Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masuala ya Nje
wa TBL Group, Georgia Mutagahywa, (kulia) na Mkurugenzi Mkazi
wa AMREF Health Afrika Tanzania Dk.Florence Temu. wakionyesha waandishi wa
habari (hawapo pichani) hati za mkataba wa makubaliano ya kuchimba
Kisima cha maji katika Wilaya ya Muleba mkoa wa Kagera.Hafla
ilifanyika katika Ofisi za AMREF jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkazi wa Amref Health Afrika Tanzania
Dk.Florence Temu (katikati) na Mtaalamu wa Maji,Afya na Usafi wa
Mazingira wa Amref Health Afrika- Tanzania Mhandisi Charles Mlingi (kushoto)
wakimsikiliza Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masuala ya Nje wa TBL Group, Georgia
Mutagahywa, (kulia) jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya
kusaini mkataba wa makubaliano na Amref Health Africa –Tanzania wa
kuchimba kisima cha maji katika Wilaya ya Muleba mkoa wa
Kagera.
Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masuala ya Nje wa TBL
Group, Georgia Mutagahywa, (kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa
habari (hawapo pichani) baada ya kusaini mkataba wa makubaliano na AMREF
Health Africa –Tanzania wa kuchimba visima virefu vya maji safi
katika Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.Kushoto ni Mkurugenzi
Mkazi wa AMREF Health Africa Tanzania Dk.Florence Temu.
************
KAMPUNI ya TBL Group imesaini mkataba mkataba na
Shirika lisilo la Kiserikali la AMREF Tanzania kwa ajili ya kuchimba
kisima cha maji chenye kina kirefu katika kijiji cha Busole Wilayani
Muleba,mradi wenye thamani ya zaidi ya milioni 67 ambao ukikamilika
utanufaisha wananchi wa kijiji hicho na vijiji jirani.
Akiongea wakati wa hafla ya kusaini mkataba huo
jijini Dar es Salaam jana,Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa TBL Group,Georgia
Mutagahywa alisema kuwa msaada huo ni utekelezaji wa moja ya sera ya
kampuni ya kutumia sehemu ya faida inayopata baada ya kulipa kodi kusaidia
huduma za kijamii.
Alisema kampuni imeingia ubia na AMREF
Tanzania katika utekelezaji wa mradi huu kwa kuwa ni moja ya taasisi ambao inao
utaalamu wa kutekeleza miradi ya maji vijijini ambayo imeonekana kunufaisha
jamii katika sehemu mbalimbali za nchini.
“Tunafurahi kushirikiana na AMREF katika mradi
huu unaotarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja,tuna uhakika
utawapunguzia wanawake adha ya kutembea mwendo mrefu kutafuta maji,kupunguza
utoro wa wasichana mashuleni pia utawezesha wakazi wa maeneo hayo kupata maji safi
na kupunguza uwezekano wa kupata maradhi yatokanayo na matumizi ya maji yasio
salama”.Alisema Mutagahywa.
Alisema TBL Group ikiwa kampuni
inayotegemea malighafi ya maji kwa asilimia kubwa katika viwanda vyake inaelewa
changamoto iliyopo ya upungufu wa maji katika sehemu mbalimbali na ndio maana
imekuwa ikisaidia kufanikisha miradi ya kuwapunguzia wananchi adha ya maji kwa
kusaidia kuwachimbia visima kama ambavyo imefanya katika mradi huu “Tunaelewa
tatizo la maji ni changamoto kubwa na tutaendelea kushirikiana na
serikali na wadau wengine kufanikisha miradi ya maji katika sehemu mbalimbali
nchini”.Alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa AMREF
Tanzania,Dk.Florence Temu,aliishukuru TBL Group kwa kuamua kushirikiana na
taasisi yake kutekeleza mradi wa maji wa kuboresha maisha ya wananchi wa wilaya
ya Muleba.
“Tunashukuru kushirikiana na TBL Group katika
mradi huu na tutahakikisha tunaufanikisha na unaleta manufaa kwa
wananchi kama ilivyokusudiwa kwa kuwa tunao utaalamu na uzoefu wa
muda mrefu wa kuendesha miradi ya uchimbaji wa visima vya maji katika maeneo ya
vijijini na tumefanikisha uazishwaji wa miradi shirikishi ya maji sehemu
mbalimbali vijijini”.Alisema Dk. Temu.
Aliongeza kuwa katika hatua ya awali
kampuni itafanya utafiti ili kubaini sehemu ya kuchimba kisima hicho na baada
ya kufanikisha zoezi na kuufanya mradi huo kuwa endelevu itatoa elimu kwa
wananchi ili wauone mradi huu kuwa ni wa kwao hata baada ya kukamilika.
0 comments:
Post a Comment