Katika maisha ya kawaida ya mwanadamu, kuna kuweka malengo ili kufikia mafanikio. Inapotokea malengo yametimia, moyo hujaa furaha kwani mlango wa kufanikiwa unakuwa umefunguka.
Haya ndiyo yaliyotokea kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Kwa TRA, mwaka wa fedha 2026/2027 umeanza vizuri. Hii ni kufuatia Mamlaka hiyo kukusanya shilingi trilioni 3.245 kwa mwezi Julai, 2026, ambapo makusanyo hayo ni sawa na asilimia 109 ya lengo la kukusanya trilioni 2.971 kwa mwezi huo.
Ni kwamba; mwaka mpya wa fedha huanza Julai 1 ya kila mwaka. Hivyo mwezi wa kwanza wa mwaka mpya wa fedha ni kuanzia Julai 1 hadi 31. Kwa malengo ambayo TRA ilijiwekea, ni kukusanya shilingi trilioni 2.971, lakini lengo hilo limetimia na kuzidi, ambapo zimekusanywa shilingi trilioni 3.245.
Kimsingi, bajeti iliyopitishwa na bunge kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ni shilingi trilioni 62.33, ambapo asilimia 74 ya fedha hizo zinategemewa kukusanywa kupitia mapato ya ndani (own sources).
Katika fedha hizo, TRA inawajibika kukusanya shilingi trilioni 41.08, sawa na asilimia 67 ya bajeti nzima katika kipindi cha Julai 1, 2026 hadi Juni 30, 2027.
Akiwa katika hafla ya Uwekezaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya TRA, Kizimkazi, Zanzibar, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Omar, ameipongeza TRA kwa kufanikiwa kukusanya shilingi trilioni 3.245 kwa mwezi Julai, 2026.
Naye, Kamishna Mkuu wa TRA, CPA Yusuph Mwenda, amesema wanaendelea kuwahudumia vyema walipakodi na kutatua changamoto zao ili Mamlaka ifanikishe malengo.
"Kutokana na usimamizi wako mzuri Mheshimiwa Waziri wa Fedha na ushirikiano na walipakodi, tunakuhakikishia tutavuka lengo hilo na kupitia, ishara inaonyesha kwamba tumeanza mwaka wa fedha kwa nguvu kubwa na tuna imani tutafikia na kuvuka malengo tuliyowekewa," amesema CPA Mwenda.
MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA SAFARI YA UKUSANYAJI MAPATO WENYE TIJA
Mosi, kufanya malipo kwa njia za kieletroniki. Moja ya mabadiliko ya sheria za kodi ni pamoja na kuhimiza malipo ya kieletroniki ili kuendana na uchumi wa kidijitali unaoachana na matumizi ya fedha taslimu (cashless economy). Ni muhimu kufanya malipo kwa njia za kieletroniki kama simu na benki.
Pili, kudai na kutoa risiti halali ya kieletroniki. Ni muhimu kwa mnunuaji kudai risiti pale anapofanya malipo na muuzaji nae atoe risiti halali ya kieletroniki (EFD), ili serikali ipate kodi yake halali. Mmoja kati ya hawa wawili au wote wawili wasipotimiza wajibu wao, serikali itakosa mapato, na hivyo kushindwa kutimiza kikamilifu malengo ya kuwahudumia wananchi.
Tatu, kuwa waaminifu katika kurekodi taarifa za mauzo. Muuzaji anapaswa kuandika taarifa sahihi za mauzo ili Mamlaka iwe na taarifa sahihi za mwelekeo wa biashara au shughuli za uzalishaji zinazofanyika. Kwa mabadiliko ya sheria za kodi yaliyofanyika, udanganyifu katika uandishi wa taarifa za mauzo, adhabu yake ni mhusika kulipa mara mbili ya kiwango kilichofanyiwa udanganyifu.
Nne, kuboresha uhusiano baina ya walipakodi na TRA. Pamoja na mafanikio katika eneo la uhusiano, bado suala hili linapaswa kuhimizwa kwani walipakodi ndiyo waliobeba hatma ya maendeleo ya nchi yetu. Namna yeyote ya kuwapuuza, ni kuikosesha serikali mapato na kuua shughuli zao za uzalishaji ambazo zinachangia kutoa ajira na kuongeza mapato ya nchi.
Tano, kutoa makadirio ya kodi yanayoendana na kiwango cha biashara. Wakati mwingine, mfanyabiashara anaweza kufunga baishara pale anapokadiriwa kiwango kikubwa zaidi ya uwezo wa biashara yake. Hivyo basi, ukadiriaji kodi unapaswa kumwezesha mfanyabiashara kukua na si kumrudisha nyuma.
Sita, ajenda ya kujitegemea iwe ni ajenda ya kitaifa na si ya viongozi. Mwelekeo wa serikali ni kujitegemea kibajeti. Ajenda hii imefungamanishwa na ulipaji kodi wa hiari na wa kizalendo. Katika safari ya maendeleo ya nchi yetu wananchi na walipakodi kwa ujumla, tuone fahari kulipa kodi kwani kodi hizo ndizo zitakazotujengea heshima ya kujitegemea na kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ya kimkakati nchini.
Saba, kutoa elimu endelevu ya kodi kwa walipakodi na wananchi. Elimu ya kodi izidi kutolewa ikizingatiwa serikali imefanya mabadiliko makubwa ya sheria za kodi. Elimu ya kodi itolewe kwa wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo. Klabu za kodi ziimarishwe katika taasisi za elimu nchini. Pia, elimu hiyo itolewe sehemu za wazi kama sokoni, vituo vya mabasi ili kujenga uelewa mkubwa kwa wananchi. Pia, TRA iwafuate wafanyabiashara kule walipo kuwapa elimu ya kodi.
Ni faraja kuona mwaka mpya wa fedha umeanza kwa kishindo cha makusanyo yaliyozidi malengo yaliyowekwa. Nchi yetu itaendelea kupiga hatua kubwa za maendeleo endapo wananchi tutalipa kodi kwa uaminifu. Hakuna mwingine wa kutuletea maendeleo katika nchi yetu - ni sisi wenyewe tunawajibika, hivyo kodi zetu zitaamua maendeleo yetu.
Mungu Ibariki Tanzania.
0620800462.







0 comments:
Post a Comment