Nafasi Ya Matangazo

January 08, 2025

Arusha, 08 Januari, 2025
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ina jukumu la kukadiria, kukusanya na kuhasibu mapato ya serikali kuu. Katika hali ya kutambua mchango mkubwa wa walipakodi, TRA imekuwa na utamaduni wa kuwashukuru na kuwapongeza walipakodi na wadau wetu kutokana na mchango wao mkubwa wa kulipa kodi au kurahisisha ulipaji wa kodi.
 
TRA tumetenga tarehe 23 Januari, 2025 kuwa siku maalumu ya kutambua na kutoa shukrani na tuzo kwa Mlipakodi waliotekeleza wajibu wao wa kisheria kwa hiari kwa mwaka 2023/2024.
 
Lengo la kutoa tuzo hizi ni kutambua juhudi za walipakodi na kuunga mkono taasisi/watu binafsi waliowezesha TRA kukusanya kodi kwa urahisi. Walipakodi watakaotunukiwa ni wale walioonesha mwitikio wa hali ya juu kwa hiari, mchango mkubwa katika ukusanyaji wa mapato, na wasio na rekodi yoyote ya udanganyifu au ukwepaji wa kodi katika kipindi husika. TRA inashirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali kufanikisha malengo yake, na kwa sababu hiyo, wadau wenye kiwango cha juu zaidi cha ushirikiano watapewa tuzo pia.
 
Mwaka huu, jumla ya walipakodi na wadau 1228 watatunukiwa vikombe, ngao, na vyeti kama ishara ya kutambua mchango wao katika kujenga taifa kupitia ulipaji wa kodi kwa hiari au kwa kusaidia TRA kwa njia moja au nyingine katika ukusanyaji wa mapato. Ili kustahili kuchaguliwa kupata tuzo za Mlipakodi, vigezo vifuatavyo ni vimezingatiwa:-
 
      I. Uzingatiaji wa sheria za kodi kwa hiari.
    II.Kulipa kiasi kikubwa cha Kodi au Ushuru kwa mwaka wa fedha                 2023/24.
   III.Ulipaji kodi kwa hiari katika kipindi cha mwaka husika 2023/2024.
  IV. Uzingatiaji wa matumizi ya mashine za VFD/EFD kwa usahihi.
   V. Kuwasilisha ritani za kodi au nyaraka za forodha kwa wakati na                 kwa usahihi.
  VI. Kulipa kodi na ushuru wa forodha kwa wakati na kwa usahihi.
 VII.Kutohusika katika ukwepaji wa kodi na shughuli za udanganyifu.
VIII.Kutoa ushirikiano kwa TRA katika masuala ya kikodi pindi                         inapohitajika
  IX.Kuboresha kiwango cha utendaji kazi katika maeneo yote ya                         uendeshaji.
 
Walipakodi waliotimiza vigezo vilivyotajwa watazingatiwa, mradi kwamba walipakodi hao hawajajihusisha na udanganyifu au ukwepaji wa kodi katika kipindi husika.
 
Aidha, kutakuwepo na vipengele vya washindi wa kitaifa kama vifuatavyo:-
 
1. Walipakodi waliofuata sheria za kodi kwa hiari
2. Walipakodi waliolipa kiasi cha kodi kikubwa kwenye ngazi ya wilaya         au mkoa au kitaifa.
3.Walipakodi waliowasilisha nyaraka sahihi za forodha na kwa wakati.
 
Wakati tunaadhimisha siku ya Shukrani kwa Mlipakodi Mamlaka ya Mapato Tanzania inapenda kutoa wito kwa walipakodi wote kuendelea kulipa kodi stahiki na kwa wakati. TRA pia inawahimiza wafanyabiashara wote kuendelea kutimiza wajibu wao wa  kutoa risiti halali kila wanapouza, na mwananchi kuhakikisha wanadai risiti za EFD, kwani hiyo ndiyo njia pekee inatuunganisha watanzania wote kulipa kodi ya Serikali.
 
“Pamoja Tunajenga Taifa Letu”
  
Richard M. Kayombo
Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano
 
Posted by MROKI On Wednesday, January 08, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo