1)
Kutokana na kutokuwepo na taarifa sahihi kuhusu deni
la Taifa kuna umuhimu wa kukutanisha wadau wakuu wanaohusika hususani BOT,
HAZINA, Kamati za Bunge na CAG ili kuweza kujua kwa usahihi zaidi ukubwa wa
deni hilo. Vile vile imeamuliwa kuwa
Serikali ishauriwe kuunda chombo huru kitakachosimamia deni la taifa.
2)
Baada ya kuanzisha mfumo mpya wa bajeti ya Serikali
mwaka huu kuna umuhimu wa kuandaa mkutano wa kutathimini mafanikio na
changamoto za mfumo huu na kujadili mambo ya kuboresha zaidi mfumo mzuri wa
bajeti ya Serikali.
3)
Kamati za Bunge zinazoshughulikia usimamizi wa fedha
na rasilimali za taifa zishughulikie zaidi Maafisa Masuuli hatarishi (risk
based) ili kuleta thamani ya fedha katika utendaji wao. Kamati zishirikiane na CAG katika kuamua ni
Afisa Masuuli yupi aitwe kukutana na Kamati.
4)
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na
Bunge na TAMISEMI waanzishe utaratibu wa kuratibu mikutano na mafunzo ya
Wakurugenzi wa Halmashauri kwa pamoja kuliko kila Wizara kuwaita watendaji hao
katika sehemu mbalimbali kwa muda tofauti na kuwafanya kutokuwepo ofisini kwa
kipindi kirefu.
5)
Mfumo wa kutunza kumbukumbu za hesabu na nyaraka
mbalimbali katika Serikali Kuu na Halmashauri uboreshwe ili zinapohitajika
zipatikane kwa wakati muafaka bila kisingizio cha aina yoyote.
6)
Kuhusu ukaguzi wa ufanisi CAG asisubiri mpaka asikie
malalamiko kutoka kwa wananchi au kwenye magazeti bali akague mara kwa mara
sehemu zote zenye matatizo.
7)
Taarifa za mwaka za Kamati za Bunge ziwe na kipengele
cha kiwango cha utekelezaji wa mapendekezo ya Kamati yaliyotolewa awali. Kamati
ziwezeshwe kifedha ili ziweze kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo yao. Kanuni
za Bunge zieleze utaratibu wa ufuatiliaji wa Maazimio ya Bunge na namna
utekelezaji wake utavyowasilishwa Bungeni.
Vile vile Bunge litenge siku ya kujadili Serikali ilivyoshughulikia hoja
za Kamati za Bunge. Spika ashauriwe
kuhusu umuhimu wa kuunda Kamati ya Bunge ya kufuatilia ahadi za Serikali.
8)
Mikataba katika ngazi ya Serikali za Mitaa iandikwe
kwa lugha ya Kiswahili.
9)
Serikali inatakiwa kufanya jitihada za ziada kuzalisha
wataalam wa fani ya manunuzi. Kuna
umuhimu wa PPRA kuongezewa nguvu za ziada za kiutendaji ikiwa ni pamoja na
fedha na wafanyakazi.
10) Bajeti
ya Bunge iongezwe kupitia Mfuko wa Bunge na iwasilishwe Bungeni na Naibu Spika
na sio Ofisi ya Waziri Mkuu.
11) Serikali
iandae mjadala wa kitaifa wa kutafuta ufumbuzi wa kukabiliana na vitendo vya
rushwa na mmomonyoko wa maadili vinavyoongezeka kwa kasi hapa nchini. Vilevile
viongozi wa umma na watendaji waongoze kwa mfano kwa kutojihusisha na vitendo
vya rushwa katika kutekeleza majukumu yao.
12) Sheria
ya Maadili ya Viongozi wa Umma haiweki uwazi wa kutangaza umiliki wa mali za
viongozi. Hii inapelekea viongozi
kutoweka wazi mali wanazomiliki na ni rahisi mtu kuzushiwa umiliki usio wa
ukweli. Ni vyema Sekretarieti wakafanya
utafiti wa umiliki wa mali kwa viongozi wa Umma na kuweka taarifa hizo katika
tovuti ya Sekretariati ili kuwawezesha wananchi kuweza kuona mali
zinazomilikiwa na viongozi wao; na pale ambapo kiongozi hatakuwa ametoa taarifa
ya umiliki huo basi taarifa hiyo itolewe kwa Tume.
13) Kwa
kuwa leseni za udereva za sasa zinaweza kuweka kumbukumbu za makosa ya usalama
barabarani, basi TRA ikishirikiana na
Wizara ya Mambo ya Ndani zihakikishe ya kuwa Askari wa Usalama
Barabarani wanatumia utaratibu huu wa kisasa wa kutoa “notification” na kutoa risiti za malipo za
elektroniki.
14) Maduhuli
ya Serikali sasa yakusanywe kwa kutumia risiti za elektroniki. Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika
ya Umma yaanze kutumia risiti za eletroniki mara moja ili kudhibiti upotevu wa
mapato ya serikali yanayotokea hivi sasa katika kutumia risiti zinazoandikwa
kwa mkono. Pia ofisi za serikali zifanye manunuzi yake kwa wafanyabiashara
wanaotumia mashine za kielektroniki.
15) TRA
ihamasishe wananchi na wafanya biashara umuhimu wa matumizi ya risiti za
elektroniki, wafanyabiashara waelimishwe umuhimu wa kutoa risiti hizo na
wananchi waelimishwe umuhimu wa kudai risiti kila wanapofanya manunuzi. Elimu
na uhamasishaji huo unaweza kufanywa kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo
sanaa, timu za michezo, bendi za muziki, redio, TV, mbao za matangazo n.k.
16) Serikali
idhibiti makampuni ya uwakala wa kupakia na kupakua mizigo (clearing and forwarding) yaliyopo
Bandarini ili kudhibiti mapato ya forodha.
17) Sheria
ya “Anti Money Laundering” ya 2006
irekebishwe ili iweke viwango vya fedha ambazo mtu anaweza kuingia au kutoka
nazo nchini bila kuzitaja (declare).
Kuna umuhimu wa Waziri wa Fedha kutengeneza kanuni za kutekeleza Sheria hiyo.
18) Benki
Kuu iandae mfumo thabiti wa usimamizi wa Maduka ya Fedha (Foreign Bureau de
Change), na kuhakikisha kutungwa kwa sheria inayozuia matumizi ya fedha za
kigeni katika shughuli za kibiashara hapa nchini.
19) “The Proceeds of Crime Act, 1991”
ifanyiwe marekebisho na kuweka kifungu kinachomwezesha AG/DPP kuwa na mamlaka
ya kuomba mahakama kufungua kesi ya madai (Civil Forfeiture) kwa watu
wanaotuhumiwa kwa ufisadi.
20) Imesisitizwa
kwamba CAG akague misamaha ya kodi na kuweka taarifa hiyo kwenye taarifa za
kila mwaka.
21) Serikali
iimarishe Taasisi zinazoshughulikia maadili utawala bora na uwajibikaji kama
vile Sekretariati ya Maadili ya Viongozi, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala
Bora, Takukuru, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Tume ya Utumishi
wa Mahakama, Kamati ya Maadili ya Bunge ili ziweze kufanya kazi zake kwa mujibu
wa sheria na kanuni zilizoanzisha Taasisi hizo.
22) PCCB
na vyombo vingine vinavyohusiana na kushughulikia masuala ya jinai wawe
waalikwa kwenye vikao vya Kamati za Bunge ili waweze kutoa ushauri kwenye
kamati hizo.
0 comments:
Post a Comment