Nafasi Ya Matangazo

August 10, 2026


Fundi Mussa Malale akielekeza jambo kwa msimamizi wake katika mradi wa ujenzi wa Uwanjha wa Ndege wa Kimataifa wa  Msalato Mkoani Dodoma.

Na Ssgt Mawazo Mtondo - DODOMA
Jeshi la Magereza linaendelea kutoa Programu mbalimbali za Urekebishaji kwa Wafungwa ili kuwapa ujuzi utakaowasaidia kujitegemea kwa kujiajiri au kuajiriwa pindi wamalizapo vifungo magerezani.

Magereza Tanzania Habari, tumefanya mahojiano na aliyekuwa mfungwa, Ndugu Mussa Malale, ambaye ni miongoni mwa wanufaika wa programu za urekebishaji zinazotekelezwa na Jeshi la Magereza.

Akizungumza katika mahojiano hayo, Ndg. Malale amesema kipindi chote alichokuwa gerezani alipewa mafunzo mbalimbali ya ufundi stadi, ikiwemo ufundi wa viyoyozi (Air Conditioning – AC), yaliyotolewa na wakufunzi wenye uzoefu na kumjengea ujuzi uliokuwa msingi wa mafanikio yake baada ya kumaliza kifungo.

Amesema baada ya kuachiliwa huru alianza kufanya kazi ya kuendesha gari la kubeba mchanga, lakini shughuli hiyo ilisimama baada ya gari kuharibika. Baadaye, rafiki yake alimshauri kutafuta kibarua katika mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege Mpya wa Msalato jijini Dodoma.

Malale, amesema alifanyiwa majaribio ya vitendo na kufanikiwa kuonesha uwezo wake, hatua iliyomwezesha kupata kibarua na kushiriki katika kazi za ufungaji wa viyoyozi katika mradi huo mkubwa, ambapo ametoa shukrani kwa Jeshi la Magereza kwa kumpatia ujuzi ambao hakuwa nao kabla ya kuingia gerezani.

Ushuhuda wa aliyekuwa Mfungwa, Ndg. Mussa Malale ni ushahidi wa mafanikio ya programu za urekebishaji zinazotekelezwa na Jeshi la Magereza, zinazowapa wafungwa elimu, mafunzo ya ufundi stadi na stadi za maisha zinazowawezesha kujitegemea, kupata ajira na kurejea katika jamii wakiwa raia wema wenye mchango chanya kwa maendeleo ya Taifa.

Usikose kufuatilia kampeni ya "MAGEREZA NURU YA MABADILIKO" kupitia kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na TBC kila siku kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 3:00 asubuhi, ili upate simulizi na ushuhuda wa mafanikio ya shughuli za urekebishaji zinazotekelezwa na Jeshi la Magereza.
Posted by MROKI On Monday, August 10, 2026 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo