Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa wito kwa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na masomo ngazi ya Stashahada mwezi Machi mwaka huu katika programu tano za kipaumbele kuchangamkia fursa ya mikopo ili waweze kuwa wanufaika na hatimaye waweze kumudu gharama za elimu.
Wito huo umetolewa Januari 5, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Dk. Bill Kiwia ambapo dirisha la maombi litafunguliwa rasmi Januari 15 na kufungwa Februari 15, huku waombaji ambao si wanufaika na wamedahiliwa kusoma kozi za kipaumbele wakiombwa kutumia vyema siku hizo 30 zilizotolewa kukamilisha maombi yao.
Programu tano za kipaumbele zinajumuisha kozi za masuala yafuatayo:
Kwanza, masuala ya Afya na Sayansi Shirikishi. Hapa inajumuisha kozi za masuala ya Maabara, Meno, Uuguzi, Sayansi ya mazingira na afya na nyingine zinazofanana na hizi.
Eneo la pili la kipaumbele linajumuisha kozi za Ualimu na Mafunzo ya Ufundi. Waliodahiliwa kusomea Ualimu katika masomo ya Fizikia, Kemia, Hisabati, Elimu ya Ufundi kama umeme na Ufundi mwingine wanakaribishwa kuomba.
Eneo la tatu ni Usafiri na Vifaa. Hapa inahusisha kozi za Ufundi na ukarabati wa ndege, Meli, Reli, Usanifu majengo, Usafiri wa majini, Vifaa na nyingine zinazofanana na hizi
Eneo la nne ni masuala ya Uhandisi wa Nishati, Madini na Sayansi ya Ulimwengu. Katika kipaumbele hiki, kozi za masuala ya Nishati ya jua, Mafuta, Gesi, Mazingira, Maji, Mipango Miji, Umeme, Umwagiliaji na kozi nyingine zinazofanana na hizi.
Eneo la Tano na la mwisho ni Kilimo na Mifugo. Wanafunzi waliodahiliwa kusomea masuala ya Chakula na Lishe, Ngozi, Uzalishaji sukari, Mbegu, Mifugo, Umwagiliaji, Misitu, Kilimo, Uvuvi na nyingine zinazofanana na wanakaribishwa kuomba.
Huu ni mwendelezo wa maamuzi yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kupanua wigo wa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu ambapo kwa kuanzia, wanafunzi wa ngazi ya Stashahada wanaosoma kozi za kipaumbele wamekuwa miongoni mwa wanufaika wa mikopo hiyo.
Aidha, katika kipindi cha miaka 20 tangu kuanzishwa Bodi hii, takribani Shilingi Trilioni 8 zimekopeshwa kwa waombaji mbalimbali.
0 comments:
Post a Comment