Mwenyekiti wa Jukwaa Huru la Wazalendo Ndugu Salum Ally Hapi akizungumza na waandishi wa habari kwenye hotel ya Travetine ,Magomeni jijini Dar es Salaam, kulia ni Katibu wa Jukwaa hilo Ndugu Mtela Mwampamba.
Ndugu wanahabari,
Mbele yenu sisi tuliowaita hapa ni Jukwaa Huru la Wazalendo ambalo
limeitisha mkutano huu ili kufikisha yale tuliyoyakusudia kuwaeleza umma wa
watanzania.
Sote tunatambua kuwa nchi yetu imetoka katika uchaguzi mkuu ambao umetupatia
viongozi wapya wa awamu ya tano ya uongozi wa taifa letu chini ya Dr. John
Pombe Joseph Magufuli. Tunapenda kuwapongeza watanzania wote kwa uchaguzi wa
amani na utulivu. Aidha kwakua ndio mara yetu ya kwanza kuzungumza nanyi
tunapenda kuwapongeza wanahabari wote kwa kazi nzuri ambayo mmekua mkiifanya
kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu nchini. Tunawashukuru sana.
Mkutano wetu huu umebeba madhumuni makubwa mawili.
Kwanza ni kumpongeza Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
hotuba yake aliyoitoa Bungeni siku ya ufunguzi wa Bunge la 11 la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 19/11/2015. Tunaiunga mkono Hotuba yake
ambayo kwa kweli ilikuwa imebeba Uzalendo, Ujasiri, dira ya kweli ya maendeleo
ya taifa letu na muuelekeo mpya wa Serikali ya awamu ya tano. Mambo yote
aliyozungumzia Mh. Rais yamebeba maslahi mapana ya nchi yetu na yanalenga
kuijenga Tanzania mpya ambayo waasisi wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere na Abeid Amani Karume walikusudia kuijenga.
Pili, pamoja na mambo mengi yaliyogusiwa na hotuba ya Mh. Rais, eneo la
kubana matumizi na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kwa Serikali ni
moja katika mambo ambayo Jukwaa hili limeamua kuyaunga mkono kwa vitendo.
Mh. Rais alitoa mchanganuo wa eneo moja tu la safari za nje na jinsi lilivyo
ligharimu Taifa mabilioni ya shilingi na kuahidi kuwa serikali ya awamu ya tano
chini ya uongozi wake itajikita katika kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.
Aidha Mh. Rais ameanza kutekeleza kwa vitendo ahadi yake hiyo ya kupunguza
matumizi yote yasiyo ya lazima Serikalini, ikiwemo hafla, warsha, makongamano
na safari za nje.
Jukwaa Huru la Wazalendo, linatambua kuwa kwa miaka kadhaa mbunge wa Kigoma
Mjini Mh. Zitto Kabwe amekuwa na msimamo wa kutokupokea posho za kitako tangu
akiwa mbunge wa Kigoma Kaskazini katika Bunge la 10. Pamoja na mh. Zitto,
Jukwaa pia limepokea taarifa za baadhi ya wabunge wa Bunge la 11 la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania walioamua kuunga mkono juhudi za Mh. Rais za kupunguza
matumizi yasiyo ya lazima serikalini kwa kukataa hadharani kupokea posho ya
kitako ya mbunge (sitting allowance).
Mnamo tarehe 23/11/2015, mbunge wa Singida Magharibi (CCM) Mh. Elibariki
Imanuel Kingu alimwandikia barua Katibu wa Bunge akieleza msimamo wake wa
kukataa kulipwa posho ya kitako ya Bunge (sitting allowance) katika kipindi
chote cha miaka mitano (2015 - 2020). Huyu anakuwa ni mbunge wa pili
baada ya Mh. Zitto Kabwe kutoka hadharani na kukataa posho ambazo msingi wake
ni unyonyaji wa wanyonge na ubadhirifu wa kodi za wananchi. SOMA ZAIDI BOFYA HAPA
Jukwaa linapenda kumpongeza Mh. Kingu Mbunge kwa ujasiri wake na Uzalendo
kwa Taifa lake, uliomfanya kuunga mkono juhudi za Mh. Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa vitendo.
Jukwaa linatambua ya kwamba, mapambano ambayo Mh. Kingu Mbunge ameyaanzisha
ni makubwa, magumu na yanahitaji kuungwa mkono na watanzania wote wanaoipenda
nchi yao bila kujali itikadi za vyama. Tunafahamu, wapo baadhi ya wabunge
wabinafsi na wasio na huruma na wanyonge wa Taifa letu ambao hawajafurahishwa
na hatua hii ya wabunge kama Zitto na Kingu ya kukataa posho ya kitako. Baadhi
ya wabunge wameanza kumpigia simu na kumtumia jumbe (sms) za vitisho mh.
Elibariki Kingu (MB) na wengine wakibeza kuwa anatafuta cheo.
Jukwaa linalaani hatua za wabunge hao wanaopinga nia njema ya Mh. Elibariki
Kingu na Mh. Zitto Kabwe kwa uamuzi wao wa kukataa posho za kinyonyaji na hivyo
basi, Jukwaa linawaomba wananchi wote majimboni, kuwataka wabunge wao
waliowachagua kueleza misimamo yao hadharani juu ya kuunga mkono hatua ya
kukataa posho kama njia ya kupunguza matumizi ya Serikali yasiyo ya lazima.
Jukwaa linafahamu ya kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye
mwenye mamlaka ya mwisho ya kuidhinisha masharti ya kazi za kibunge na stahiki
wanazopaswa kulipwa katika kazi hiyo.
Kwa heshima na unyenyekevu mkubwa, tunamuomba na kumshauri Mh. Rais John
Pombe Magufuli atakapokuwa anaidhinisha masharti na stahiki hizo, atusaidie
kuifuta kabisa posho ya kitako ya wabunge (sitting allowance).
Aidha, Jukwaa linamuomba mh. Rais kuzipitia na kutoa agizo la kufutwa kwa
posho zote zisizo za lazima zinazolipwa kwa watumishi wa umma wa kada
mbalimbali yakiwemo mashirika ya umma.
Jukwaa letu linatoa wito kwa wabunge wote bila kujali vyama vyao, kuungana
na Mh. Kingu(MB) na Mh. Zitto(MB) katika kukataa malipo ya posho ya kitako ili
kupunguza mzigo mkubwa ambao Serikali inaubeba kuhudumia wabunge. Fedha hizi ni
vyema zielekezwe katika kutatua kero za wananchi vijijini kama vile ukosefu wa
maji, madawati, vitanda vya Hospitali n.k.
Tunasisitiza kwamba, Ubunge ni Utumishi,na wala sio Utukufu. Kazi ya Mbunge
ni kuwawakilisha wananchi wake na si kuwanyonya. Tufike mahali kama Taifa tuwe
na nidhamu ya matumizi ya kodi za wananchi na mgawanyo sawa wa keki ya Taifa.
Kuendelea kulipana posho hizo ni ishara ya unyonyaji, dhuluma na kuongeza pengo
kati ya wenye nacho na wasionacho nchini. Jambo hili linakuza chuki na hasira
miongoni mwa wananchi wa hali ya kawaida dhidi ya viongozi wao na serikali kwa
ujumla.
Tunawaahidi kuwa Jukwaa litaendeleza harakati (movement) na vuguvugu hili
kwa kuanzia na Bunge kwasababu ndio wawakilishi wa wananchi. Tutaendelea kupaza
sauti zetu ili wabunge wengi zaidi Wazalendo wajitokeze na kukataaa posho hizi.
Tunajua kuwa wapo miongoni mwao wabunge wazalendo ambao wataguswa na wito huu
na kuuunga mkono hadharani.
Aidha tutaendelea kuwasemea kwa wananchi wabunge ambao bado hawataki kukataa
posho hizi bila kujali vyama vyao. Tunawaomba wananchi kote nchini kutuunga
mkono katika harakati hizi ili tuweze kuokoa mabilioni ya shilingi yanayopotea
kila Bunge linapokaa Dodoma kupitia posho ya kitako (sitting allowance).
Tutaandaa maandamano nchi nzima ya kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi
kuwashinikiza wabunge kukataa posho hizi. Makongamano na mdahalo mbalimbali
itaandaliwa na jukwaa ili kujenga uelewa wa pamoja wa wananchi na kuwa na sauti
moja katika kupinga posho za wabunge, watumishi wa serikali na mashirika ya
umma. Haya yatafanyika katika kufikia kusudio letu la kumuunga mkono Mheshimiwa
Rais katika hatua yake ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kwa Serikali.
Hatutaogopa wala kutishwa na yeyote katika kutekeleza jukumu hili zito.
Ahsanteni sana.
ALLY SALUM HAPI - MWENYEKITI
MTELA MWAMPAMBA - KATIBU
0 comments:
Post a Comment