Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mh.Samia Suluhu Hassan akiwa katika mazungumzo na Mkurugenzi wa Idara
ya Afrika kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF-) Abebe Aemro Selassie Ikulu
Jijini Dodoma leo tarehe 29 Juni, 2021.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 29 Juni, 2021 amefanya
mazungumzo na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika Bw.Abebe Aemro Selassie kutoka
Shirika la Fedha Duniani (IMF) kuhusu masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na
jinsi Shirika hilo litakavyosaidia Tanzania kukabiliana na ugonjwa wa Corona.
Mhe. Rais Samia amekutana na Mkurugenzi huyo ambaye aliambatana na ujumbe wake Ikulu Jijini Dodoma.
Bw. Selassie ametoa salamu kutoka kwa Mkurugenzi wa IMF Bi. Kristalina Georgieva ambaye amemuhakikishia Mhe. Rais Samia kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Tanzania katika kufikia maendeleo yanayokusudiwa.
Akizungumzia kuhusu kukabiliana na ugonjwa Corona (Covid 19), amesema IMF ipo tayari kuendelea kufanyakazi na Wataalam wa Tanzania kuandaa andiko litakalowezesha kupata msaada wa fedha kwa ajili ya kupambana na athari zitokanazo na ugonjwa wa Corona.
Pia Bw. Selassie amesema IMF itasaidia Tanzania kupata fedha kwa ajili ya kuimarisha sekta zilizoathirika na ugonjwa wa Corona ikiwa ni pamoja na sekta ya Utalii, Maji na Afya.
Kwa upande wake Mhe. Rais Samia amesema kupitia Kamati Maalum aliyoiunda kukabiliana na ugonjwa wa Corona itashirikiana na Wizara ya Fedha kuandaa mpango wa jinsi ya kutekeleza maazimio ya ripoti maalum kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo wa Corona.
Mhe. Rais Samia ameishukuru IMF kwa kuendelea kufanya kazi na Serikali yake kwa lengo la kuhakikisha Tanzania inapiga hatua kubwa ya kimaendeleo.
0 comments:
Post a Comment