Malazi, chakula na mavazi ni mahitaji ya msingi ya binadamu. Mwanadamu anapoyapata mahitaji haya kwa ukamilifu wake, hujenga utulivu wa akili, moyo na ari ya kufanya kazi kwa bidii.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) nchini kinatekeleza mpango mkakati wake wa kuhakikisha watumishi wa Chama wanajengewa makazi ya kudumu kwani makazi ni hitaji la msingi la binadamu.
Kupatikana kwa makazi hayo, kunachochea uwajibikaji na uchapakazi wa watumishi hao, ambao wapo nchi nzima kwa madhumuni ya kuwatumikia wananchi.
CCM mkoani Tanga, chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake, Rajab Abdallah, maarufu "Ustadhi Rajab," ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MCC), umedhamiria kuhakikisha ujenzi wa nyumba 36 unakamilika kwa wakati katika wilaya zote tisa za mkoa wa Tanga.
Kila wilaya zitajengwa nyumba nne za makatibu wa Chama wilaya, na za makatibu wa jumuiya ya vijana, wanawake na wazazi. Jumla ya gharama za nyumba zote 36 ni shilingi bilioni 2.5.
Ikumbukwe kuwa, katika Uchaguzi Mkuu wa Chama wa mwaka 2022, Ustadhi Rajab aliahidi endapo atachagukiwa katika nafasi ya Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga, atahakikisha anasimamia na kuwezesha ujenzi wa nyumba hizo.
Ujenzi wa nyumba hizo unaendelea vizuri na ni faraja kuona, Mei 31, 2026, Ustadhi Rajab alikabidhi hundi ya shilingi milioni 500 kwa Katibu wa CCM mkoa wa Tanga, Mfaume Kizigo, ili ziwezeshe shughuli za ujenzi wa nyumba hizo ambazo malengo ni kukamilika ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.
Ustadhi Rajab amekuwa na ubunifu wa kuwashirikisha marafiki zake na wadau mbalimbali katika shughuli za maendeleo ndani ya mkoa wa Tanga, jambo linalosaidia utatuzi wa changamoto kwa haraka.
Kwa hakika, Ustadhi Rajab amefanya kazi kubwa na ya kupongezwa katika mradi huu kabambe wa ujenzi wa nyumba 36 za watumishi wa Chama mkoani humo. Ahadi ni deni na sasa deni hilo linalipwa.







0 comments:
Post a Comment