Mwandishi Wetu
Wataalamu wa afya wanasema sigara haina manufaa yoyote kwa binadamu zaidi ya kuathiri afya na yeyote anayetumia tumbaku anawekwa kwenye kundi la wagonjwa.
Wavutaji wengi wa sigara wanafahamu sigara zina madhara mengi ya kiafya lakini si rahisi kwao kuziacha kwa vile wanajihisi bila kuvuta hawana uwezo wa kutekeleza kazi zao kikamilifu.
Kwa miaka mingi, wataalamu wamebaini kuwa pamoja na tumbaku kuwa na viambata vingi, kinachochochea hamu ya mara kwa mara (uraibu) ya uvutaji wa sigara ni kemikali aina ya nikotini.
Dk Ananya Mandal wa Chuo Kikuu cha Afya cha West Bengal nchini India anasema mtu anapovuta sigara, moshi wake huandamana na kemikali ya nikotini hadi kwenye mapafu na kunyonywa na vifuko vya hewa ambavyo huiingiza kwenye mfumo wa damu.
Katika makala yake aliyoiandika na kuchapishwa na Jarida la News Medical, Dk Mandal anasema iwapo mtu atakuwa anatafuna tumbaku, nikotini itakuwa inafyonzwa na ngozi laini puani na kuingizwa kwenye mfumo wa damu.
Nikotini inapokuwa kwenye mfumo wa damu husafiri hadi kichwani na kuachana na mishipa ya damu na kuingia kwenye ubongo.
Uchunguzi wa kisayansi umebaini kuwa nikotini baada ya kuingia kwenye mfumo wa damu si chini ya sekunde saba inakuwa imeufikia ubongo. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI MAKALA HAYA.
Ikiwa kwenye ubongo hupitia hatua kadhaa kabla ya kufanywa ni sehemu ya kazi za seli za mfumo wa fahamu.
“Hapa nikotini hujifananisha na kemikali nyingine ijulikanayo kama acetylcholine ambayo kazi yake ni kusambaza hewa safi,” anasema Dk Mandal, akifafanua:
“Hii hewa safi ni kwa ajili ya kutunza afya na kuwezesha utendaji mzuri wa viungo muhimu mwilini kama vile moyo, misuli na eneo la uwekaji kumbukumbu kwenye ubongo lijilikanalo kama cognitive.”
Dk Mandal anasema nikotioni ina umbo linalofanana na acetylcholine na inapopokelewa bila vikwazo na ubongo na humo hufanya mambo tofauti na kemikali hiyo ya kawaida mwilini.
“Tofauti na acetylcholine, Nikotini huenda kuvuruga utendaji wa ubongo. Nikotini husababisha acetylcholine ionekane kwenye ubongo sio ya maana sana. Badala yake, nikotini huonekana ni ya muhimu na manufaa zaidi,” anasema Dk Mandal.
Anaongeza: “Ni kwa sababu hiyo, ubongo unakuwa na tamaa ya kuona utendaji wake unahitaji nikotini ili kufanya kazi vizuri. Hapa ndipo mtu anakuwa na uraibu wa tumbaku. Ina maana asipotumia tumbaku hujisikia vibaya au mwili hauwezi kutekeleza wajibu wake. ”
Anasema uchunguzi wa maabara unaonyesha kuwa nikotini inakuwa kwenye tumbaku kavu kwa kiwango cha asilimia kati ya 0.3 hadi 0.6.
“Mvutaji hujenga tabia kwamba bila kutumia sigara utendaji wake wa ubongo haukai vizuri. Hivyo hujaribu kuvuta mara nyingi iwezekanavyo ili kufanya ubongo wake kupata nikotini ya kutosha. Hapa anakuwa amejijengea uraibu wa sigara.”
Jambo la kufahamu, anasema ni kwamba nikotini pia ina madhara mwilini lakini siyo kiambata pekee kinachoathiri mwili kwenye tumbaku.
Tafiti zinaonyesha kuwa moshi wa sigara una kemikali zaidi ya 4,000, ambazo zinauathiri mwili kwa njia mbalimbali.
Kati ya hizo, kemikali zaidi ya 50 zinasababisha saratani za aina mbalimbali kama vile za mapafu na koo.
Zipo aina zaidi ya 100 za saratani zinazomuandama binadamu na hupewa jina kulingana na kiungo inachoshambulia.
Tafiti zinaonyesha kuwa kwa kadiri dunia inavyopiga hatua za kiuchumi katika maeneo ya nchi zinazoendelea ndivyo pia magonjwa yasiyoambukiza yanavyozidi kujitokeza na kuipa hofu jamii.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dkt. Crispin Kahesa anasema tumbaku inachochea saratani za aina zote.
Anafafanua kwamba tumbaku huharakisha seli za mwili zilizoathirika kuingia katika hatua ya saratani eneo lolote la mwili.
Anatoa mfano kuwa kama mtu anaweza kuanza kuugua saratani sasa wakati ambapo kama asingekuwa anavuta ingeanza kuonyesha dalili baada ya miaka 20 ijayo.
“Saratani ni moja ya janga hatari katika afya zetu kwani wengi wa wagonjwa hushindwa kupona na huumwa muda mrefu na kupata mateso makubwa mwisho huishia kufariki,” anasema.
Dkt. Kahesa anasema tumbaku huchochea saratani kwa kushirikiana na vichocheo vingine kama vile pombe, virusi vya Ukimwi na kupungua kinga.
Makala haya yameandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanaopambana na Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza Tazania (TJNCDF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TANCDA). Maoni au ushauri tuma TJNCDF, S.L.P 13695, Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment