JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA FEDHA
Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo akiwa na mkoba wa Bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2011/2012
HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA, MHESHIMIWA MUSTAFA HAIDI MKULO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA SERIKALI KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2011/2012
UTANGULIZI:
1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kujadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2012. Pamoja na hotuba hii, vipo vitabu vinne vinavyoelezea kwa kina takwimu mbalimbali za Bajeti. Kitabu cha Kwanza kinahusu makisio ya mapato. Kitabu cha Pili kinaelezea makisio ya matumizi ya kawaida kwa Wizara na Idara zinazojitegemea ambapo cha Tatu kinahusu makisio ya matumizi ya kawaida kwa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na cha Nne kinaelezea makadirio ya matumizi ya maendeleo kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Mikoa pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2011 ambao ni sehemu ya Bajeti hii.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuchaguliwa tena kuongoza kwa muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Nne. Aidha, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa imani kubwa aliyonayo kwangu kwa kunichagua kwa mara nyingine tena kuongoza Wizara kubwa na nyeti, ninamuahidi kuwa sitamuangusha. Pia ninampongeza Dkt. Mohammed Gharib Billal kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vile vile,
ninampongeza Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb.) kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge na kuteuliwa tena na hatimaye kupitishwa na Waheshimiwa Wabunge kuwa Waziri Mkuu kwa muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Nne.
3. Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza wewe binafsi Mhe. Spika Anne Makinda (Mb.) kwa kuchaguliwa kuwa Spika na hivyo kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza Bunge katika Afrika Mashariki. Kuchaguliwa kwako kunatokana na imani kubwa waliyonayo Waheshimiwa Wabunge kwa kuzingatia busara zako, uwezo na uzoefu wako ndani ya Bunge hili. Napenda pia kumpongeza Mhe. Job Ndugai (Mb.) kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika. Nawapongeza pia mawaziri wenzangu wote pamoja na Naibu mawaziri wote, kwa kuteuliwa kwao na Mhe. Rais kushika nyadhifa hizo. Aidha, napenda niwapongeze wabunge wote kwa kuchaguliwa na kuteuliwa kuingia katika Bunge hili.
4. Mheshimiwa Spika, naomba pia nichukue fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa wale wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha matayarisho ya Bajeti hii. Maandalizi ya Bajeti ya Serikali yanahusisha wadau na vyombo mbalimbali. Kipekee ninaishukuru Kamati ya Fedha na Uchumi chini ya uenyekiti wa Mhe. Dkt. Abdallah Omari Kigoda, Mbunge wa Handeni, pamoja na kamati nyingine za kisekta kwa ushauri mzuri waliotoa wakati wakichambua mapendekezo ya Bajeti hii.
5. Mheshimiwa Spika, naomba niishukuru kwa namna ya pekee Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2011 na nyaraka mbalimbali za sheria ambazo ni sehemu ya bajeti hii. Kwa upande wa Wizara ya Fedha, nawashukuru Naibu Mawaziri, Mhe. Gregory Teu (Mb) na Mhe. Pereira Ame Silima (Mb). Namshukuru Katibu Mkuu Ndugu Ramadhani M. Khijjah na Naibu Makatibu Wakuu, Ndugu Laston T. Msongole, Dkt. Servacius B. Likwelile na Ndugu Elizabeth Nyambibo. Napenda kuwashukuru Prof. Benno Ndulu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Ndugu Harry Kitilya, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania na Dkt. Albina Chuwa, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa. Aidha, napenda kuwashukuru Wakuu wa Idara na wafanyakazi wote wa Wizara ya Fedha. Vile vile, namshukuru Mpigachapa Mkuu wa Serikali kwa kuchapisha Hotuba hii kwa wakati. Mwisho, nawashukuru wataalamu na wale wote waliotoa mapendekezo kuhusu sera, mikakati na masuala mbalimbali ya kodi ambayo yamezingatiwa katika kuandaa Bajeti hii.
6. Mheshimiwa Spika, huu ni mkutano wa kwanza wa Bajeti kwa Bunge hili baada ya uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge uliofanyika mwezi Oktoba mwaka 2010 na kukirejesha Chama Cha Mapinduzi pamoja na Serikali yake katika kipindi cha pili cha Awamu ya Nne. Wananchi wana matumaini makubwa kwa Bunge hili kwamba litasaidia kuongeza kasi ya kuwapatia maendeleo na kuondokana na umasikini wa kipato unaowakabili wananchi walio wengi. Hili linajidhihirisha kwa uwepo wa Waheshimiwa Wabunge wenye umri, jinsia, elimu, na uzoefu mbalimbali. Ni matumaini ya Serikali kuwa uwepo huo wa Waheshimiwa Wabunge utakuwa ni chachu katika kuwaletea maendeleo wananchi kwa ari zaidi, kasi zaidi na nguvu zaidi.
7. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka wa fedha unaoishia 2010/2011, imeendelea kutumika kama chombo muhimu katika kutekeleza Sera na Malengo ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii. Katika kipindi hiki, yamekuwepo mafanikio ya kuridhisha katika kutoa huduma bora kwa wananchi na kuimarisha miundombinu ili kuwezesha kukua kwa uchumi na kupunguza umaskini.
8. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2011/12 itazingatia vipaumbele vifuatavyo:
i) Umeme;
ii) Maji;
iii) Miundombinu ya usafiri na usafirishaji (reli, bandari, barabara, viwanja vya ndege, Mkongo wa Taifa);
iv) Kilimo na umwagiliaji; na
v) Kupanua ajira kwa sekta binafsi na ya umma.
Bajeti itahakikisha pia kuwa mafanikio yaliyopatikana katika sekta za elimu na afya yanalindwa pamoja na kuimarisha ubora wa huduma zinazotolewa.
Mikakati ya Kupunguza Makali ya Maisha kwa Mwananchi
9. Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto zinazowakabili wananchi katika kupambana na makali ya maisha. Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2011/12, pamoja na mambo mengine, inalenga katika kuchukua hatua za kurekebisha hali hiyo. Kumekuwepo na changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji hatua za makusudi kuchukuliwa na wadau mbalimbali ikiwemo Serikali, sekta binafsi na mwananchi mmoja mmoja ili kupunguza makali ya maisha kwa mwananchi. Hatua zitachukuliwa maeneo yafuatazo:-:
i) Kasi ya kupanda kwa bei za bidhaa na huduma: Kasi ya ongezeko la bei za bidhaa na huduma nchini pamoja na mambo mengine inasababishwa na: kuongezeka kwa bei za mafuta katika soko la dunia; kutopatikana kwa umeme wa uhakika na hivyo kuathiri uzalishaji; na upungufu wa chakula nchini na nchi jirani. Serikali itachukua hatua mbalimbali kukabiliana na hali hiyo kama ifuatavyo:
a) Ongezeko la bei za mafuta ya petroli: Ongezeko la bei za mafuta ya petroli linatokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa bei katika soko la dunia. Kwa mfano baada ya msukosuko wa uchumi duniani bei ya mafuta ilishuka hadi Dola za Kimarekani 40 kwa pipa. Kwa sasa bei ya mafuta katika soko la dunia imefikia takribani Dola 120 kwa pipa ambayo ni mara tatu ya bei iliyokuwepo awali. Aidha, ongezeko la bei linachangiwa pia na kuongezeka kwa gharama za bima ya mizigo kwa meli zinazoleta mizigo nchini kutokana na tishio la maharamia baharini, uagizaji wa mafuta wa kampuni moja moja na migogoro ya kisiasa katika nchi za Mashariki ya Kati na kaskazini mwa bara la Afrika. Pamoja na sababu zilizotajwa, bidhaa ya mafuta ya petroli inapoingia hapa nchini hutozwa ushuru wa bidhaa (excise duty) na ushuru wa mafuta (fuel levy). Zipo pia tozo mbalimbali zinazotozwa na Mamlaka zinazotoa huduma katika mfumo wa uagizaji na upokeaji wa mafuta. Taasisi zinazotoza tozo hizo ni pamoja na EWURA, SUMATRA, Shirika la Viwango la Taifa (TBS), Kiwanda cha TIPER, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Mamlaka ya Bandari na makampuni yanayoagiza mafuta. Pamoja na hatua zilizochukuliwa na Serikali za kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani na kuweka viwango maalum vya ushuru wa bidhaa kwenye mafuta, bado bei ya mafuta imeendelea kuwa kubwa na kuongeza gharama za maisha.
Mheshimiwa Spika, ili kupunguza makali ya ongezeko la bei ya mafuta nchini, Serikali imeamua kufanya mapitio ya namna ya kukokotoa tozo zinazotozwa na Mamlaka mbalimbali kwa lengo la kuzipunguza na zoezi hili litakamilika katika mwaka wa fedha 2011/12. Aidha, Serikali pia inakamilisha taratibu za ununuzi wa mafuta kwa wingi kwa lengo la kuyauzia makampuni ya usambazaji kwa bei ya jumla. Kanuni zitakazotoa mwongozo katika uagizaji mafuta kwa pamoja zimekamilika na utaratibu huu unategemewa kuanza katika mwaka wa fedha 2011/12. Utaratibu huu unatarajiwa kupunguza bei na gharama za usafirishaji wa mafuta hayo. Pamoja na juhudi hizi za Serikali, sekta binafsi inahimizwa kuwezesha upatikanaji wa huduma ya kutumia gesi kama nishati mbadala wa mafuta ya petroli hasa mijini. Ni matarajio yangu kwamba hatua hizi zitaleta unafuu wa bei ya mafuta hapa nchini na hivyo kupunguza gharama za maisha kwa wananchi na kuboresha uchumi kwa ujumla.
b) Upungufu wa Nishati ya umeme: Nchi yetu inakabiliwa na upungufu wa nishati ya umeme kutokana na kiwango kidogo cha uzalishaji usioendana na mahitaji. Kwa kuzingatia kuwa umeme una umuhimu wa kipekee katika kukuza uchumi wa nchi, Serikali itachukua hatua kadhaa za kukabiliana na upungufu huu, ikiwemo kukamilisha mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 100 Dar es Salaam na ule wa megawati 60 Mwanza; kuiwezesha TANESCO kupata mikopo kutoka taasisi za fedha za kimataifa kwa ajili ya kununulia mitambo ya uzalishaji na kuangalia upya namna ya kugawanya shughuli za Uzalishaji, Usafirishaji na Usambazaji; kwa lengo la kuiachia TANESCO kujikita kwenye eneo ambalo ina uwezo nalo kiushindani na hivyo kuleta ufanisi katika sekta nzima ya umeme. Aidha, kutokana na kukamilishwa kwa sera, sheria na kanuni za ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP), Serikali itaandaa utaratibu wa kuhusisha sekta binafsi katika sekta ya umeme na inatarajiwa kwamba baadhi ya miradi ya uzalishaji umeme itatekelezwa kwa njia ya ubia kati ya Serikali na sekta binafsi. Serikali imeshaanza majadiliano na wawekezaji katika uzalishaji wa umeme kwa ubia katika miradi ifuatayo; Mtwara MW 300, Mpanga MW 144, na miradi ya usafirishaji umeme wa kV 400 ya Morogoro-Tanga-Kilimanjaro-Arusha km 682 na upanuzi wa Gridi ya Kaskazini Magharibi kwa mikoa ya Kagera, Kigoma na Rukwa - km 1000. Serikali inawashauri wananchi kuanza kutumia vyanzo mbadala vya umeme wa jua, upepo na nishati inayotokana na biogesi pamoja na kutumia kwa uangalifu nishati ya umeme iliyopo.
c) Kuimarisha Hifadhi ya Chakula: Kutokana na kuendelea kuwepo kwa upungufu wa chakula kulikosababishwa na ukame katika baadhi ya maeneo ya nchi, Serikali itaendelea kuimarisha hifadhi ya chakula kwa kuongeza ununuzi wa mazao ya chakula katika Wakala wa Hifadhi ya Chakula ya Serikali (NFRA). Aidha, hifadhi hiyo itatumika kupunguza bei ya chakula nchini kwa kusambaza nafaka kwa bei nafuu katika masoko wakati wa uhaba. Kadhalika, wananchi wanashauriwa kuendelea kulima mazao yanayohimili ukame pamoja na kilimo cha umwagiliaji na kuzingatia kuweka akiba ya chakula cha kutosha.
ii) Kuongeza Ajira: Mheshimiwa Spika, Ukosefu wa ajira, hasa kwa vijana umeendelea kuwa ni changamoto kubwa, hivyo, Serikali inafanya juhudi za makusudi kupanua ajira katika maeneo mbalimbali kama ifuatavyo:-
a) Mpango wa Ukanda wa Kilimo wa Kusini mwa Tanzania (Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania-SAGCOT). Mpango huu ni mkakati wa kuleta mapinduzi ya kilimo ambao utatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na na wadau mbalimbali wa kilimo, wakiwemo washirika wa maendeleo. Utekelezaji wa Mpango huu ambao ni sehemu ya Kilimo Kwanza, utasaidia kupunguza umaskini miongoni mwa wananchi wanaoishi vijijini kwa kuwaongezea mavuno ya mazao yao na kukuza ajira miongoni mwa Watanzania. Katika mwaka 2011/12 Benki ya Dunia inatarajia kuchangia Dola za Kimarekani milioni 60 sawa na shilingi bilioni 92.8. Tunakamilisha taratibu za kupata fedha hizo na tutawasilisha Bungeni kwa ajili ya kuidhinisha matumizi yake.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia itaendelea kufanya maboresho ya kilimo cha mazao, ufugaji na uvuvi. Kwa upande wa mazao, Tanzania ina mabonde mazuri yenye rutuba kwa kilimo cha mpunga katika mikoa ya Tabora, Mwanza, Shinyanga, Kigoma, Pwani, Mbeya, Kilimanjaro, Tanga na Morogoro. Chini ya utaratibu huu, wakulima wadogo wadogo watawezeshwa kupata huduma za mikopo, ugani, mbegu bora na mbolea. Utafiti unaonesha kuwa kwa kutumia vizuri mabonde hayo, pembejeo na tija katika uzalishaji, inawezekana kutoa fursa za ajira mchanganyiko.
b) Viwanda vya kusindika mazao ya kilimo vitasaidia kuongeza thamani ya mazao na ajira. Aidha, eneo jingine la kuongeza ajira ni kupitia mwingiliano (linkage) baina ya viwanda vya nguo na sekta ya kilimo. Juhudi zinazoendelea za kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme kwa kutumia vyanzo mbadala vya umeme wa maji na mafuta ambavyo ni upepo, jua na biogesi, zitasaidia kufanikisha mpango wa uzalishaji wa bidhaa viwandani. Kadhalika, Serikali itaboresha mazingira ya sekta ya viwanda (vikubwa, vidogo na vya kati), ili kuviwezesha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
c) Kuongeza kasi ya utekelezaji wa MKURABITA, ili mpango huu uweze kuchangia ongezeko la ajira. Serikali kwa kushirikiana na AZAKI, AZISE na wadau wengine, itaendelea kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs), ili kuongeza ajira. SIDO, VETA na vyuo vya maendeleo ya wananchi na vijana vitaboreshwa zaidi ili visaidie kutoa mafunzo ya ujasiriamali ambayo yataongeza ajira. Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kuwawezesha waombaji wa mikopo kwa kutumia dhamana ya Serikali kupitia mifuko iliyo chini ya Benki Kuu na kupitia benki zao za biashara kupata mikopo kwa ajili ya shughuli zao za uzalishaji. Utaratibu huu umenufaisha wajasiriamali wengi ikiwa ni pamoja na vyama vya ushirika na sekta binafsi.
d) Kuharakisha maboresho yanayoendelea katika sekta ya fedha na utekelezaji wa sera ya uwezeshaji ambazo zitasaidia upatikanaji wa mikopo kwa wananchi ili waweze kupata mitaji na kujiajiri. Hatua zinazochukuliwa na Serikali katika eneo hili ni pamoja na kuharakisha upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa, kuanzishwa kwa taasisi ya kuratibu taarifa sahihi za waombaji wa mikopo (credit reference bureau ) ambayo itakuwa inahifadhi taarifa sahihi za wakopaji (credit reference databank); na mwisho, kuhamasisha mashirika ya umma, sekta binafsi na mifuko ya hifadhi ya jamii kuongeza fursa za ajira katika maeneo yao kwa kuwekeza katika vitega uchumi na kutoa mafunzo ya kujiajiri kwa vijana wasio na ajira.
10. Mheshimiwa Spika, ni matarajio yangu kwamba hatua hizi zitasaidia kuleta unafuu na hivyo kupunguza gharama za maisha kwa wananchi na kuboresha uchumi kwa ujumla. Serikali inaomba ushirikiano wa kila mmoja wetu ili hatua hizo zilete matokeo yanayotarajiwa.
HOTUBA KAMILI INGIA HAPA
0 comments:
Post a Comment