Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeanza kutumia teknolojia ya kisasa kufanya uchunguzi wa kina wa udongo kabla ya ujenzi wa miradi ya barabara, madaraja na miundombinu mingine hatua inayolenga kuongeza usalama, ubora na uimara wa miradi ili iweze kudumu kwa muda mrefu ikiwemo kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Hatua hiyo inawawezesha wataalamu kupata taarifa za kina kuhusu tabaka za udongo na miamba zilizopo chini ya ardhi hivyo kusaidia kubaini aina ya msingi na mbinu za ujenzi zinazofaa kulingana na mazingira ya eneo husika.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa ziara ya waandishi wa habari katika maabara za TARURA, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Tafiti na Udhibiti Ubora wa Wakala huo, Mhandisi Vincent Lwanda amesema uchunguzi wa udongo ni miongoni mwa hatua muhimu katika kuhakikisha miundombinu inayojengwa inakuwa salama, imara na yenye uwezo wa kudumu kwa muda mrefu.
Amesema TARURA imekuwa ikifanya tafiti kuhusu udongo pamoja na vifaa mbalimbali vinavyotumika katika ujenzi huku taarifa zinazopatikana kupitia vipimo hivyo zikitumika kuwawezesha wataalamu kufanya maamuzi sahihi wakati wa kupanga na kutekeleza miradi.
Ameeleza kuwa TARURA imewekeza takribani zaidi ya shilingi bilioni 2 katika mtambo maalumu unaotumika kuchimba ardhi na kuchukua sampuli za udongo na miamba kutoka kwenye kina cha chini ya uso wa ardhi kwa ajili ya uchunguzi wa kitaalamu.
"Maabara hizi hazitumiki kwa ajili ya barabara pekee, tunawakaribisha wananchi wanaofanya ujenzi waweze kuleta malighafi zao kwa ajili ya kupima ubora", amesema.
Amesema matumizi ya maabara yamechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha ubora wa barabara zinazotekelezwa na TARURA tofauti na awali ambapo baadhi ya barabara ziliharibika muda mfupi kutokana na kutofanyika kwa uchunguzi wa kutosha wa udongo na vifaa.
Amesema kuwa TARURA ina maabara kuu jijini Dodoma pamoja na maabara nyingine 16 katika maeneo mbalimbali nchini ambazo pia zinatoa huduma kwa wananchi, taasisi, wakandarasi na watu binafsi wanaotekeleza shughuli za ujenzi.
Vilevile, amesema wakandarasi wanaotekeleza miradi ya TARURA wanatakiwa kutumia maabara katika hatua mbalimbali za ujenzi huku matokeo ya vipimo yakitumika kama sehemu muhimu ya kuthibitisha ubora wa kazi kabla ya malipo.
Ameongeza kuwa maabara za TARURA zimekuwa na mchango katika kukuza ujuzi wa kizazi kijacho cha wahandisi kwa kutoa fursa kwa wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali nchini kupata mafunzo kwa vitendo.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Vifaa Kitengo cha Tafiti na Udhibiti wa Ubora TARURA Makao Makuu, Emmanuel Kilasi amesema TARURA imepata mtambo mpya "drilling rig" ambao unatumika kuchimba na kutoa sampuli za udongo kwa ajili ya uchunguzi wa hali ya ardhi.
Amesema mtambo huo una uwezo wa kuchukua sampuli za udongo kutoka kina cha mita 200 hadi 300 chini ya uso wa ardhi taarifa zinazopatikana kupitia sampuli hizo husaidia kubaini uwezo wa udongo kubeba mzigo jambo ambalo ni muhimu katika kupanga misingi ya miundombinu mikubwa kama madaraja, barabara na majengo.
Amesisitiza kuwa upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu hali ya ardhi kabla ya ujenzi ni hatua muhimu katika kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji au baada ya kukamilika kwa miradi huku wataalamu wakiwa na uwezo wa kuchagua teknolojia na aina ya ujenzi inayolingana na mazingira ya eneo.
Naye, mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Vivian Mwakabaja amesema mafunzo aliyoyapata katika maabara za TARURA yamemsaidia kuunganisha maarifa anayopata darasani na utekelezaji halisi wa kazi za uhandisi ambapo mafunzo hayo yamemwezesha kujifunza namna ya kupima ubora wa udongo na kubaini uwezo wake wa kubeba mizigo.













0 comments:
Post a Comment