Nafasi Ya Matangazo

January 17, 2018

Mwandishi Wetu

Tabia na mienendo ya watu kimaisha imekuwa ni sababu ya matatizo kwao binafsi, jamii na hata kwa uchumi wa nchi, ambao unahitaji sana nguvu kazi inayotokana na afya njema.

Afya ya mtu yeyote inategemea sana namna anavyokula, anavyoishi na kujiweka katika mazingira yanayomzunguka ili kujikinga na maradhi.

Miongoni mwa mambo yanayohatarisha afya za watu wengi nchini ni ulaji usiofaa, kutokufanya mazoezi au kazi ngumu, utumiaji wa tumbaku, vileo na vipodozi visivyo salama. 

Tabia nyingine mbaya kwa afya ni uchafuzi wa mazingira, hewa, maji na uzalishaji wa makelele yasiyokuwa ya lazima.

Mambo mengine ni ile hali ya mtu kujiweka katika mazingira hatarishi kiusalama kama vile ngono zembe na mwendo kasi wa vyombo vya usafiri kiasi cha kuweza kusababisha ajali na kujeruhiwa au kufa.

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa magonjwa yasiyoambukiza yanaongezeka kwa kasi katika jamii ya Watanzania. 

Magonjwa hayo ni kama vile kisukari, maradhi ya moyo, saratani, magonjwa sugu ya njia za hewa na mapafu, ajali za barabarani na magonjwa ya akili. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI MAKALA HAYA.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa magonjwa yasiyoambukiza yataongezeka zaidi katika Bara la Afrika kuliko mabara mengine, kutokana na mabadiliko ya teknolojia kubadilisha mitindo ya kuishi.

Utafiti uliofanywa na Sayoki G.M Mfinanga na wenzake juu ya magonjwa ya kuambukiza kwa kuyalinganisha na yale yasiyo ya kuambukiza miongoni mwa jamii ya Watanzania umebaini kuwa ugonjwa wa shinikizo la juu la damu sasa unafikia kiasi cha asilimia 45 ya magonjwa yote kwa watu wenye umri zaidi ya miaka 25 na magonjwa ya kisukari na saratani nayo pia yanaongezeka kwa kasi. Hivyo Watanzania hawana budi kuanza kuchukua tahadhari.

Afya inaweza kuboreshwa na kudumishwa kwa kuzingatia mtindo wa maisha unaofaa. 

Jambo muhimu ni kufahamu kwamba hakuna ugonjwa ambao hauna chanzo.
Wataalamu wa afya ya jamii wanasema kuwa takribani asilimia 53 ya magonjwa ya binadamu husababishwa na mtindo wa maisha usiofaa kwa mfano: ulafi, ulevi, kutofanya kazi ngumu, kutofanya mazoezi na ngono zembe.

Wataalamu wanaongeza kusema kuwa asilimia 21 ya magonjwa hutokana na uchafu wa mazingira na mwili na asilimia 16 hutokana na yale ya kurithi kupitia vinasaba (DNA).



Utafiti huo umebaini kuwa asilimia 10 ya magonjwa husababishwa na makosa yatokanayo na tiba kwa mfano matumizi mabaya ya dawa, vipimo vikubwa vya dawa na tiba zisizofaa.

Mambo ya kuepukwa
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa mtu binafsi anaweza kuimarisha afya yake iwapo atazingatia kanuni sahihi za afya.

Mwenyekiti wa Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania, Profesa Andrew Swai anasema kila mtu anapaswa kufanya mazoezi ili kuimarisha mwili.

“Sukari inayoingia mwilini kutokana na vyakula na vinywaji inapaswa kutumika kwa kuushughulisha mwili. Isipotumika ndipo inasababisha madhara mwilini,” anafafanua Profesa Swai.

Isitoshe, anashauri kula vyakula vya nafaka isiyokobolewa na matunda na siyo juisi ya matunda. Hii ni kutokana na ukweli kwamba nyuzinyuzi kwenye matunda husaidia sukari kuingia polepole mwilini tofauti na inayopatikana kwenye juisi.

Watanzania wengi hawali kiasi cha kutosha cha matunda na mbogamboga. Waingereza wana msemo: “An apple a day will keep the doctor away…An apple before bed makes the doctor beg his bread”. 

Huu ni msemo ambao unahimiza watu kutumia matunda mara kwa mara ili kiuepuka maradhi badala ya kusubiri hadi unapoanza kudhoofu ndiyo utumie, maana ugonjwa utakulazimisha ukatafute tiba.

Wanatumia msemo huo kuonyesha umuhimu wa kula vyakula vyenye asili ya mimea hasa matunda. Matunda pamoja virutubisho vingine, huupatia mwili vitamin C ambayo ni ya muhimu kwa ajili ya kinga ya mwili.

Ni muhimu kupunguza ulaji wa nyama na kuongeza mboga na matunda ili kuzuia magonjwa ya moyo, saratani, kisukari na kitambi.

Mwisho, magonjwa mengi huchukua muda mrefu kuanza kuonyesha dalili au kutambuliwa hivyo Profesa anashauri wenye umri zaidi ya miaka 40 kufanya uchunguzi wa mara kwa mara kwa magonjwa kama vile shinikizo la damu, kisukari na saratani.

Makala haya yameandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanaopambana na Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza Tazania (TJNCDF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TANCDA). Maoni au ushauri tuma TJNCDF, S.L.P 13695, Dar es Salaam.


Posted by MROKI On Wednesday, January 17, 2018 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo