Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepokea kwa masikitiko makubwa,
taarifa za kifo cha Mzee Edwin Isaac Mbiliewi Mtei, kilichotokea usiku wa
tarehe 19 Januari, 2026, jijini Arusha.
"Kwa niaba ya Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa niaba yangu binafsi, natuma salamu za
rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki, na wote walioguswa na msiba
huu," alisema Rais Dkt. Samia.
Rais Dkt. Samia alimkumbuka
Marehemu Mtei kama mmoja wa watumishi na viongozi wenye mchango mkubwa katika
ujenzi wa Taifa kwenye eneo la fedha, mipango na uchumi, aliyehudumu katika
nafasi mbalimbali ikiwemo Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (1966 -
1974), na kushiriki kuimarisha misingi ya uendeshaji wa Benki Kuu na uthabiti
wa mfumo wa fedha nchini.
Aidha, Rais Dkt. Samia alisema
Mzee Mtei ataenziwa katika historia ya siasa za vyama vingi kama miongoni mwa
waasisi wa demokrasia ya ushindani wa vyama, akitajwa kuwa ni miongoni mwa
waanzilishi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Aliongeza kuwa, mchango wa
Marehemu utaendelea kukumbukwa na kuenziwa na vizazi vya sasa na vijavyo,
hususan kupitia maandiko yake binafsi (autobigraphy) yanayoeleza safari yake ya
maisha na utumishi wake wa uongozi katika kuijenga Tanzania.
Rais Dkt. Samia anawaombea
faraja, nguvu na amani; familia, ndugu na wafiwa wote, na kumuomba Mwenyezi
Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi, Amina.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)





0 comments:
Post a Comment