Nafasi Ya Matangazo

January 18, 2018

Mwandishi Wetu 
KINYWA ni moja ya viungo muhimu katika mwili wa binadamu hasa ikizingatiwa kwamba kinatumika kula, kuzungumza, kuhisi na ni sehemu ya uzuri wa sura ya mtu.

Kutoboka meno na kuharibika fizi vyote vinaweza kuathiri baadhi ya sifa za kinywa, kumfanya mtu atumie fedha nyingi kwa matibabu na hata kuathiri muonekano halisi wa mtu.

Mfano mzuri ni kwamba mtu aking’oa meno mengi mdomoni anaweza akaathiri muonekano mzuri wa mdomo na mashavu, kushindwa kutafuna na hata kutamka maneno vizuri, na asipokuwa mwangalifu katika kusafisha kinywa pia anaweza kuwa anatoa harufu mbaya mdomoni.


Kuoza meno ni nini?

Ushirika wa Vyama Vinavyokabili Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza (TANCDA) katika kuelimisha jamii juu ya magonjwa ya kinywa inaeleza kuwa kuoza kwa meno ni hali ya sehemu ya juu ndani ya jino kutoboka kutokana na ulaji wa mara kwa mara wa vyakula vyenye sukari.

Taarifa hiyo ya TANCDA inasema vijidudu vya bakteria humeng’enya mabaki vya vyakula vya sukari mdomoni na kutoa tindikali ambayo husababisha kudhoofu kwa sehemu ya nje ya meno na baadae hutoboka.

Takwimu zinaonyesha kati ya asilimia 60 hadi 90 ya watoto wote wenye umri wa kwenda shule duniani kote wana ugonjwa wa meno kutoboka.

Hapa nchini, watoto wenye umri kati ya miaka mine hadi sita, mtoto mmoja kati ya watatu ana jino lililotoboka au kuoza.

Vyakula vinavyochochea bakteria kuathiri meno ni biskuti, soda, keki, chokoleti, pipi, kashata, aisikrimu, visheti na ubuyu wenye sukari. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI MAKALA HAYA.


Dalili za kuoza meno

Kwa kawaida meno ni meupe, hayana vitobo na kazi yake muhimu ni kukata, kusaga vyakula na kuweka umbo zuri la mdomo kwa nje na anapotabasamu au kucheka.

TANCDA inaeleza kuwa dalili za meno kuoza ni alama nyeusi sehemu za pembeni au kutafunia, uwepo wa shimo kwenye jino au meno, maumivu ya meno, kuvimba sehemu ya fizi au shavu upande ambao jino au meno yanauma.

Njia za kuzuia kutoboka au kuoza kwa meno ni kupiga mswaki pamoja na dawa mara mbili kwa siku, hasa asubuhi na jioni.

Namna nyingine ni kuhakikisha unaondoa mabaki ya vyakula katikati ya meno kwa kutumia vijiti au uzi na hakikisha unakula mlo kamili.

Wataalamu wa kinywa pia wanashauri jamii kuepuka kuoza au kutoboka kwa meno kwa kupunguza ulaji wa vyakula vyenye sukari mara kwa mara na kujenga utamaduni wa kuhudhuria kituo cha afya kwa ajili ya uchunguzi angalau mara moja kwa mwaka.

Kuchunguza afya ya kinywa, hata kama huumwi ni njia ya kubaini mapema matatizo ya meno au fizi na kuchukua hatua kabla ya tatizo kujitokeza. Wataalamu husafisha kinywa kwa kutumia vifaa maalumu vya kuondoa uchafu na kufanya meno na fizi kuwa na afya njema.

Nini kinatokea kama jino likitoboka na kutotibiwa mapema? TANCDA inaeleza kuwa matibabu yasipofanyika mapema mhusika atahisi maumivu, ukakasi au ganzi unapokula vitu baridi au moto, jino linaweza kuvunjika, na hushindwa kutafuna vizuri chakula.

Matatizo mengine yanayoweza kujitokeza ni kutoka usaha kinywani, kutoa harufu mbaya na kupungua kwa ubora wa maisha.


Matatizo ya fizi

Nini maana ya ugonjwa wa fizi? TANCDA inaelezea ugonjwa wa fizi kuwa ni athari zinazotokea katika fizi, misuli na mfupa unaoshikilia jino kwenye taya.

Tafiti mbalimbali zilizofanywa nchini, TANCDA inasema zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wana matatizo ya fizi.

Mtu anaweza kujiuliza, nini kinachosababisha magonjwa ya fizi? TANCDA inaeleza kwenye taarifa yake ya uelimishaji jamii kuwa kutosafisha kinywa vizuri ni moja ya chanzo cha magonjwa ya fizi.

“Kutopiga mswaki kwa ufasaha husababisha kutengenezwa kwa utando mlaini ambao hujishikiza kwenye meno na hivyo kuruhusu vijidudu vya bakteria wanaoishi kwenye vinywa kutengeneza tindikali ambayo huathiri fizi,” inaeleza sehemu ya taarifa ya TANCDA.

Mambo mengine ambayo yanaweza kusababisha matatizo ya fizi ni uvutaji wa sigara, mabadiliko ya homoni kwa wanawake na magonjwa kama vile kisukari, Ukimwi na saratani.

Dalili za ugonjwa wa fizi ni kutokwa na harufu mbaya mdomoni, fizi kuvimba na kuonekana katika rangi nyekundu na maumivu au kutoka damu kwenye fizi.

Dalili nyingine ni kuhisi maumivu wakati wa kutafuna chakula, meno kulegea, meno kuwa na hisia ya ukakasi na sehemu ya mzizi wa jino kuonekana kutokana na fizi kuharibika.

Magonjwa ya fizi yasipotibiwa huweza kusababisha maumivu, meno kung’ooka yenyewe au kulazimika kuyaondoa na kupungua ubora wa maisha.

Kwa mama mjamzito akiwa na matatizo ya fizi anaweza kusababisha kujifungua mtoto mwenye uzito pungufu.

Ili kuepukana na magonjwa ya fizi ni kuhakikisha unapiga mswaki kwa usahihi mara mbili kwa siku; asubuhi na jioni kabla ya kulala, kuacha kutumia tumbaku na kusafisha meno kwa kutumia vijiti na uzi.


Makala haya yameandaliwa na Chama cha Waandishi Wanaokabili Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TJNCDF) kwa kushirikiana na Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania (TDA). Maoni na ushauri tuma TJNCDF, S.L.P. 13695, Dar es Salaam.








MWISHO


Posted by MROKI On Thursday, January 18, 2018 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo