini chanzo
mkusanyiko wa mchanga mkoani Dar es Salaam na kuziba mifereji nasi tunaendelea kutoa
elimu na kusimamia Sheria ya Mita 60 na Usafishaji wa mito kwa kutoa mchanga na
takataka nyingine,” alisema Mhe. Khamis.
0 comments:
Post a Comment