Rais wa Jamhuri ya Malawi,
Mheshimiwa Joyce Banda (pichani kulia) amemwelezea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kama mwanademokrasia na kiongozi hodari
anayepigania amani na utawala bora.
Aidha, Rais Banda amewaelezea
wanawake maarufu wa Tanzania, Mama Gertude Mongella na Dkt. Asha Rose Mingiro
kama baadhi ya matunda ya juhudi za Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC) kuleta usawa wa kijinsia katika eneo la Kusini mwa Afrika.
Rais Banda ametoa sifa hizo
kwa Rais Kikwete na Watanzania hao wawili leo, Jumamosi, Agosti 17, 2013 wakati
alipozungumza kwenye hotuba ya kupokea uongozi wa SADC kwenye Ufunguzi wa
Mkutano wa Mwaka wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa SADC kwenye Kituo cha Mikutano
cha Bingu wa Mutharika mjini Lilongwe, mji mkuu wa Malawi. Mkutano huo wa 33 wa
wakuu wa nchi SADC ni wa siku mbili.
Akizungumza baada ya kuwa
amepokea Uenyekiti wa SADC kutoka kwa Rais Armando Emilio Guebuza wa
Mozambique, Rais Banda amesema kuwa uongozi wa Rais Kikwete wa Asasi ya Siasa,
Ulinzi na Usalama ya SADC umethibitisha na kuonyesha dhahiri kuwa kiongozi huyo
wa Tanzania ni mwanademokrasia anayepigania amani na utawala bora wakati wote.
“Wakati wa uongozi wake wa
SADC-Troika, Rais Kikwete amejihusisha kwa karibu sana na ujenzi na utetezi wa
demokrasia, utafutaji amani na jitihada za kuongeza kiwango cha utawala bora
katika eneo letu la Afrika,” Mama Banda amewaambia mamia ya wasikilizaji kwenye
ukumbi huo wa Bingu wa Mutharika.
Kuhusu Mama Mongella na Dkt.
Asha Rose Mingiro, Rais Banda amesema kuwa Watanzania hao wawili ni sehemu ya
wanawake kadhaa katika eneo la SDAC ambao wamefanikiwa kupata nafasi kubwa za
uongozi kipindi ambako SADC imeelekeza
nguvu zake katika kuleta usawa wa kijinsia.
Wakati wa uongozi wake wa
SADC-Troika, Rais Kikwete amejihusisha sana na kutafuta suluhu na utatuzi wa
migogoro ya kisiasa katika nchi za Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
(DRC) na Madagascar.
Rais Kikwete amemaliza muda
wake wa uongozi wa Troika leo na nafasi yake inachukuliwa na Rais Hifikepunye Phohamba
wa Namibia.
Mbali na Marais Kikwete, Banda
na Guebuza, viongozi wengine ambao wamehudhuria mkutano na shughuli za leo ni
pamoja na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe,
Rais Joseph Kabila Kabange wa DRC, Rais Khama Ian Khama wa Botswana, Dkt. Tom
Thabane ambaye ni Waziri Mkuu wa Lesotho, Waziri Mkuu wa Mauritius na Makamu wa
Rais wa Zambia, Mheshimiwa guy Scott.
Jumla ya nchi 14
zinawakilishwa katika Mkutano wa mwaka huu wa wakuu wa nchi wanachama wa SADC
kati ya nchi 15 wanachama wa Jumuia hiyo. Madagascar haishiriki Mkutano huo kwa
sababu ya kusimamishwa uanachama kwa sababu ya mgogoro wa kisiasa nchini humo.
0 comments:
Post a Comment