Mwandishi wetu
UGOJWA wa kisukari hutokana na kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu kuliko inavyotakiwa. Sukari kwenye damu ikizidi viwango vya kawaida kwa muda mrefu husababisha madhara mengi mwilini.
Chama cha Ugonjwa wa Kisukari (TDA) katika taarifa yake juu ya “nini ufahamu kuhusu ugonjwa wa kisukari’ kinasema sukari mwilini hutokana na vyakula pamoja na vinywaji ambavyo mtu anavitumia kila siku na kazi yake kubwa ni kuupa mwili nguvu.
Athari za ugonjwa wa kisukari
Ugonjwa wa kisukari unasababisha athari nyingi mwilini. Miongoni ni pamoja na magonjwa ya moyo kuwa zaidi ya mara mbili zaidi ya watu wasio na ugonjwa huo.
Matatizo mengine ni shinikizo la damu, kiharusi, kuharibika mishipa ya damu na ile ya fahamu kiasi cha kusababisha ganzi, vidonda na hata gangirini ya miguu. Takwimu zinaonyesha kwamba ugonjwa wa kisukari ni moja ya sababu za watu wengi kukatwa miguu.
Ugonjwa wa kisukari pia husababisha kuharibika kwa figo na kuzifanya kushindwa kufanya kazi. Pia husababisha matatizo ya macho na upofu.
Madhara mengine ni kupungua kwa kinga ya mwili na kuuweka mwili katika hatari ya maambukizi ya ngozi, fizi, njia ya mkojo, uke na kifua kikuu. Vile vile unaweza kusababisha kupungua nguvu za kiume, utendaji wa kazi na kuathiri uchumi. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI
Dalili za Kisukari
Zipo dalili nyingi lakini miongoni ni kuhisi kiu mara kwa mara, kwenda haja ndogo mara kwa mara, kuwa dhaifu, uchovu kila wakati, kupungua uzito au kukonda.
Dalili nyingine ni kusikia njaa kila wakati, wanawake huwashwa sehemu za siri, kutoona vizuri, kupungua nguvu za kiume, ganzi, kuhisi kuchomwachomwa, miguu kuoza, vidonda na majeraha kutopona haraka na majipu mwilini.
Je, waweza kujikinga usiugue kisukari?
Jibu ni ndiyo. Tunaweza kujikinga na ugonjwa wa kisukari kwa kupunguza unene kwani unene hupunguza uwezo wa mwili kutumia sukari. Uzito wako usizidi urefu mara urefu mara 25.
Kwa mfano mtu mwenye urefu wa mita 1.63 uzito unatakiwa usizidi 1.63 x 1.63 x 25 = kilo 66. Urefu uwe kwa mita na uzito uwe kwa kilo.
Njia nyingine ni kujishughulisha mwili kwa kufanya chocchote kitakachokufanya utoke jasho au moyo kwenda mbio kwa angalau nusu saa kila siku, hata kama sii mnene.
Kujishughulisha ni kufanya jambo lolote la kutumia misuli mwilini, kwa mfano kutembea, kukuimbia, kufanya kazi za nyumbani, kulima, michezo mbalimbali, kucheza dansi, n.k. Kujishughulisha ni muhimu sana kwa matumizi ya sukari mwilini na afya kwa ujumla. Kukaa kwa muda mrefu bila kujishughulisha nako sii vizuri, inatakiwa usikae zaidi ya saa moja bila kujishughulisha, kwa angalau dakika mbili au tatu.
Njia nyingine ni kupunguza matumizi ya pombe au kuacha kabisa, kutotumia sigara au aina yoyote ya tumbaku na kuepuka misongo ya mawazo. Msongo wa mawazo ni kisababishi kikubwa cha kisukari na sukari kuzidi kuwa juu kwa walio na kisukari. Tunaweza kuepuka misongo mingi kwa kuwa wakweli kuhusu mahitaji yetu ya lazima, uwezo wetu na muda tulionao. Tuna haja ya kuamua ni kipi tuwaachie wengine au kushirikiana kwani mtu mmoja hawezi yote.
Njia ya mwisho lakini iliyo na umuhimu mkubwa ni kula chakula inavyotakiwa. Sehemu kadhaa za mwili hufanya kazi muda wote tangu kuzaliwa hadi kufa bila kupumzika. Viungo hivyo ni kama ubongo, mapafu, moyo na figo.
Nani anaugua kisukari
TDA inasema kwamba tafiti mbalimbali zilizofanywa hapa nchini na duniani zimebaini kuwa mtu yeyote anaweza kupata ugonjwa wa kisukari.
TDA inaeleza kuwa tafiti zilizofanywa hapa nchini zimebaini kwamba Watanzania tisa kwa kila 100 wenye umri wa miaka 25 na kuendelea wanaugua ugonjwa wa kisukari.
Mbaya zaidi, TDA inaeleza kuwa kati ya hao tisa ni wawili tu ambao wanajijua kuwa wanaugua kisukari. Wale wasiojijua huendelea kusishi na kisukari kwa muda mrefu na hugunduliwa baada ya ugonjwa kusababisha madhara makubwa mwilini yasiyofichika.
Hivyo watu wote wenye miaka 45 na kuendelea wanashauriwa kupima afya angalau mara moja kila mwaka ili kugundua kama wana kisukari au magonjwa mengine ambayo mwanzoni hayana dalili, kama vile msukomo wa juu wa damu, magonjwa ya moyo, na hata saratani.
Hadi sasa, TDA inasema ugonjwa wa kisukari hauna dawa ila mtu mwenye kisukari anaweza kuishi maisha marefu kama watu wengine ikiwa atafuata ushauri wa wataalamu jinsi ya kuuthibiti ugonjwa.
Makala haya yameandaliwa na Chama cha Waandishi Wanaokabili Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza (TJNCDF). Maoni na ushauri tuma S.L.P. 13695, Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment