Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Serikali imeainisha mkakati mahsusi wa kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini nchini, kwa kuweka kipaumbele katika utoaji wa leseni, upatikanaji wa mitaji, teknolojia, masoko ya uhakika pamoja na maeneo yenye taarifa za utafiti.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, wakati wa kikao cha kwanza cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kilichofanyika leo Januari 15, 2025 katika Ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni jijini Dodoma.
Waziri Mavunde amesema kuwa shughuli zote za utafutaji, uchimbaji, uongezaji thamani na biashara ya madini zinatekelezwa kwa mujibu wa Sera ya Madini ya mwaka 2009 na Sheria ya Madini, Sura ya 123, kwa lengo la kuhakikisha wachimbaji wadogo wananufaika ipasavyo na rasilimali za madini kwa tija na uendelevu.
Ameeleza kuwa utekelezaji wa Sera na Sheria hizo umeleta mageuzi makubwa katika sekta ya madini, ambapo mchango wake katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 2.7 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 10.1 mwaka 2024.
Ameongeza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na kuimarika kwa usimamizi, uwazi na uwajibikaji, hali iliyosababisha makusanyo ya maduhuli ya Serikali kuongezeka kutoka shilingi bilioni 173.7 mwaka wa fedha 2012/13 hadi kufikia shilingi trilioni 1.071 mwaka 2024/25.
Waziri Mavunde amesema, Serikali imeendelea kuwapa kipaumbele wachimbaji wadogo kwa kuwatengea maeneo yenye taarifa za utafiti na kuwapatia leseni za uchimbaji mdogo katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Nyanhwale, Simanjiro, Mbogwe na Chunya, hatua inayolenga kuongeza tija, usalama na mapato yao.
Aidha, amesema Wizara ya Madini imeanzisha mkakati wa Mining For A Brighter Tomorrow (MBT) unaolenga kuwawezesha wachimbaji wadogo katika nyanja za mitaji, teknolojia na taarifa za kijiolojia, ili waweze kujitegemea badala ya kutegemea wadhamini kutoka nje ya nchi. Mpaka sasa, zaidi ya wachimbaji wadogo 12,000 wamenufaika na mpango huo.
Kwa upande wa biashara ya madini nje ya nchi, Waziri Mavunde amesema mauzo ya madini yameongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 1.94 mwaka 2013 hadi dola bilioni 4.12 mwaka 2024. Aidha, Serikali imeanzisha masoko 44 ya madini na vituo 114 vya ununuzi na uuzaji wa madini, hatua iliyoboresha upatikanaji wa masoko ya uhakika na bei shindani kwa wachimbaji.
Katika eneo la ajira, amesema ajira za moja kwa moja katika kampuni za madini zimeongezeka kutoka ajira 7,280 mwaka 2011 hadi ajira 19,371 mwaka 2024. Sambamba na hilo, ununuzi wa bidhaa na huduma za ndani umeongezeka kutoka shilingi trilioni 1.85 mwaka 2018 hadi shilingi trilioni 4.41 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 88.
Akizungumzia kuimarishwa kwa akiba ya fedha za kigeni, Waziri Mavunde amesema kuanzia Oktoba 1, 2024, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilianza kununua dhahabu kupitia viwanda vya ndani vya kusafisha dhahabu, na hadi kufikia Desemba 2025 ilikuwa imenunua tani 16.4 za dhahabu zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 2.2. Hatua hiyo imeifanya Tanzania kuingia katika orodha ya nchi kumi bora barani Afrika kwa hifadhi ya dhahabu.
Ameongeza kuwa Sera ya Madini pia inasisitiza uwajibikaji wa kampuni za madini kwa jamii (CSR), ambapo miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa shule, miradi ya maji, barabara, huduma za afya na kilimo inaendelea kutekelezwa katika maeneo yanayozunguka migodi.
Kwa upande wao, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, Makamu Mwenyekiti Mhe. Simon Songe na Wajumbe wa Kamati hiyo wameipongeza Wizara ya Madini kwa mafanikio yaliyofikiwa, pamoja na kuipongeza Benki Kuu ya Tanzania kwa kununua zaidi ya tani 16 za dhahabu ndani ya kipindi kifupi.
Aidha, Kamati imesisitiza haja ya Wizara ya Madini kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuongeza wigo wa utafiti wa madini kutoka asilimia 16 ya sasa ili kuongeza fursa za ushiriki wa Watanzania katika sekta ya madini.
Akiwasilisha taarifa kuhusu Sera na Sheria zinazosimamia Wizara ya Madini, Kamishna wa Madini, Dkt. AbdulRahman Mwanga, amesema utekelezaji wake umewezesha kuanzishwa kwa viwanda 16 vya kuyeyusha madini na viwanda sita vya kusafisha madini, pamoja na migodi miwili ya kati na migodi mikubwa miwili iliyo katika hatua mbalimbali za kuanza uzalishaji.











0 comments:
Post a Comment