Mwandishi Wetu
AFYA bora ya kinywa na meno kwa mtoto ni muhimu na ina uhususiano wa moja kwa moja na afya yake kwa ujumla. Utunzaji huu unatakiwa kuanza na meno ya utotoni
Wazazi au walezi wengi wamekuwa wakijiuliza kwa nini wahangaike kutunza meno ya utotoni ambayo yanatarajiwa kung’oka?
Katika mahojiano na Daktari wa afya ya kinywa na meno, Dk Frank Mbaga anasema meno ya utoto ni muhimu kwa kuwa hali mbaya ya afya ya meno ya utotoni huathiri hali ya afya ya meno ya ukubwani, humzuia mtoto kutafuna vizuri na hushindwa kutunza nafasi kwa ajili ya meno ya ukubwa.
Madaktari wa afya ya kinywa na meno na watafiti wanakualiana kwamba mambo yanayochangia maamubukizo na ugonjwa wa kuoza na kutoboka meno mapema kwa watoto ni matumizi ya vitu vyenye sukari na matumizi ya chupa za chuchu ya maziwa.
“Tatizo la utobokaji wa mapema wa meno ya watoto linatisha kwa sababu linaonekana kama ni ugonjwa wa kawaida, na limekuwa likiongezeka kwa kasi zaidi kwa watoto wadogo.”
Takwimu za Tinanoff & O`sullivan za mwaka 1997 zinaonyesha kuwa asilimia 90 ya watoto wenye umri kati ya miaka 3-5 wanatatizo hili. Na katika nchi zinazoendelea hali ni mbaya kwani ni asilimia 70. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI MAKALA HAYA
“Afya bora ya kinywa na meno huepusha maumivu, hupunguza uwezekano wa uambukizo, na huwezesha kutafuna vizuri ili kupata virutubisho muhimu kwa ajili ya kujenga kinga dhidi ya magonjwa na kusaidia ukuaji.
Anaongeza: “Afya nzuri ya kinywa na meno pia humfanya mtoto aweze kuhudhuria masomo ipasavyo na hivyo kupata matokeo mazuri”.
Akizungumzia sababu na njisi ya kukabiliana na tatizo hilo, Dk Mbaga anasema tatizo hilo husababishwa na matumizi ya mara kwa mara na ya muda mrefu ya sukari na vitu vyenye sukari. “Meno yanaathirika kwa urahisi kwa sababu bakteria hushamiri kwenye maeneo yenye sukari na hivyo kuendeleza kazi ya kutoboa meno.”
Bakteria wanaoishi kinywani humeng’enya mabaki ya vyakula tunavyokula na kutoa tindi kali ambayo inadhoofisha sehemu ya nje ya jino na kusababisha jino kutoboka.
Anaongeza: “Mtoto akiwa amelala au anasinzia huku chuchu ya chupa ya maziwa au chuchu ya mama ikiwa mdomoni mwa mtoto, huongeza muda wa sukari kukaa kwenye meno ya mtoto na hivyo kuongeza tobo. Hili ni jambo la kuepuka.”
Akizungumzia dalili za mwanzo za ugonjwa wa kuoza kwa meno ya mtoto, Dk Mbaga anasema dalili za mwanzo ni alama za chaki nyeupe au mistari kwenye meno na tabaka gumu la enameli.
Ugonjwa wa kutoboka huchukua miezi au miaka kadhaa kuonekana, hivyo ni muhimu kuuzuia ukiwa katika umri mdogo.
“Ikiwa haujatibiwa mapema baada ya vijishimo kuanza, hutengeneza usahaa, na miundo ya ndani ya jino na nyama huharibiwa.
Anasema matumizi ya mara kwa mara ya fluoridi huongeza udhibiti wa jino dhidi ya bakteria na hivyo kuzuia kutoboka.
“Utunzaji sahihi, matumizi ya fluoridi na ulaji unaofaa huwa na manufaa ya kurejesha madini.
Anaongeza: “Sukari ni kichocheo kwa bakteria kuanza mchakato wa kuozesha meno, hivyo suala la kupunguza matumizi ya sukari katika lishe ya mtoto ni jambo muhimu. Watoto wadogo wanategemea wazazi wao. Hivyo kuzuia kutoboka kwa ameno ya watoto hutegemea wajibu wa mzazi au mlezi wake.
Dk Mbaga anahitimisha kwa kusema: “Njia bora za kutekeleza mpango kwa kuzia kutoboka kwa meno kwa watoto wadogo hutegemea wazazi au walezi kuelewa kuwa wana uwezo wa kudhibiti,”
Anaongeza: “Madaktari wa afya ya kinywa na meno, wataalamu wa afya, na jamii kwa ujumla, ni lazima kutambua kwamba zinahitajika jitihada za pamoja ili kuhakikisha uboreshaji wa huduma muhimu kwa watoto ili waweze kupata huduma nzuri na stahiki za meno wanazostahili.”
Makala haya yameandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanaopambana na Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza Tazania (TJNCDF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TANCDA). Maoni au ushauri tuma TJNCDF, S.L.P 13695, Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment