WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amezindua Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano
2021/2022–2025/2026 utakaogharimu shilingi trilioni 114.8, ambapo sekta binafsi
inatarajiwa kuchangia shilingi trilioni 40.6 na sekta ya umma shilingi trilioni
74.2.
“...fedha hizo zinajumuisha
mikopo na misaada ya wabia wetu wa maendeleo. Kwa niaba ya Mheshimiwa Samia
Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kuwahakikishia
kwamba fedha hizi zitapatikana na malengo tuliyojiwekea yatatekelezwa.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo
(Jumanne, Juni 29, 2021) wakati akizindua Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa
wa Miaka Mitano 2021/2022–2025/2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya
Kikwete, jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema mpango huo
una dhima ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu na
umejikita katika kuchochea uchumi shindani na shirikishi; kuimarisha uwezo wa
uzalishaji viwandani na utoaji huduma; kukuza uwekezaji na biashara; kuchochea
maendeleo ya watu; na kuendeleza rasilimali watu.
Amesema Serikali itahakikisha
malengo ya Mpango huo yanafikiwa. “Kamwe hatutafumbia macho tabia ya ukwepaji
kodi, kazini, ufujaji wa fedha na rushwa na tutaendelea kuenzi bunifu na
kupokea mawazo mbadala yenye lengo la kuboresha utekelezaji wa Mpango huu.”
“Katika Mpango huu wa Tatu
tutaendelea kutekeleza miradi ya kielelezo kama ilivyokuwa katika Mpango wa
Pili hususan ujenzi wa reli kwa kiwango cha Kimataifa (SGR), ujenzi wa mradi wa
kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115;
ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta (EACOP) na ununuzi wa meli na ujenzi wa
bandari ya uvuvi (Mbegani).”
Kadhalika, Waziri Mkuu
ameongeza kuwa mpango huo ni mkakati mahsusi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya
Mwaka 2020. “Niwaahidi Watanzania kwamba mambo yote tuliyoahidi wakati wa
kampeni za uchaguzi wa mwaka 2020, yanaenda kutekelezwa kupitia Mpango huu.”
Waziri Mkuu amesema mpango huo
umezingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025; Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya
2020; Mpango Elekezi wa Muda Mrefu 2011/2012–2025/2026 na Matokeo ya Tathmini
Huru ya utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano
2016/2017–2020/2021.
Pia, Waziri Mkuu amesema
mpango huo umezingia sera na mikakati mbalimbali ya kisekta; matokeo ya tafiti
zilizofanywa na vyuo na taasisi mbalimbali nchini; Dira ya Afrika Mashariki
2050; Dira ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika 2050; Ajenda 2063 ya
Maendeleo ya Afrika; Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030; na Makubaliano ya
Paris chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi.
“Wizara ya Fedha na Mipango
endeleeni na utaratibu wa kutoa elimu ya kutosha ili kumwezesha kila mmoja
kushiriki kikamilifu katika utekelezaji. Aidha, ninaagiza Wizara, Taasisi za
Umma, Idara Zinazojitegemea Wakala za Serikali, Sekta Binafsi na Wadau wote wa
maendeleo kuhakikisha ofisi zao zina nakala ya Mpango huu na kuanza
kuutekeleza.”
Kwa upande wake, Katibu Mkuu
wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba amesema mpango huo ni mwendelezo
wa jitihada za Serikali za kuimarisha upangaji mipango na kusimamia rasilimali
za ndani ya nchi ikijumuisha rasilimali za madini, maliasili, gesi asilia, ardhi,
fedha na rasilimali watu kwa lengo la
kuboresha hali ya maisha ya Watanzania wote.
Amesema ili kuhakikisha mpango
huo unatekelezwa kwa ufanisi na unafikia malengo yaliyopangwa, Wizara imeandaa
mwongozo wa kitaifa wa ufuatiliaji na tathmini wa miradi na programu za
maendeleo na mfumo wa kitaifa wa kusimamia miradi ya maendeleo.
Naye, Mwakilishi Mkaazi wa
Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Nchini Tanzania, Christine
Musisi amesema wananchi, Serikali, wadau wa maendeleo, sekta binafsi watautumia
mpango huo kama nyenzo muhimu ya utekelezaji wa kufikia malengo ya Dira ya
Taifa ya Maendeleo ya 2025 na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030. Pia
ameihakikishia Serikali kwamba mashirika yote ya Umoja wa Mataifa yataunga
mkono utekelezaji wa mpango huo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
0 comments:
Post a Comment